Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza wakati alipotembelea Ofisi za Mamlaka ya Serikali Mtandao katika Kituo cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Serikali Mtandao (eGovRIDC) kilichopo Ndaki ya Sayansi ya Kompyuta, Habari na Mawasiliano - Chuo Kikuu cha Dodoma.
Mkurugenzi Mkuu Eng. Benedict Ndomba akielezea umuhimu wa kuanzishwa kwa Kituo cha Mafunzo ya Utafiti na Ubunifu kinachosimamiwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao.
Baadhi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao wakisikiliza kwa makini maelekezo ya Waziri Mhe. Jenista Mhagama wakati alipotembelea kituo hicho cha Utafiti na Ubunifu.

Na Mwandishi Wetu, Dodoma
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amewataka wanafunzi wanaofanya mafunzo kwa vitendo kutumia fursa waliyoipata vizuri kwa kuwa wabunifu, waadilifu na wazalendo kubuni mifumo ya kimkakati itakayosaidia Serikali kutatua changamoto mbalimbali katika jamii.

Mhe. Waziri amesema hayo tarehe Agosti 10, 2022 wakati alipotembelea Ofisi za Mamlaka ya Serikali Mtandao katika Kituo cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Serikali Mtandao (eGovRIDC) kilichopo Ndaki ya Sayansi ya Kompyuta, Habari na Mawasiliano - Chuo Kikuu cha Dodoma.

Mhe. Waziri Mhagama ameongeza kuwa ujenzi wa kituo cha utafiti utachochea ari ya vijana kujifunza kwa vitendo na kuchangia katika ustawi wa taifa kupitia tafiti mbalimbali zinazofanywa hasa katika utatuzi wa changamoto mbalimbali katika jamii.

na kuibua vipaji ambavyo vitasaidia kuleta maendeleo na kuimarisha mahusiano mazuri ndani na nje ya nchi.

“Ninaitaka Mamlaka ya Serikali Mtandao kutafuta rasilimali fedha na kuweka mpango wa kimkakati wa namna ya kuongeza idadi ya vijana wanaokuja kufanya mafunzo kwa vitendo katika masuala ya TEHAMA ili kuchochea utafiti na ubunifu”, amesema Mhe. Mhagama.

Ameongeza kuwa endapo utafiti na ubunifu utaimarika, Serikali itakuwa na mifumo ya kimkakati na kutakuwa na suala la ukusanyaji wa mapato litakuwa rahisi, mazingira ya uwekezaji na biashara yataimarika, usimamizi wa fedha za umma na utakuwa umeboreshwa na kutakuwa na upatikanaji wa huduma bora kwa umma kwa wakati na kwa gharama nafuu.

Mhe. Mhagama amesema utekelezaji wa mifumo hii uende sambamba na usimamizi wa Sera, Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo iliyowekwa ili kuhakikisha Jitihada za utekelezaji wa Serikali Mtandao zinaonekana na kufikia lengo la kuwa na uchumi wa kidijitali.

Naye Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi ameipongeza Mamlaka ya Serikali Mtandao kwa Juhudi kubwa wanazofanya katika utekelezaji wa jitihada za Serikali Mtandao nchini,

Amesema Mamlaka kupitia wanafunzi hao imefanya kazi kubwa ya utafiti na ubunifu wa mifumo inayowezesha Serikali kutatua changamoto mbalimbali za kisekta na kukuza matumizi ya TEHAMA nchini.

“Nawapongeza Mamlaka, kama Serikali tunatambua mnachokifanya na tunawatia moyo kama nchi tumesogea mbele na tunahitaji kusonga mbele zaidi katika masuala ya TEHAMA”.

Aidha, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao, Eng. Benedict Ndomba amesema suala la Utafiti na Ubunifu ni la msingi na linasaidia kwa kiasi kikubwa kuendeleza jitihada za Serikali Mtandao katika maeneo mbalimbali kama vile ujenzi, usimamizi na uendeshaji wa mifumo na miundombinu ya serikali mtandao.

Eng. Ndomba amesema Mamlaka imefanikiwa kuongeza idadi ya wanafunzi wa mazoezi waliopita katika Kituo hicho kutoka idadi ya wanafunzi 33 katika awamu ya kwanza hadi kufika wanafunzi 72 katika awamu ya pili.


Kwa sasa, Eng. Ndomba amesema Mamlaka imepanga kuongeza uwezo wa Kituo ili kiweze kuchukuwa wanafunzi 300 hadi 500 kwa wakati mmoja ili kuchochea Ubunifu na Utafiti katika utekelezaji wa jitihada za Serikali Mtandao.


Mamlaka ya Serikali Mtandao ilianzisha Kituo cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Serikali Mtandao (e-GovRIDC) mwaka 2019 kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma kwa umma kupitia utafiti na kufanya ubunifu katika maeneo mbalimbali.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...