Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeelezwa kuwa marehemu Faruhani kabla ya kuuwawa na kufukiwa alikuwa amefungwa na kamba ya katani mikononi na kichwani alifungwa plasta.

Daktari bingwa wa magonjwa ya binadamu na vifo vya mashaka, Innocent Mosha ameeleza hayo leo Septemba 26, 2022 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Joyce Minde wakati akitoa ushahidi katika kesi ya mauaji inayomkabili Hemed Ally.

Katika Kesi hiyo, Hemed anashtakiwa kwa kumuua Farihani Maluni na kumzika mbele ya nyumba aliyokuwa akishi iliyoko Ilala Sharif Shamba, Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam.

Akiongozwa na wakili wa serikali Salome Asey kutoa ushidi wake, Dkt. Mosha amedai, Februari 9, 2015 akiwa kwenye eneo lake la Kazi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, alipelekewa taarifa na RCO Ilala ikimtaka kwenda Sharif shamba Ilala kuchunguza mwili wa binadamu unaosadikiwa kufukiwa ndani ya Fensi.

Amedai kuwa alichukua vifaa vyote vya kazi na kuongozana na askari polisi hadi eneo la tukio."Tulifika eneo la tukio majira ya saa sita kasoro mchana na kukuta vijana wakiwa wameishaanza kufukua eneo hilo ambapo kwa urefu walishafukua mita moja na nusu huku upana ukiwa ni mkubwa sana zaidi ya mita tano" amedai Dkt. Mosha.

Ameendelea kudai kuwa, baada ya kufukuliwa kwa eneo hilo, ndani ya shimo walikuta matofali mapya, masalia ya mwili yaliyokuwa yamezungushiwa ndani ya godoro, huku mikono ya masalia yale ya mwili ikionekana kufungwa kwa katani na fuvu likiwa na plasta. Pia amedai walikuta nguo za marahemu ikiwemo, suruali, fulana na nguo ya ndani ambazo ndugu wa marehemu walizitambua.

" Baada masalia ya mwili huo kuonekana wananchi waliokuwepo katika eneo hilo walikuwa na taharuki wakitaka kumpiga mtuhumiwa aliyekuwepo pale na kunifanya nishindwe kufanya uchunguzi mahali pale ikabidi tuchukue yale masalia na nguo hadi Hospitali Muhimbili, ambapo napo tulifika muda ukiwa umeenda sana.

Amedai, Februari 10,2015 ndipo alifanya uchunguzi akiwa na askari pamoja na ndugu wa marehemu walioweza kutambua mavazi ya marehemu ikiwemo fulana ya pinki.

Amedai katika uchunguzi wake alibaini kuwa yale yalikuwa ni masalia kweli ya binadamu kwa kuangalia fuvu, mpangilio wa meno na mifupa michache iliyokuwepo.

Hata hivyo shahidi huyo amedai, haikuwa rahisi kujua chanzo cha kifo cha marehemu ila kutokana na uwepo wa plasta eneo la fuvu nilihisi marehemu aliuwawa kwa kuzibwa mdomoni na kumfanya akose pumzi.

baada ya kutoa ushahidi, Dkt Mosha aliiomba mahakama kupokea ripoti ya uchunguzi kama kielelezo ambapo mahakama imepokea kama kielelezo.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi kesho kutwa, Septemba 28, 2022 itakapokuja kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka inadaiwa Juni mwaka 2014 Hemed Ally aanatuhumiwa kumuua Farihani Maluni eneo la Sharif Shamba ndani ya Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...