Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Mohamed Mchengerwa ametoa pongezi kwa Bondia Mtanzania Twaha Kiduku kwa kumchapa kwa alama za majaji wote watatu (unanimous decision) Bondia Abdo Khaled kutoka Misri, usiku wa Septemba 24, 2022 Mtwara.
Kwa ushindi huo, bondia Kiduku ameweza kutetea ubingwa wake wa UBO Afrika (UBO all Africa Champion) na Mkanda mpya wa ubingwa wa Mabara (UBO Intercontinental).
Hili ni pambano la 20 kushinda kwa Kiduku , akitoka sare 1 na kupoteza 8 akiwa na rekodi ya kucheza mapambano 29.
Mhe. Mchengerwa amefafanua kwamba dhamira ya Serikali kwa sasa ni kutumia michezo kuitangaza Tanzania.
Aidha, ametoa wito kwa wanamichezo kuthamini michezo na kufanya kama kazi inayoweza kubadili maisha yao na kuinua uchumi wa nchi kwa ujumla.
Amesema, Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan itaendelea kusaidia wanamichezo wanaofanya vizuri ili wafike mbali.
Kwa upande wake muandaaji wa pambano hilo Selemani Semunyu ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia kwa mchango mkubwa wa uwekezaji inayofanya kwenye sekta za michezo na sanaa.
Amesema wao kama wadau wataendelea kuonesha vipaji walivyonavyo vijana na kuomba wadhamini kujitokeza kusaidia maandalizi, kwani kwa kutegemea viingilio pekee ni ngumu kukidhi gharama.
"Na Sasa dhamira yetu ni kufanya pambano kubwa Dar es Salaam au mkoa ambao unaweza kusaidia katika kutafuta udhamini wa pambano hilo" amefafanua Semunyu.
Pambano hilo lilipambwa na mapambano ya utangulizi ambayo yalikuwa na mvuto mkubwa kwa wadau hususan pambano baina ya Emmilian Polino (JKT) na Osama Arabi (Mtwara) baada ya bondia chipukizi Osama kuonesha kiwango kikubwa hadi mwisho wa mchezo licha ya kushindwa katika pambano hilo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...