Na Said Mwishehe, Michuzi TV 
ASASI ya AGENDA imeishauri Serikali ya Tanzania na Serikali nyingine za Afrika kuchukua hatua za makusudi kulinda watu wao hasa watoto na akina mama wawazito na wanaonyonyesha kama inavyotakiwa kwenye Mkataba wa Minamata unaolenga kupiga marufuku matumizi ya dawa yenye Zebaki kwa tiba ya meno.
Mwito huo umetolewa leo na maofisa wa Asasi hiyo wakati wakiadhimisha Maadhimisho ya Tiba ya Meno bila Zebaki Barani Afrrika ambayo hufanyika kila ifikapo Oktoba 13 hadi 10 ya kila mwaka  tangu yalipoanza mwaka 2014 ikiwa mwaka huu ni maadhimisho ya tisa.
Akizungumza mbele ya waandishi wa habari leo Oktoba 18, 2022 , Ofisa Programu Mwandamizi wa AGENDA Dorah Swai amefafanua ni vema Serikali za nchi mbalimbali barani Afrika zikachukua hatua za kupiga marufu matumizi ya dawa yenye Zebaki.
“Kama inavyotakiwa na marekebisho ya  Mkataba wa Minamata unaolenga kupiga marufu matumizi ya dawa hiyo kwa watoto na wanawake walio chini ya miaka 15.Hii ni ifikapo mwaka 2023 kama inavyotakiwa pia katika kanuni za Zebaki Tanzania(2020) na Mwongozo wa Pili wa Utoaji wa Huduma za Afya ya Kinywa Tanzania(2020),”amesema Swai.
Ameongeza nyaraka ambazo zimetajwa ni za kuwezesha utekelezaji wa Mkataba wa Minamata nchini Tanzania na zimepigwa marufuku matumizi ua dawa ya Amalgamu kwa makundi ya watu walio na uwezekano mkubwa zaidi kudhurika na dawa hiyo nchini ambao ni pamoja na watoto chini ya miaka 15, wanawake walio kwenye umri wa kuzaa , wajawazito na wanawake wanaonyonyesha.
“Tunatoa rai kwa Serikali kuhakikisha kliniki za meno nchini zinatii zuio la matumizi ya dawa hiyo kwa kuwa dawa mbadala za kuziba meno zisizo na Zebaki zikiwepo Composite resin na Glass Ionomer zinapatikana na zimetumika kwa miongo kadhaa nchini Tanzania na nyingine za Afrika.”
Kuhusu Wiki ya Tiba meno bila zebaki barani Afrika amesema huadhimishwa katika wiki ya terehe 13-20 Oktoba na Asasi ya AGENDA na mashirika mengine yasiyo ya kiserikali zaidi ya 50 barani Afrika yanaadhimisha wiki hii muhimu kwa ajili ya kujikinga dhidi ya madhara yatokanayo na matumizi ya dawa yenye zebaki kwa matibabu ya meno ijulikanayo kama amalgam.
“Maadhimisho ya mwaka huu ni ya tisa tangu kuzinduliwa mwaka 2014 .Kaulimbiu ya mwaka huu ni Tekeleza marekebisho ya mkataba wa minamata ya kupiga marufuku matumizi ya dawa zenye zebaki  kutibu meno kwa watoto  na wanawake wa umri wa kuzaa ifikapo 2023,”amesema Swai.
 
Kwa upande wake Ofisa Programu Mkuu wa AGENDA Silvani Mng’anya amesema uwekezaji wa chujio la dawa hiyo ya kuziba meno(Amalgam) kwenye kliniki za meno ni wa gharama kubwa na ngumu kutekelezeka kwa kuwa taka za amalgam zinaponaswa ndani yake zinapojaa ni lazima chujio lisafirishwe hadi nchi za Magharibi kwa ajili kuondolewa na kuteketezwa kwa namna ambayo haitaleta madhara makubwa zaidi kwa watu na mazingira.

“Baada ya kutumia hizo njia ngumu wamiliki na waendeshaji wa kliniki za meno(za umma na binafsi ) wanapaswa kuelekeza juhudi zao katika kuhimiza matumizi ua dawa za kuziba meno zisizo na Zebaki ambazo ni bora zaidi na hazina hatari kwa afya au kuchafua mazingira,”amesema Mng’anya.

Aidha amesema amalgam imeundwa na mchanganyiko wa zebaki , fedha , bati ,shaba na metali nyinginezo ambapo zebaki ni hadi asilimia 50 kwa uzani.
“Zebaki pindi inapokuwa katika mwili wa mama, mimba na watoto wanaweza kuathiriwa nayo kupitia maziwa ya mama.Pia inaweza kuathiri ukuaji wa ubongo wa mtoto, athari kama hizo zinaweza kusababishwa na kula samaki ambao wameathiriwa na zebaki kutoka kwenye maji yaliyochafuliwa na zebaki iliyotokana na amalgam.”
Amesema baadhi ya dalili za athari za Zebaki ni kuteteka, kutoona na kusikia vizuri , kupooza , kukosa usingizi na kukosa utulivu wa kihisia .Hivyo ametumia nafasi hiyo kuendelea kuiomba Serikali kuendelea kutoa elimu kuhusu usafishaji wa kinywa ili kuondokana na meno kutoboka na kisha kutibiwa kwa kutumia dawa yenye zebaki ambayo madhara yake ni makubwa.
 
Aidha amesema Umoja wa Ulaya, Nigeria na  Zambia tayari zimeondoa matumizi ya amalgam ya meno kwa watoto, wanawake wajawazito na wanawake wanaonyonyesha huku Cameroon ,Madagscar na Benin nazo zilishaondoa matumizi ya amalgam katika hospitali zote , hivyo ni wakati wa nchi zilizosalia za Afrika kuchukua hatua kama hizo.Ofisa Programu Mkuu wa Asasi ya AGENDA Silvani Mng’anya (kushoto) akiwa na Ofisa Programu Mwandamizi wa asasi hiyo Dorah Swai wakionesha Muongozo wa pili wa  utoaji wa huduma za afya ya kinywa na meno Tanzania kwa waandishi wa habari leo Oktoba 18,2022 ambao AGENDA walishiriki kuandaa kwa kushirikiana na Wizara ya Afya wakati wa maadhimisho ya Wiki ya tiba ya meno bila zebaki barani Afrika ambayo ufanyika katika wiki ya terehe 13-20 ya Oktoba kila mwaka .Programu Mwandamizi wa Asasi ya AGENDA Dorah Swai(kulia)akifafanua jambo kwa waandishi wa habari(hawapo pichani) kuhusu mathara yanayotokana na matumizi ya dawa yenye zebaki kwa tiba ya meno kwa watoto na wanawake wenye umri wa kuzaa wakati Maadhimisho ya wiki ya Tiba meno bila zebaki barani Afrika.Kushoto ni Ofisa Programu Mkuu wa Asasi ya AGENDA Silvani Mng’anya.Baadhi ya waaandishi wa habari wakiwa maofisa wa ASASI ya Agenda wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kumalizika kwa mkutano ulioandaliwa na asasi hiyo kwa ajili ya kuzungumzia Maadhimisho ya Wiki ya Tiba ya meno bila Zebaki barani Afrika ambayo huadhimishwa katika wiki ya tarehe 13-20 Oktoba ya kila mwaka.Ofisa Programu Mwandamizi wa Asasi ya AGENDA Dorah Swai(kulia) akimuonesha picha ya jino ambalo limezibwa  na dawa yenye madini yenye zebaki(amalgamu) mwandishi mwandamizi wa gazeti la Nipashe Mary Geofrey .Ofisa Programu Mkuu wa Asasi ya AGENDA Silvani Mng’anya (kushoto) akisisitiza jambo wakati akielezea umuhimu wa Serikali za nchi za Afrika kuhakikisha zinatekeleza makubaliano yaliyopo kwenye mkataba wa Minamata katika kuzuia matumizi ya dawa yenye zebaki kutibu meno kwa watoto na wanawake wanawazito na wanaonyonyesha.(PICHA ZOTE NA SAID MWISHEHE)
 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...