Na Mwandishi Maalum – Dar es salaam

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imeanzisha kliniki ya matibabu ya moyo inayoanza saa kumi jioni hadi saa mbili usiku ili kutoa nafasi kwa wagonjwa walioshindwa kufika kliniki za asubini kupata huduma.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kliniki hiyo jana jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema kuanzishwa kwa kliniki hiyo kumelenga kuboresha utoaji wa  huduma bora kwa wagonjwa wanaotibiwa katika Taasisi hiyo.

Dkt. Kisenge alisema kuna wagonjwa ambao wanashughuli nyingi wakati wa asubuhi na pia baadhi ya wazee wanashindwa kuamka alfajiri kwa ajili ya kuwahi  kliniki lakini kuwepo kwa kliniki ya jioni kutawasaidia wagonjwa wote kupata muda wa kuhudhuria kliniki zao.

“Tumeanzisha Kliniki mpya ya matibabu ya moyo ambayo itakuwa inaanza saa kumi hadi saa mbili usiku lengo likiwa ni kuwasaidia wagonjwa ambao wanataka kupata huduma za matibabu ya moyo wakati wa jioni,”.

“Taasisi yetu imekuwa ikipata wagonjwa takribani 400 kila siku na wengine wengi wanahitaji kupata huduma za matibabu lakini hawapati kwasababu wanakosa muda na nafasi ya kutibiwa katika siku husika, hivyo basi tumeona tuendelee kuimarisha  huduma na kuwasaidia hasa wazee ambao wanashindwa kuamka asubuhi na kuwahi kliniki,” alisema Dkt. Kisenge.

Dkt. Kisenge alisema kuwepo kwa kliniki ya jioni kutatoa fursa kwa wagonjwa wa moyo ambao wanafanya kazi za kuajiriwa kwani watapata nafasi ya kwenda kazini na baada ya majukumu yao ya kazi watafika  katika taasisi hiyo kwa ajili ya  kupatiwa huduma katika kliniki ya jioni.

“Tunaendelea kuboresha huduma zetu na sasa tutakuwa tunawafuata wananchi mahali walipo ambapo tumejipanga kuzunguka zaidi ya mikoa 15 ili tuweze kuwapatia huduma za matibabu ya moyo na kutoa elimu kwa madaktari walioko mikoani ili na wao waweze kuwabaini na kuwapatia huduma wagonjwa wetu moyo”, alisema Dkt. Kisenge.

Akizungumzia kuhusu kliniki hiyo Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo aliyebobea katika kutoa huduma za vipimo vya moyo Henry Mayala alisema kliniki hiyo ya jioni itatoa fursa pia kwa wagonjwa hao kufanyiwa vipimo vya magonjwa ya moyo.

“Siku za nyuma vipimo vya magonjwa ya moyo vilikuwa vinatolewa kwa idadi na wagonjwa wengine kupewa tarehe za kurudi kwa ajili ya vipimo husika lakini kupitia kliniki hii ya matibabu ya moyo inayoanza jioni tutaendelea kutoa huduma za vipimo kwa wagonjwa wengi zaidi,”.

“Kupitia kliniki ya jioni iliyoanzishwa tutaenda kupunguza msongamano wa wagonjwa wetu kwani vipimo vya kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiography-ECHO) na vipimo vya kuangalia mfumo wa umeme wa moyo unavyofanya kazi (Electrocardiography-ECG) vitakuwepo kuanzia asubuhi hadi saa mbili usiku,” alisema Dkt. Mayala.

Kwa upande wa wagonjwa waliohudhuria kliniki hiyo walishukuru kwa kuanzishwa kwa huduma ya kliniki ya jioni ambayo inatoa nafasi kwa wagonjwa wengi zaidi kupata nafasi ya kutibiwa.

“Ninaushukuru uongozi wa JKCI kwa kuanzisha kliniki ya jioni kwani kwa kupitia kliniki hii kutarahisisha upatikanaji wa matibabu hasa kwa watu wazima ambao kuamka asubuhi ni changamoto,”.

“Hapo awali ilitulazimu kufika JKCI alfajiri lakini kutokana na idadi ya wagonjwa kuwa wengi tulijikuta tunakaa hadi jioni lakini kupitia kliniki hii ya jioni tutakuwa tunakuja mchana kupata huduma bila msongamano na kurejea nyumbani kwa wakati,” alisema Omary Chudi.

Halima Mbaga anayetibiwa katika Taasisi hiyo alisema kliniki ya jioni ya matibabu ya moyo inawapa fursa wagonjwa wa moyo kufika JKCI wakati wowote kwa ajili ya kupatiwa huduma za matibabu na vipimo vya magonjwa ya moyo.

Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Henry Mayala akiwaeleza wagonjwa waliohudhuria kliniki ya jioni inayoanza saa kumi jioni hadi saa mbili usiku kuwa huduma za vipimo vya magonjwa ya moyo vitakuwa vinapatikana katika kliniki hiyo.Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akizungumza na wagonjwa wanaotibiwa katika Taasisi hiyo kuhusu Kliniki mpya ya matibabu ya moyo inayoanza saa kumi jioni hadi saa mbili usiku aliyoizundua jana jijini Dar es Salaam.Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akizungumza na mgonjwa aliyehudhuria kliniki mpya inayoanza saa kumi jioni hadi saa mbili usiku wakati wa uzinduzi wa kliniki hiyo uliofanyija jana jijiniDar es Salaam.Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter
Kisenge akimpima shinikizo la damu na kiwango cha oksijeni kwenye damu
mgonjwa aliyehudhuria kliniki mpya ya matibabu ya moyo inayoanza saa kumi
jioni hadi saa mbili usiku wakati wa uzinduzi wa kliniki hiyo uliofanyika jana jijini
Dar es Salaam.Picha na Khamis Mussa


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...