Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Anthony Mavunde amewataka Wakulima wa zao la Mkonge kuongeza tija ya Uzalishaji wa zao hilo kwani Serikali imejipanga kikamilifu kuhakikisha inaweka mazingira bora yatakayomsaidia mkulima wa mkonge kuzalisha kwa tija na kufikia malengo ya kuongeza uzalishaji wa mkonge kufikia tani 120,000 kwa mwaka 2025/26.

Naibu Waziri Mavunde ameyasema hayo jana tarehe 04 Desemba 2022, katika Mkutano wa 3 wa Wadau wa Sekta ya Mkonge uliofanyika jijini Tanga akimwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Kassim M. Majaliwa (MB).

Amesema katika Bajeti ya mwaka huu wa fedha 2022- 2023 Serikali imeongeza bajeti ya utafiti na uzalishaji mbegu bora kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) ili kuongeza uzalishaji wa miche ya mkonge kufikia miche 10,000,000, kuboresha maabara ya kituo cha Utafiti TARI Mlingano, kufanya tafuti juu ya mbegu bora zenye ukinzani wa magonjwa ikiwa ni pamoja na kusambaza matokeo ya tafiti kwa wakulima na kutoa huduma za ugani.

"Moja ya changamoto kubwa inayowakabili wakulima wa mkonge ni upungufu wa makorona unaopelekea mkonge kuvunwa mara moja kwa mwaka badala ya mara mbili, na hivyo kusababisha hasara kubwa kutokana na mkonge kuozea shambani. Katika Bajeti ya mwaka wa fedha 2022 - 2023 Serikali imepanga kununua Korona tatu (3) za kuchakata Mkonge Ili kuwawezesha wakulima kuongeza uwezo wa kuchakata mikonge yao pindi wakivuna na kuepusha kuozea Mashambani".

"Sambamba na hilo, Serikali imeweka utafiti wa mbegu na mbinu bora za kilimo kama kipaumbele cha kimkakati cha kwanza, lengo ni kuhakikisha wakulima wanazalisha kwa tija na kunufaika na jasho lao. Kupitia TARI Mlingano, jitihada kubwa zimeendelea kuelekezwa katika kuongeza uzalishaji kwa wingi wa mbegu bora ya mkonge ili wakulima wengi waipate kiurahisi, wapande kwenye mashamba yao na kuongeza tija" alibainisha Mhe. Mavunde.

Vilevile, katika kuhakikisha tija ya uzalishaji inaongezeka kwa wakulima, Mavunde alibainisha kuwa Serikali inaendelea na uboreshaji wa maabara za udongo na tissue culture katika Kituo cha TARI Mlingano, lengo ni kutambua mahitaji ya virutubisho kwenye udongo na kuongeza kasi ya uzalishaji wa miche bora ya mkonge kupitia teknolojia ya tissue culture.

Pia, Mhe. Mavunde  ameitaka Bodi ya Mkonge kushirikiana na wadau wote kwenye mnyororo wa thamani kuweza  kubuni bidhaa mbalimbali zinazotokana na mkonge kama vifaa vya ujenzi, bidhaa mbadala wa mbao, sukari ya mkonge, pombe ya mkonge, karatasi maalum, bio gas, mbolea na chakula cha mifugo. Hatua hiyo, itapelekea kuongeza thamani ya zao la mkonge kwa kumnufaisha mkulima kupitia bei nzuri na pato la taifa kwa ujumla.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Mavunde amezitaka Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB) na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), kukaa pamoja na kujadiliana aina ya vifungashio wanavyovitumia, ujazo wake pamoja na ubora ili Bodi ya Mkonge iweze kusimamia utengenezaji wa vifungashio na kuongeza wigo wa soko la mkonge Nchini.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mheshimiwa Omary Mgumba alimshukuru Naibu Waziri kwa ujio wake na kushauri kwamba ufanisi na tija ya uzalishaji wa zao la mkonge unaendana moja kwa moja na umiliki wa mashamba na makorona, na hivyo kuipongeza Wizara ya Kilimo kwa kuja na hatua ya kununua korona 3 ambazo zitakwenda kuongeza tija kwa wakulima kwenye AMCOS zao ambao wanamiliki mashamba na kukosa makorona kwa ajili ya uchakataji.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...