Na Mwandishi Wetu Michuzi TV

MWENYEKITI wa Bodi ya Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana(CMSA) Dk.John Mduma amesema shindano linalohusu masoko ya mitaji kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu, ambapo Mamlaka ya Masoko  wanatarajia washiriki wapatao 18,000 watashiriki Shindano hilo.

Akizungumza wakati akizindua Shindano hilo ambalo limeandaliwa na CMSA Dk.Mduma amesema hatua hiyo ni muhimu kwani inatarajiwa kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu fursa zinazopatikana katika masoko ya mitaji huku akieleza shindano hili ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Jumuishi wa Huduma za Kifedha wenye lengo la kuongeza ushiriki wa wananchi kwenye sekta rasmi ya fedha.

"Shindano hili ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha 2019/20 – 2029/30” wenye lengo la kuwezesha upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya kujenga uchumi shindani kwa maendeleo ya watu.Natoa pongezi kwa Uongozi wa CMSA kwa kuandaa shindano hili ambalo linafunguliwa leo Desemba 7,2022.

"Na linatarajiwa kufungwa Machi 31, 2023. Ninatambua kazi hii haikuwa ndogo na rahisi lakini mmeweza kufanya kazi yenu vizuri na hivyo kufanikisha hatua hii kwa weledi na kwa ufanisi mkubwa.Ninanipongeza Mamlaka kwa kubuni shindano ambalo linatoa fursa ya ushiriki wa wanafunzi wote Tanzania, ikiwa ni Tanzania Bara na Visiwani, kwa kuwa shindano hili linatumia teknolojia ya mawasiliano ya mtandao kwa njia ya simu za mkononi, tovuti, na barua pepe,"amesema Dk.Mduma.

Aidha,amesema anatambua shindano hilo limeweza kuvutia Mamlaka za Masoko ya Mitaji kutoka Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika kuweza kutembelea Tanzania na kujifunza jinsi ya kuendesha mashindano kama haya katika nchi zao na kwamba anatarajia zawadi ambazo Mamlaka itatoa kwa washindi wa shindano hili, zitakuwa chachu kwa wanafunzi wengine kushiriki katika mashindano kama haya katika siku za usoni.

Amesema miongoni mwa zawadi zitakazotolewa ni kwa washiriki wavulana 6 na wasichana 6 wenye alama za juu, kufanya ziara za kutembelea maeneo mbalimbali ili kujifunza zaidi maswala ya masoko ya mitaji ikiwa ni pamoja na masoko ya hisa na kampuni kubwa zinazohusika na utoaji huduma katika masoko ya mitaji hapa nchini na nje ya nchi.

"Ninatarajia mafunzo kutokana na ziara hizo yatasaidia kujenga ujuzi wa washiriki katika masoko ya mitaji na uchumi hapa nchini. Aidha, wanafunzi ambao watapata fursa ya kupata ziara za mafunzo, watakuwa mabalozi bora wa masuala ya masoko ya mitaji kwa wanafunzi wengine, kwa kutoa elimu na ujuzi kwa wanafunzi katika vyuo vikuu, elimu ya juu na umma kwa ujumla.

"Ninatambua wanafunzi waliopatiwa mafunzo katika shindano lililopita wamepata fursa ya kufanya kazi katika kampuni kubwa za Kimataifa zinazotoa huduma za ushauri katika masuala ya fedha, kodi na uwekezaji. Aidha ninatambua kwamba baadhi yao wameanzisha kampuni ambazo zimepata leseni ya kutoa huduma katika masoko ya mitaji na wengine wameanzisha jukwaa la utoaji wa elimu ya uwekezaji kwa vijana yaani Young Investors Forum."

Pia amesema anatambua uwepo wa wanafunzi washindi wa shindano hilo kwa miaka iliyopita ambao wameweza kuendeleza ndoto zao za kushiriki kwenye soko la hisa na hivyo kutumia sehemu ya fedha zao walizopata kama zawadi kununua hisa za kampuni mbalimbali zilizoorodheshwa kwenye Soko la Hisa.

"Hawa sasa wamekuwa wawekezaji halisi na sio kwa kusoma tu. Napenda kuwapongeza na ni mfano wa kuigwa. Hawa pia, leo tumewakabidhi vyeti vya umiliki wa hisa zao walizonunua kwa fedha za zawadi ya ushindi na wengine wameongezea zaidi ya hizo. Natoa rai kwa washiriki wa mwaka huu kuiga mfano huu bora sana wa kuwa wawekezaji halisi katika masoko ya mitaji.

"Pia ninatoa rai kwa Mamlaka iweze kuweka mikakati ya kuboresha mpango kazi wake wa kutoa elimu kwa umma kwa kufikia makundi mbalimbali mijini na vijijini na kuongeza utoaji huduma zaidi ili kuwezesha kutekeleza malengo ya Mamlaka ya kuendeleza na kusimamia masoko ya mitaji hapa nchini,"amesema Dk.Mduma

Aidha anatambua mafunzo hayo sasa yanaendeshwa kwa ushirikiano baina ya Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana na Taasisi ya Kimataifa ya Uwekezaji na Dhamana yaani Chartered Institute for Securities and Investment (CISI) ya mjini London nchini Uingereza. Mafunzo hayo yameonyesha chachu kubwa katika kuongeza ujuzi na ueledi kwa wahitimu wa mafunzo haya unaowawezesha kukabiliana na kasi ya mabadiliko ya maendeleo ya sekta ya masoko ya mitaji ulimwenguni.

Hivyo ni matumaini yake Mamlaka itaendelea kudumisha ushirikiano huu, kwani unawaweka wataalamu wanaohitimu mafunzo haya kuwa ni miongoni mwa wataalamu wanaotambulika kimataifa, na hivyo kuwezesha wawekezaji wa kimataifa kuongeza imani juu ya masoko ya mitaji hapa nchini.

Pia amesema Serikali kupitia Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana ina jukumu la kusimamia, kuratibu na kuendeleza sekta ya masoko ya mitaji hapa nchini. Sekta hiyo ni muhimu katika upatikanaji wa mitaji ya muda mrefu kwa kampuni na husaidia umilikishaji kwa umma wa njia za uchumi, hivyo kuchangia utekelezaji wa miradi ya maendeleo na ukuaji wa uchumi wa nchi yetu.

" Hivyo ni imani yangu kuwa ninyi mliotunukiwa vyeti siku ya leo mtatoa mchango mkubwa katika kufanikisha azma ya Serikali ya ujenzi wa uchumi wa viwanda nchini. Niwahakikishie Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi madhubuti wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, iinathamini na inatambua sana juhudi zenu za kuongeza uelewa wa masoko ya mitaji na kuwawezesha wananchi kiuchumi na kijamii."

MWENYEKITI wa Bodi ya Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana(CMSA) Dk.John Mduma akizungumza jana jijini Dar es Salaam wakati akizindua shindano linalohusu masoko ya mitaji kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu, ambapo Mamlaka ya Masoko  wanatarajia washiriki wapatao 18,000 watashiriki Shindano hilo.

MWENYEKITI wa Bodi ya Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) Dk.John Mduma akipongezwa na Ofisa  Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) CPA Nicodemus Mkama mara baada ya kuzindua shindano linalohusu masoko ya mitaji kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu, ambapo Mamlaka ya Masoko  wanatarajia washiriki wapatao 18,000 watashiriki Shindano hilo.

MWENYEKITI wa Bodi ya Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana(CMSA) Dk.John Mduma (wa tatu kulia) akibonyeza kitufe kuashiria uzinduzi wa   shindano linalohusu masoko ya mitaji kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu, ambapo Mamlaka ya Masoko  wanatarajia washiriki wapatao 18,000 watashiriki Shindano hilo.





 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...