WAZIRI wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Nassor Mazrui na ujumbe wake, watembelea Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Binadamu (NIMR) jijini Dar es Salaam hivi karibuni na kufanya Mazungumzo ya Menejimenti ili kujadili na kukubaliana maeneo stahiki ya ushirikiano katika tafiti za afya.

Katika ziara hiyo Mhe. Mazrui aliambatana na Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Utafiti wa Afya ya Zanzibar (ZAHRI), Profesa Mohammed Sheikh, baadhi ya wajumbe wa bodi hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa ZAHRI Bi Mayassa S. Ally na Watumishi wanaowakilisha Wizara ya Afya-Zanzibar.

Akitoa salam zake kwa Menejimenti ya NIMR wakati alipokutana nao Mhe. Mazrui ameipongeza na kuishukuru NIMR kwa ushirikiano inaoutoa kwa ZAHRI, kwani umeiwezesha taasisi hiyo kujifunza mengi katikakuimarisha mifumo yake ya utendaji kazi na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya utafiti wa afya -Zanzibar.

“Zanzibar ni eneo zuri la utafiti kwa maeneo yenye changamoto ya afya ya jamii, tunawakaribisha NIMR kuja Zanzibar kwa kuhamia, ili kushirikiana kwa ukaribu na ZAHRI katika kazi za utafiti zinazoweza kutekelezwa kwa pamoja.” Alifafanua Mhe. Mazrui.

Kikao hicho baina ya Waziri wa Afya Zanzibar, NIMR na ZAHRI kilitanguliwa na uwasilishaji wa taarifa kuhusu uanzishwaji wa NIMR, majukumu yake na maeneo mbalimbali ya utekelezaji wa miradi ya utafiti wa afya ambapo Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi, Profesa Said Shehe Aboud aliiwasilisha.

Uwasilishaji wa taarifa hiyo ulifuatiwa na mjadala ulioangalia namna bora ya kuimarisha ushirikiano katika kazi za utafiti ambapo maeneo ya ushirikiano yalibainishwa na washiriki.

Mjadala huo ulihitimishwa kwa kutia saini Mkataba wa Ushirikiano baina ya ZAHRI na NIMR, tukio ambalo lilishuhudiwa na Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe Mazrui na Wanasheria wa taasisi hizo mbili.

Mkataba huo unalenga kuimarisha ushirikiano katika tafiti za afya, shughuli za Maabara, Mafunzo kwa Watafiti na kuibua programu za kubadilishana uzoefu na teknolojia katika utendaji wa kazi za utafiti wa afya.

Kwa Upande wake Mkurugenzi wa Kuratibu na Kukuza Utafiti –NIMR, Dkt. Paul Kazyoba amesema maeneo ya ushirikiano yatahusisha tafiti za magonjwa mbalimbali yakiwemo magonjwa ya Saratani, Afya ya Mama na Mtoto, figo, Changamoto zitokanazo na Korona (UVIKO-19), Ufuatiliaji wa Maralia, Magonjwa ya Ngozi na magonjwa yasiyoambukiza.
Walioketi Pichani wakitia saini Mkataba huo wa Ushirikiano wa miaka mitano, baina ya ZAHRI na NIMR ni Mkurugenzi Mkuu wa NIMR Profesa, Said Shehe Aboud (kushoto) na Mkurugenzi Mkuu wa ZAHRI Dkt. Mayassa S.Ally. Waliosimama wakishuhudia ni Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Nassor Ahmed Mazrui (Katikati), Anna Julia Kimwaga-Meneja-Huduma za Sheria NIMR (Kulia) na Amina M. Jabir Katibu wa Bodi ya ZAHRI (kushoto).
Mkurugenzi Mkuu wa NIMR Profesa, Said Shehe Aboud (kushoto) na Mkurugenzi Mkuu wa ZAHRI Dkt. Mayassa S.Ally wakionesha mkataba wa ushirikiano baina ya ZAHRI na NIMR katika shughuli mbalimbali zikiwemo za utafiti katika Sekta ya afya.

Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Nassor Ahmed Mazrui (mwenye miwani katikati) akifafanua jambo wakati alipotembelea Maabara ya Vinasaba ya NIMR inayoendeshwa kupitia Mradi wa Utafiti wa Ufuatiliaji wa Malaria kwa kutumia mbinu za Vinasaba (Molecular Surveilance of Malaria in Tanzania-MSMT) wa kwanza kulia ni Mtafiti Mkuu Kiongozi wa Mradi Dakta Deus Ishengoma.
Baadhi ya Wajumbe wa Bodi ya ZAHRI na Watumishi wa Wizara ya Afya Zanzibar wakipata maelezo kuhusu Maabara ya Vinasaba ya NIMR na utendaji kazi wake katika tafiti za Malaria nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa NIMR, Profesa Said Shehe Aboud akizungumza wakati wa ziara kwa Mhe. Mazrui na ujumbe wake, mara baada ya kupokelewa katika Taasisi hiyo. Profesa Aboud aliambatana na baadhi ya Wajumbe wa Menejimenti ya NIMR.
Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Mazrui akizungumza na Watumishi walioshiriki katika kikao hicho.
Mkurugenzi wa Kuratibu na Kukuza Utafiti NIMR Dkt. Paul Kazyoba akiratibu zoezi la utambulisho wa Watumishi walioshiriki kikao hicho kutoka Wizara ya Afya Zanzibar, ZAHRI na NIMR. Aliyeketi ni Msaidizi wa Waziri wa Afya Zanzibar, Abdalla Iddi Masoud.
Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Nassor Ahmed Mazrui aliyeketi katikati akiwa katika picha ya pamoja na Watumishi wa NIMR, ZAHRI na Wizara yake ya Afya Zanzibar, baada ya kukamilisha ziara yake NIMR.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...