NAIBU Waziri Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Deo Ndejembi amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kutilia mkazo miradi yote inayotekelezwa na TASAF kwenye halmashauri zao ili kuepusha matumizi mabaya ya fedha.
Ndejembi ametoa agizo hilo wakati wa ziara yake ya kukagua miradi inayotekelezwa na TASAF katika Mkoa wa Geita alipotembelea miradi ya elimu na afya katika Wilaya za Chato na Geita ambapo pia amewasimamisha waratibu wa TASAF wa Halmashauri ya Geita Mji na Halmashauri ya Wilaya ya Geita.
" Ninatoa maelekezo kwa Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kuweka mkazo mkubwa kwenye usimamizi wa miradi ambayo TASAF inaitekeleza kwenye halmashauri zao, haiwezekani miradi mingine wanaisimamia vizuri inakamilika lakini ya TASAF inatelekezwa utadhani siyo ya Serikali.
Mkoa wa Geita umepata zaidi ya Sh Bilioni 2 kutoka kwenye fedha za OPEC ambazo Rais Dkt Samia Suluhu Hassan amezitafuta Kwa ajili ya wananchi wa Mkoa huu, sasa kama Wizara hatutovumilia kuona fedha hizi hazitumiki kama ambavyo zielekezwa, niwatake Wakurugenzi kujitathmini kwenye utekelezaji wa miradi hii.
Tulishatoa maelekezo Wakurugenzi wateue waratibu wa TASAF ambao watashughulika na TASAF tu na siyo kazi nyingine, matokeo yake wanakaidi unakuta Mratibu wa TASAF pia ni Afisa Biashara jambo ambalo linasababisha miradi hii mikubwa ikose usimamizi mzuri, sasa hatutovumilia tena uzembe utakaofanywa na halmashauri kwenye miradi hii," Amesema Ndejembi.
Ndejembi pia amewasimamisha katika majukumu yao Waratibu wa TASAF wa Halmashauri ya Geita Mji na Halmashauri ya Wilaya ya Geita huku pia akimtaka Mratibu wa Mkoa kujitathmini. Ametoa maelekezo hayo baada ya kutoridhishwa na kasi na utekelezaji wa miradi hiyo.
" Ninaelekeza pia Waratibu wa TASAF Geita Mjini na Halmashauri ya Wilaya ya Geita nao warudi kwenye majukumu yao na Wakurugenzi teueni watu wengi na nipate nakala zao, sijaridhishwa na kasi ya miradi yenu hivyo natoa wiki mbili muikamilishe na Februari 13 nitarejea kukagua tena.

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...