HIFADHI ya Gesimasowa yenye ukubwa wa kilometa za mraba zaidi ya
760 ambayo ipo katika Halmashauri ya Madaba Wilaya ya Songea mkoani
Ruvuma ni miongoni mwa vivutio adimu vya utalii ambavyo havifahamiki na
wengi.
Hifadhi hiyo ilianzishwa kama msitu wa hifadhi mwaka 1975 na Mkuu wa
Mkoa wa Ruvuma wa wakati huo, Hayati Dkt.Lawrence Gama.
Mwaka 2015,Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma katika kipindi hicho hayati Said
Mwambungu alisimamia mchakato wa kupandisha hadhi msitu huo na
kuwa hifadhi.
Moja ya vivutio vilivyopo katika hifadhi hii ni mapumziko ya ndege maarufu
duniani anayeitwa tandawili machaka (Derhams) wenye uwezo wa kuruka
toka bara moja hadi bara jingine,ndege hao wanazaliana katika Hifadhi ya
Taifa ya Kitulo iliyopo Makete mkoani Njombe.
Afisa Maliasili na Utalii wa Mkoa wa Ruvuma Afrikanus Challe anabainisha
kuwa utafiti umebaini kuwa ndege hao wanapumzika ndani ya hifadhi hiyo
kwa miezi kadhaa kisha wanaendelea na safari kupitia Bonde la ufa hadi
ziwa Nyasa hatimaye wanasafiri hadi nchini Afrika ya Kusini na mabara
mengine ya Ulaya na Amerika.
Kulingana na Challe,hifadhi ya Gesimasowa ni mapito ya ndege hao
ambao wanatoka Kaskazini mwa Afrika kuelekea Afrika ya Kusini ambao
wanafuata milima ya Livingstone iliyopo ziwa Nyasa na kwamba ndege hao
pia wanapumzika Mwambao mwa ziwa Nyasa ambako kuna mazingira
ambayo yanavutia ndege hao kuishi.
Hata hivyo Challe anasema,Hifadhi ya Gesimasowa pia ina mfumo wa
ikolojia wa pori la Selous ambalo sasa ni Hifadhi ya Taifa ya Nyerere kwa
kuwa hifadhi hiyo ni mapitio ya wanyamapori wanaotoka katika Hifadhi ya
Taifa ya Nyerere kuelekea Bonde la ziwa Nyasa kupitia pori la Liparamba
hadi Hifadhi ya Niasa nchini Msumbiji na kurudi tena Tanzania.
Anawataja wanyama ambao unaweza kuwaona katika hifadhi ya
Gesimasowa kuwa ni tembo, simba,ndege, nyati, pofu na samaki adimu
duniani aina ya mbelele na mbasa.
Challe anabainisha zaidi kuwa Hifadhi ya Gesimasowa ni maingiliano ya
mito miwili ya Hanga na Lutukira katika Halmashauri ya Madaba ambayo
inatengeneza mto Ruhuhu unaomwaga maji yake ziwa Nyasa.
Anasema Mto Ruhuhu ndiyo mazalia ya samaki aina ya mbelele na mbasa
ambao katika duniani nzima wanapatikana ziwa Nyasa pekee.
“Utafiti umebaini Samaki aina ya mbelele na mbasa ni adimu,wanapatikana
ziwa Nyasa pekee na wanazaliana katika mto Ruhuhu ambao unachangia
asilimia 20 ya maji katika ziwa Nyasa’’,anasema Challe.
Utafiti kuhusu Samaki hao katika mto Ruhuhu na ziwa Nyasa ulifanywa na
Mtafiti Fransis Challe mwaka 2010 ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu
Huria cha Tanzania kitivo cha Sayansi,Teknolojia na Mazingira na
chapisho la utafiti huo lilitolewa mwaka 2011.
Hata hivyo uchunguzi umebaini kuwa wavuvi katika ziwa Nyasa wanafanya
uharibifu wa mazingira katika eneo la Folkland Lituhi kwenye maingiliano
ya mto Ruhuhu na ziwa Nyasa hivyo wanaharibu vifaranga wa samaki
ambao wanaingia katika ziwa Nyasa.
Challe anasisitiza eneo la maingiliano ya mto Hanga na Mto Lutukira ndani
ya Hifadhi ya Gesimasowa linatakiwa kulindwa na kuhifadhiwa kwa
sababu Samaki aina ya mbasa na mbelele wanazaliana kwenye Maingilio
ya mito hiyo,kisha wanasafiri hadi ziwa Nyasa na kuendelea na Maisha.
Anasema wakati wa kuzaliana samaki hao wanarudi tena kwenye maingilio
ya Mto Hanga na Mto Lutukira,hivyo hifadhi ya Gesimasowa ni eneo
muhimu kitaifa na kimataifa katika Uhifadhi na utalii kwa kuwa ndiyo eneo
pekee duniani ambako Samaki jamii ya mbasa na mbelele wanazaliana.
Hata hivyo anasema hifadhi ya Gesimasowa,bado ni mpya na kwamba
lengo la serikali ni kuhakikisha kuwa maliasili zilizopo katika hifadhi hiyo
zinalindwa ili ziwe endelevu kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Kulingana na sheria ya wanyamapori namba tatu ya mwaka 2009
wananchi hawaruhusu kufanya shughuli zozote ndani ya hifadhi hizo,hivi
sasa wanyamapori wanahama toka Hifadhi ya Taifa ya Nyerere,wakipitia
hifadhi ya Gesimasowa,hifadhi ya Litumbandyosi, Pori la Liparamba na
kuvuka mpaka hadi hifadhi ya Niassa nchini Msumbiji.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas anasema ana utaja
Mkoa wa Ruvuma kuwa una fursa nyingi za utalii wa kitamaduni na ikolojia.
Anavitaja baadhi ya vivutio hivyo kuwa ni hifadhi ya Taifa ya Nyerere,Pori
la akiba Liparamba,Mto Ruvuma,Ziwa Nyasa,Makumbusho ya Taifa ya
Majimaji, hifadhi ya Mwambesi,Jiwe la Mbuji,hifadhi ya Ruhila,hifadhi ya
Gesimasowa na vivutio vingine vingi.
Milima ya Livingstone wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma moja ya maeneo ambayo yanamvutia ndege tandala machaka ambaye pia hupumzika kwenye safu za ilima hiyo akiwa safarini kuelekea Afrika ya Kusini
Ndege anayeitwa tandawala machaka mwenye uwezo wa kusafiri toka bara moja kwenda bara nyingine hupumzika katika hifadhi ya Gesimasowa iliyopo Hallmashauri ya Madaba wilaya ya Songea mkoani Ruvuma
Jamii ya samaki aina ya mbasa na mbele ambao wanapatikana katika mto Ruhuhu na ziwa Nyasa pekee
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas alipotembelea milima ya Matogoro Manispaa ya Songea ambayo ni chanzo cha mito mikubwa miwili ambayo ni Mto Ruvuma unaomwaga maji yake Bahari ya Hindi na Mto Ruhuhu unaomwaga maji yake ziwa Nyasa
Maingilio ya mto Hanga na Mto Lutukira ndani ya hifadhi ya Gesimasowa.mito hiyo ikiungana inatengeneza Mto Ruhuhu ambao unamwaga maji yake katika ziwa Nyasa,maingilio ya mito hiyo miwili ni ,eneo ambalo linatumiwa na samaki aina ya mbasa na mbelele kuzaliana



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...