Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), Rais Jakaya Mrisho Kikwete (Pichani akiwa na Rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini, Waziri Mkuu wa Ethiopia Meles Zinawi na Rais Yoweri Museveni wa Uganda) leo amesema kuwa, kimsingi, nchi za Afrika zinakubaliana kuhusu umuhimu wa kuanzishwa kwa Serikali ya Umoja wa Afrika, isipokuwa zinatofautiana kuhusu namna ya kufikia Serikali hiyo.

Amesema kuwawapo wanaotaka Serikali hiyo kuundwa mara moja, na wapo wanaotaka Serikali hiyo kufikiwa hatua kwa hatua.

Akifungua Mkutano wa Siku Mbili wa Kamati Maalum ya Wakuu wa Nchi 12 za AU (Committee of 12) kuhusu uundwaji wa Serikali hiyo leo katika Hoteli ya Ngurdoto, Arusha, Rais Kikwete amesema kuwa mwenendo mzima wa mjadala kuhusu Serikali hiyo unaonyesha kuwa kuna makubaliano ya jumla.

“Tunakubaliana kuhusu lengo kuu la kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Afrika. Tofauti pekee ya msingi ni kati ya wale wanaotaka kuundwa mara moja kwa Serikali hiyo na wala wanaotaka uundwaji wa Serikali hiyo uje hatua kwa hatua,” amesema Rais Kikwete.

Kwa sababu hiyo, amesema Rais Kikwete, ndiyo maana Kamati hiyo inayokutana Arusha inayo kazi kubwa ya kupata mwafaka wa jinsi ya kuwashauri wakuu wengine wa Afrika kuhusu jinsi ya kufikiwa kwa Serikali hiyo.

Mkutano huo unajadili ripoti ya Baraza la Utendaji la Mawaziri wa AU kuhusu uundwaji wa Serikali ya Afrika na kuhusu ripoti ya tathmini iliyofanywa kuhusu shughuli za AU ukiwamo muundo wa umoja huo.

Baraza hilo lilifanya kikao chake hivi karibuni mjini Arusha chini ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe kuandaa kikao kilichoanza leo.

Amesema Rais Kikwete: “Kazi iliyofanywa na Baraza la Utendaji itatusaidia, kwa njia nyingi, katika kufikia mapendekezo ambayo, ni matumaini yangu, kuwa yataunganisha mawazo ya pande hizo mbili na hivyo kupatikana kwa njia zitazouvusha Umoja wa Afrika kuwa Serikali ya Umoja endelevu na imara.”

Mbali na Rais Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa mkutano huo, viongozi wengine wanaohudhuria ni Rais Yoweri Museveni wa Uganda, Umaru Yarâ Adua wa Nigeria, Rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini na Waziri Mkuu wa Ethiopia, Meles Zenawi.

Nchi zinazowakilishwa na mawaziri wa nchi za nje ni Misri , Libya, Cameroun, Senegal, Botswana na Gabon. Ghana inawakilishwa na Mshauri Maalum wa Rais John Kuffour.

Mapema, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Afrika, Jean Ping amesema kuwa ni muhimu kwa baadhi ya mapendekezo Baraza la Utendaji na kamati nyingine kukubaliwa na kikao cha sasa, ili kuweza kuiimarisha AU na hatimaye kuweza kufikia Serikali ya Afrika.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 6 mpaka sasa

  1. AnonymousMay 23, 2008

    Aisee JK Mwambie menzio huyu mwenye unga kichwani akaangalie kinachoendelea huko kwao kwanza halafu ndio afirkirie Taifa la Africa baadaye. La sivyo nasi tulianzisha sasa hivi. Hata sisi tunaweza kuchoma na kuua.

    ReplyDelete
  2. AnonymousMay 23, 2008

    HUYU MHESHIMIWA AMESAHAU KUWA ALISEMA WATU WACHACHE HAWAWEZI KUWAAMULIA WAZANZIBARI KUHUSU SERIKALI YA MSETO, LAZIMA IPIGWE KURA. NILIDHANI ATAZUNGUMZIA UPIGAJI KURA AFRIKA KUHUSU SERIKALI YA UMOJA NA SIO YEYE NA WENZAKE KUTUAMLIA AU KASAHAU HUYU!

    ReplyDelete
  3. AnonymousMay 23, 2008

    tunaomba viongozi wa waafrica mkusanye maoni ya wananchi wenu juu ya kuundwa kwa seriakli ya umoja wa africa msikurupuke tu

    ReplyDelete
  4. AnonymousMay 23, 2008

    Hawa viongozi mi naona wanaota ndoto za mchana! kabla ya kufikiria serikali ya umoja wa kiafrika, inabidi kwanza tumalize migororo ya bara la Afrika, especially kule Darfur, Somalia, Zanzibar, Western Sahara, Congo,Zimbabwe, etc, na pia tuondokane na viongozi madikteta barani Afrika, bila ya kusahau ufisadi kutomezwa! Najaribu kupiga picha tuna serikali ya umoja, na tunatumia sarafu moja, halafu eti Gavana wa Benki anatoe kwa Wapopo! duh akitufisadi huyo tutamkamatia wapi??

    ReplyDelete
  5. AnonymousMay 25, 2008

    Are these folks living on the same planet as the rest of us!?

    ReplyDelete
  6. AnonymousMay 26, 2008

    Suala hilo la Serikali moja ya Afrika lipelekwe kwa wananchi wenyewe ili wapige 'KURA YA MAONI'katika kila nchi.CCM mmesahau utaratibu wetu?Thats why I Like CCM,mkuki kwa nguruwe bwana!Wanasahau haraka sana,its a Pity isn't it!Angalieni CCM isije ikawa MCC!Suruali huna unataka Shati,si vituko hivyo?

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...