Na Mwandishi Maalum,
Kyela, Mbeya
Rais Jakaya Mrisho Kikwete Jumamosi Oktoba 11, 2008) ametawazwa kuwa chifu wa Kabila la Wanyakyusa na amepewa jina rasmi la Chifu Mwangupili.
Rais amepewa heshima hiyo na wazee wa Wilaya ya Kyela, mkoa wa Mbeya, kwenye Uwanja wa Michezo wa mji wa Kyela wakati alipotembelea wilaya hiyo akiwa katika siku ya tatu ya ziara ya Mkoa huo.

Tangazo la Rais Kikwete kuwa Chifu Mwangupili limetolewa kwenye Uwanja wa Michezo wa Kyela mbele ya maelfu ya wananchi ambako pia alivalishwa wazi rasmi la kichifu na kupewa zana nyingine kukamilisha heshima hiyo.

Wazee wa Wilaya hiyo wamesema kuwa wameamua kumpa heshima hiyo Rais Kikwete kwa sababu ya uhodari wa utawala wake na kwamba Chifu Mwangupili alikuwa babu wa Chifu Magombe Mwakyusa ambaye alikuwa chifu wa eneo la Kyela.

Akizungumza mara baada ya kuwa ametawazwa kuwa chifu wa kabila hilo, Rais Kikwete amewashukuru wazee na wakazi wote wa wilaya hiyo kwa uamuzi wake wa kumtunukia heshima ya kuitwa Chifu Mwangupili.

Baada ya hapo, ametumia muda wa kutosha kuelezea utekelezaji wa ahadi za Serikali zake kitaifa na katika wilaya ya Kenya katika maeneo ya elimu, afya, miundombinu na hasa ujenzi wa barabara, uwezeshaji wa wananchi.

Kwa mara nyingine amesisitiza kuwa Serikali Kuu imekuwa inatoa fedha nyingine kwa serikali za mitaa kwa ajili ya maendeleo, lakini mara nyingine fedha hizo zimekuwa hazisimamiwi vizuri na madiwani.

Amesisitiza kuwa ni wajibu wa madiwani kusimamia vizuri fedha hizo ili matunda ya fedha hizo yaonekane katika mabadiliko ya maisha ya wananchi iwe kwa njia ya elimu, afya ama hata miundombinu.

Wilaya ya Kyela imepewa sh bilioni 12 kwa ajili ya kuendeleza miradi mbali mbali wilayani humo kwa mwaka huu.

“Kama ninavyosema kila mara, tunatoa fedha nyingi mno kuliko wakati mwingine wowote tokea tupate uhuru, lakini lazima matumizi ya fedha hizi yasimamiwe na madiwani ambao ndiyo wabunge wetu kwenye ngazi ya Serikali za Mitaa.”

Mapema akipokea taarifa ya wilaya hiyo ya Kyela, Rais Kikwete amewaonya wakazi wa wilaya hiyo kuvusha dawa kutoka Tanzania na kuzipeleka kwa jamaa zao katika nchi jirani ya Malawi.

Kwenye taarifa hiyo iliyotolewa katika eneo la mpakani kabisa mwa Tanzania na Malawi la Kasumulu, ilielezwa kuwa hospitali za wilaya hiyo zimekuwa zinakabiliwa na matatizo makubwa ya sekya ya afya ikiwa ni pamoja na ukosefu wa dawa za kutosha kiasi cha kwamba baadhi ya wakazi wa wilaya hiyo wamekuwa wakitafuta huduma za afya katika wilaya jirani ya Rungwe.
“Naambiwa sasa tatizo limepatiwa ufumbuzi, lakini pia naambiwa kuwa mmekuwa mnachukua dawa katika hospitali zetu na kuzipeleka kwa jamaa zenu Malawi.

“Hapa tunayo matatizo makubwa ya afya. Tunalo tatizo kubwa la malaria. Msipeleke dawa hizo kule nchi jirani ya Malawi. Hawa wajomba wenu kama wanataka kutibiwa wavusheni mpaka na kuwaleta huku,” amesema na kuongeza:
“Watu wa ajabu nyie. Dawa mnapeleka Malawi, halafu nyie mnakwenda Rungwe kutibiwa. Kweli ujanja mwingi huondoa maarufu.”

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...