Mimi nilipokuwa Tanzania majuzi niliwenda hadi shule yangu ya Msingi kumwomba Mwalimu Mkuu vitabu vya zamani, hadithi niliyopewa nilichoka. Ati Waalimu wakuu wa shule za msingi wote walipewa amri toka kwa Waziri wavichome vitabu vya zamani ili kutoa nafasi kwa vitabu vipya.
Huyo waziri mbumbumbu sijui alitamka akiwa amelewa buza ama gongo gani. Kumbuka zile stoo za vitabu zilivyokuwa zimejaa vitabu, vyote vikapigwa kiberiti. Najiuliza, kwa nini hakuwepo mjanja mmoja akahifadhi nakala moja moja?
Nina imani atakuwepo mtu mmoja mmoja aliyeficha kimoja na mwingine kingine na siku moja tutaviona tena na vitauzwa kwa bei nzuri kweli.
Nilipambana na maboksi ya vitabu vya Bibi na Mama kwa kuwa wao walikuwa Waalimu, wakanifahamisha kuwa sitafanikiwa kuvipata kwani wao walikuwa watiifu, hawakuchukua mali ya Shule/Serikali na kuihifadhi kama yao.

Kila mara huwa nakumbuka:Juma na Roza. Someni kwa Furaha, hatua ya tatu.Hadithi za Pazi na Jogoo alivyomning'iniza kichwa chini miguu juu, na ile hadithi ya Mwanamke aliyevalia hereni kubwa kisha akaenda sokoni kuuza bidhaa zake mara mbuzi wakapita wakarusha mguu ndani ya tundu la hereni nayo ikalikata sikio....
Unamkumbuka Kalumekenge alipokataa kwenda shule? Fimbo ikaambiwa imchape Kalumekenge ili Kalumekenge aende shule. Lakini fimbo ikakataa kumchapa Kalumekenge aliyekataa kwenda shule. Moto ukaambiwa uichome fimbo ili fimbo imchape Kalumekenge ili Kalumekenge aende shule. Lakini moto ukakataa kuichoma fimbo, iliyokataa kumchapa Kalumekenge, aliyekataa kwenda shule. Ndipo maji yakaambiwa yauzime moto, uliokataa kuichoma fimbo, iliyokataa kumchapa Kalumekenge, aliyekataa kwenda shule. Ndipo maji yaka kuuzima moto, moto ukaichoma fimbo, fimbo ikammchapa Kalumekenge, ndipo Kalumekenge akaenda shule.
Unawakumbuka Wagagagigikoko?

Unamkumbuka yule mtoto aliyetumwa kwenda kwa Bibi yake akacheza barabarani hadi simba akamla Bibi yake na kulala kitandani halafu yule mtoto alipofika akamwuliza, Bibi mbona masikio yako makubwa? Bibi akamjibu, ili niweze kukusikia vizuri. Akamwuliza tena, mbona macho yako makubwa? Akamjibu, ili niweze kukuona vizuri. Akamwuliza, mbona meno yako makubwa? Akamjibu, ili niweze kukutafuta vizuri. Ndipo akaiona miguu yake na simba akamrukia na kumla.....

Nikakumbuka na hadithi ya Usiku wa Mbalamwezi, na kabla ya hiyo ilikuwepo hadithi ya Muro na mifugo yake, halafu ilikuweko 'Leo ni Sikukuu' wachilia mbali ile hadithi ya mjukuu aliyekuwa anataka kushindana na babu yake kunywa chai lakini kumbe chai ni ya moto, basi babu yake akawa anatoa sababu ambazo zilikuwa zinaishia na neno 'fu' na kila aliposema 'fu' alipuliza chai 'fu fu fu'....

Mi nilikuwa nasoma na kurudia zile hadithi hadi nyumbani. Bibi kwa vile alikuwa Mwalimu, basi alikuwa akiazima kitabu kwa niaba yang nami nakisoma nyumbani na kukikabishgi ili kirudishwe kabla Ijumaa makusudi nisikose kuazimwa wiki inayofuata.
Nilikuwa nasoma hadi mwisho na nyuma ya kitabu, jalada, kabisa nahakikisha nimesoma kujua kama kitabu kile kina chapa ya MTUU, TPS, Oxford, Longman ama Maximillian Publishing!
Unakumbuka hesabu zilivyokuwa zimepangika kwenye vitabu halafu pembeni zina picha zinazoendana na hisabu yenyewe?

Halafu somo la mwandiko nimemkumbuka mwalimu alikuwa anatufundisha kuumba herufi kwa wimbo, 'chirioooo cha, chirioooo cha....'

Eh jamani! Wametupa jongoo na mti wake! La haula la kwata!
Nasikitika sana mimi lakini najipa moyo kuwa ipo siku tutaviona tena vitabu vyenye hadithi na mafunzo murua...

Golden Days Are Gone?
Aaaarrrrrrrgh!
Memories are made of this!
Subi

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 14 mpaka sasa

  1. Yaani umenikuna kweli, hivi vitabu ni vizuri kwa kujifunza kusoma kaswa kwa watoto wetu wanaoishi nje ya nchi.
    Please let us know ukivipata!

    ReplyDelete
  2. Umenikumbusha mbali saaaaaana. Story make laugh big time. Nimeirudia zaidi ya mara tatu. Damn you make my day.

    ReplyDelete
  3. Jamani yaani wamevichoma. Kweli kuelimika sio kumaliza Phd.

    Yaani nilikua nawaza hizi hadithi kweli na nilikua najiuliza ni wapi nitavipata. Nimegoogle kila kona nikaona tu podcast ya mama na mwana.

    Yaani hivi karibuni najifungua na malengi yangu ni kumsomea huyu mtoto hadithi za kiswahili lakini hata moja sikumbuki. Nikajua nitatuma waninunulie tu kwenye hizo stationaries store kumbe itakuwa tabu kupata hivyo vitabu.

    Nakumbuka kitabu na hadithi tulizokua tunasoma std 2, 3, and 4.

    Kuchoma vitabu kweli sio akili kabisa

    ReplyDelete
  4. Hivyo vitabu mimi nilivitafuta mpaka nikavipata.Kama unavitaka unaweza kuvipata pale St. Joseph's Cathedral.Mimi niliwanunulia watoto wangu kabla sijaondoka.Kwa hiyo kama bado upo Bongo nenda pale, walau najua viwili kati ya hivyo utavipata.
    Mdau, Cardiff

    ReplyDelete
  5. Mdau umenikumbusha mbali sana.
    Nilisoma shule ya msingi Zambia, enzi hizo tukikaa kule, halafu nikaja kusoma sekondari Tanzania.
    Kila mara watu walikuwa wakizungumzia hizo hadithi na mambo ya zamani walipokuwa ktk shule zao za msingi na mimi nikawa sijui wanasema nini. Nilijitahidi wakati niko Sekondari kwenda kununua hivyo vitabu na kuvisoma ili na mimi niwe kama wao wakihadithia mambo yao ya shule za msingi.
    Hivyo vitabu bwana ndo vilikuwa venyewe.
    Hebu sasa toa habari za vitabu vya sekondari tulivyosoma miaka ile ya zamani.

    ReplyDelete
  6. Hivyo vitabu vyote mimi ninavyo kwenye maktaba yangu. Nilijitahidi kuvikusanya wakati ule Mh Mungai alipokuwa Waziri wa Elimu. Maana nilibashiri atakuja kutoa agizo la kuchoma vitabu vyote vya zamani..... na kweli akafanya kweli. Kitu kilicho-nishtua ni kumuona anafuta vitu vya muhimu kwenye mfumo wa elimu, na nikajua kitacho fuata ni kuwa ata-amuru vitabu navyo vichomwe. Alifanikisha kuweka jina lake katika historia ya Tanzania na wa-Tanzania tutamkumbuka kwa mchango wake katika elimu.

    Mdau UK

    ReplyDelete
  7. Kweli umetugusa wengi...umslopagasi je unakumbuka? Manenge na mandawa je? Old good days.....

    ReplyDelete
  8. Kwa kweli mwenzetu umetukumbusha mbali sana sie tuliosoma zamani kwani hata mimi ningebahatika kupata walau vitabu vichache kati ya hivyo ningefurahi sana, je mnamkumbuka Kazimoto, na yule mwingine aliekuwa anagoma kunywea KANGARA home akidai kuwa pombe ya kunywea home sio tamu.AMA KWELI WAHENGA WALISEMA, "UKIPATA CHUNGU KIPYA..."

    ReplyDelete
  9. Umenikuna saana Dasa Subi, siamini kama uhondo huo wa vitabu wanawanyima vizazi vipya!? Ningependa watoto wa kizazi kipaya pia wapate vitabu hivyo. Suala hilo ni hatari na inabidi tujipange ili kuanzisha library binafsi za kuhifadhi vitabu vya zamani. Kama uko tayari tuwasiliane ili tuwahamasishe watu wengine kuanza libeneke hilo...
    agian...you are always the best dada Subiiiiii!
    Shally.

    ReplyDelete
  10. Wadau si hivyo tu napenda kukukumbusha kuwa aliyemla shangazi si simba ni mbwamwitu na akavaa kama shangazi ndio maana mtoto alishangaa akasema shangazi we mbona masikio yako yamekuwa marefu yaani akiwa kavaa kitambaa kapitisha masikioni bado yanachomoza yakimshangaza lakini akajibu nipate kusikia usemayo hiyo haitoshi kuna hadithi za esopo kuna kitabu cha pandora na sanduku aliyefungulia wadudu wakajaa ulimwengu kwa kukiuka alipoachiwa asifungue sanduku na hayo ndio tunaona kwa
    watoto wetu wakikatazwa kitu ndio kwanza tomaso wanataka kujaribu waone kitatokea nini hiyo bado je sultani zuwera ,visa vya majini ,mauguli aliyelelewa na mbwa mwitu kweli nina library ya vitabu vyote vya zamani na hadithi zake nawasimulia wanangu na wengi wanao zipenda kwa hiyo kwa yeyote namkaribisha kwangu apige chapa kila aina ya vitabu vya kiswahili

    ReplyDelete
  11. haya makubwa sasa! Yaani kupata vitabu vipya ndio tuchome vya zamani!? Hata kama havitumiki kama vitabu vya kiada, kuna ubaya gani kuviweka katika maktaba kwa ajili ya ukumbusho na pia kuwapa wanafunzi fursa ya kusoma vitabu tofauti?

    PS: Salamu kwa Juma na Roza

    ReplyDelete
  12. haya makubwa sasa! Yaani kupata vitabu vipya ndio tuchome vya zamani!? Hata kama havitumiki kama vitabu vya kiada, kuna ubaya gani kuviweka katika maktaba kwa ajili ya ukumbusho na pia kuwapa wanafunzi fursa ya kusoma vitabu tofauti?

    PS: Salamu kwa Juma na Roza

    ReplyDelete
  13. Wadau wa blogu ya jamii, heshima kwenu nyote! Nimefurahi mno tena sana kwa maoni yenu hasa kwa kuwa tumekumbushana ya kale. Mmegusa na hadithi ambazo nilikuwa nimezisahau sasa naanza kuzikumbuka tena!
    Mdau, Cardiff: Nimeshafanya utaratibu kumwomba rafiki aliyepo Dar afike St. Joseph's Cathedral Bookshop kuvinunua vitabu.
    Rafiki Shally: tunafurahi pamoja!
    Nitakapovipata vitabu hivyo, naahidi kuvifanyia kazi moja nzuri sana kwa manufaa ya vizazi vijavyo!
    Ama kweli ya kale dhahabu!

    ReplyDelete
  14. Umenikumbusha mbali sana

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...