Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 6 mpaka sasa

  1. Date::2/16/2009
    Bukoba: DC aungwa mkono kwa walimu kuchapwa viboko
    *Polisi wazima mpango wa waalim kuandamana kulaani adhabu hiyo

    Na Lilian Lugakingira


    WAKATI walimu wa mkoani Kagera wamenyimwa kibali cha kuandamana kuunga mkono uamuzi wa Rais Kikwete wa kumvua madaraka mkuu wa wilaya aliyechapa viboko walimu, wakazi wa mjini Bukoba wamedai hatua ya DC huyo ilikuwa sahihi katika kukomesha utoro uliokithiri wakati wa kazi.


    Wakazi hao wanadai kuwa walimu wengi wamejitumbukiza kwenye biashara binafsi tangu waanze kupata mikopo kutoka kwenye mabenki na hivyo kutumia muda wa kazi kwa shughuli zao binafsi badala ya kufundisha.


    Kikwete alimvua madaraka mkuu huyo wa wilaya, Albert Mnali, kwa kosa la kuwachapa walimu. Mkuu huyo alienda kwenye shule tatu za Kansenene, Katerero na Kanazi na kumuamuru koplo wa jeshi aliyeambatana naye kuwachapa walimu hao viboko kwa makosa ya uzembe na kuchelewa kazini.


    Walimu mkoani hapa walikuwa wamepanga kuandamana jana lakini maandamano hayo hayakufanyika kutokana na kutopata kibali cha Jeshi la Polisi, kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa mwenyekiti wa Chama cha Walimu cha Kagera, Dauda Bilikesi.


    Bilikesi alisema kuwa walimu walikuwa wamepanga kufanya maandamano ya amani kulaani kitendo cha mkuu huyo wa wilaya ya Bukoba cha kuwachapa walimu viboko, na kuwa kunyimwa kibali cha kufanya hivyo ni kunyimwa haki yao ya kujieleza na kutoa hisia zao.


    Taarifa kutoka ndani ya jeshi la polisi zimesema kuwa, walimu hao walinyimwa kibali kutokana na kuhofia kuvunjika kwa amani. Hata hivyo, kamanda wa polisi mkoani hapa, Henry Salewi hakuweza kupatikana kuzungumzia suala hilo.


    Wakati walimu wakishindwa kuandamana, wakazi wa wilaya ya Bukoba wanamuona DC Mnali kuwa alifanya kitendo sahihi cha kuchapa walimu viboko, wakidai kuwa utoro, uchelewaji na uzembe umezidi.


    Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti, wakazi hao walisema kuwa adhabu aliyoitoa rais kwa mkuu huyo haistahili, wakisema kuwa walimu hao walistahili adhabu hiyo kutokana na kukithiri kwa vitendo vya utovu wa nidhamu.


    Wakazi hao waliitupia lawama serikali iliyopitisha utaratibu wa walimu kupewa mikopo ambao wamesema umechangia kwa asilimia kubwa walimu kukiuka maadili ya kazi yao, ikiwemo kufanya biashara saa za kazi na kushindwa kufundisha.


    Helleni Lianda, mkazi wa kata Kashai katika manispaa ya Bukoba, alisema kuwa wapo baadhi ya walimu ambao wanafanya kazi zao kwa kufuata misingi na taratibu za kazi, lakini walimu walio wengi wamejiingiza katika biashara na kuwa wanapaswa kuchagua moja, kama kuingia madarasani kufundisha au kufanya biashara.


    “Ni haki yao kupigwa viboko; wanafanya biashara saa za kufundisha; wanafika kazini wakiwa wamechelewa; wanapiga soga kazini badala ya kufundisha. Mimi sioni sababu ya kumwadhibu DC eti kwa sababu kawapiga walimu, ni haki yao,” alisema Lianda.


    Naye Beatrice Mshumbusi, mkazi wa kata Hamugembe, alisema walimu walistahili kuchapwa viboko, akidai kuwa wamekuwa kero hasa kutokana na vitendo vyao vya kulewa saa za kazi, hali inayosababisha wengi wao kuwa wachafu kupindukia.


    Mbali na asilimia kubwa ya watu waliohojiwa kuonekana kumuunga mkono mkuu huyo wa wilaya, wapo baadhi ambao wamesema kitendo cha kuwachapa viboko walimu sio cha kiungwana maana zipo taratibu za kumwajibisha mtumishi wa serikali anayeenda kinyume na taratibu za kazi, sio kumchapa viboko.


    Baadhi ya wazazi walisema wanaandaa maandamano kupinga kitendo cha kumwajibisha mkuu wa wilaya ya Bukoba kwa sababu ya kuwapiga walimu viboko.


    Mzazi mmoja wa Hamugembe aliyejitambulisha kwa jina la Athuman alisema kuwa endapo Jeshi la Polisi litatoa kibali kwa walimu hao kuandamana kuunga mkono uamuzi wa Rais Kikwete, na wazazi wataandamana kupinga hatua hiyo.

    www.mwananchi.co.tz

    ReplyDelete
  2. Hivi mtu akikosa dawa ni kumchapa viboko? Kama siyo basi mbona waalimu wanachapa viboko wanafunzi- ni kwa sababu wanafunzi ni wadogo au wanyonge ndiyo maana wanawachapa wanafunzi? Basi na wao kumbe kwa Mkuu wa Wilaya ni wanyonge kwa hiyo wamechapwa na wao. Kama ni sawa kwa waalimu kuwachapa wanafunzi wakikosa basini sawa na wao kuchapwa wakikosa. Mantiki ya methali ya "Mkuki kwa nguruwe kwa binadamu mchungu" ni ya kukataa unafiki. Waingereza wana metahli isemayo "What is sauce for the goose is sauce for the gander" inayokataa unafiki.

    ReplyDelete
  3. Civil servants ndio wanaoogza kwa uzembe makazini na poor customer service.
    Vyuo vya serikali vya kuwapa mafunzo ya utawala bora na huduma kwa jamii vipo na wanaenda kusoma lakini hamna kitu.

    yaani ukitembelea ofisi za serikalini saa zingine unaweza kujuta kwa huduma utakayopewa. maana mtu anajisikia na nafasi yake aliyonayo hata kama ni askari tuu wa getini, utasema wana mikataba ya kazi adi kufa kwao!!!!

    Naona huyo mkuu wa wilaya ya Bukoba ameona kuwachapa viboko ndio somo peke ili walimu wakumbuke wajibu wao. Maan hata mtoto nae ukimkanya mara 1,2 au 3 hasikii basi kinachofuata ni kumuelimisha kwa vitendo.

    ReplyDelete
  4. Anon wa feb 17, 8:20 umenena kabisa kabisa hivi miili ya watoto hawasikii maumivu au hawajisikii dhalala pale wanapochapwa mboko? tena watoto wengine wakiona viboko vikizidi huwa wanajenga tabia ya kutoroka ili kuwepa fimbo.
    Wazee wanaounga mkono kitendo cha walimu kuchapwa wanaelewa na wanaijua kadhia wanayopata kwa watoto wao kukosa elimu bora kutokana na vitendo vya walimu hao wazembe. Mr Mnali anaelekea alikosa adhabu ya kumfanya mwalimu wale wawajibike sawasawa kwani pia bado anawahitaji, kwa dahabu hiyo aliyoitoa bado anahuruma sana, kwani adhabu ambayo walistahili ni kufukuzwa kazi bali yeye aliona akiwafukuza itawaathiri waliokuwemo na wasiokuiwemo, mpaka panya za nyumbani kwa aliyefukuzwa kazi zitaathirika kwa kukosa msosi humo ndani, hivyo alitafuta adhabu itakayomhusisha mlengwa moja kwa moja , na ni hiyo ya mboko, Wacha wachape walimu wa mishahara hawahitajiki enzi hizi za ushindani, yalikuwa ya zamani kuleana namradi mkono unaenda kinywani, baadhi ya waalimu wamemomonyoka maadili kabisa hawafai na hawatoi mfano mzuri kwa wanafunzi.

    ReplyDelete
  5. Kwa kweli kitendo cha walimu kuchapwa viboko nina kiafiki kweli wamekuwa wazembe mno. Tunalipia gharama watoto wasome wao hutumia muda kwa ajili ya biashara.

    Tena DC ni mnyamahanga anauchungu na watu wa Bukoba wakati sio kwao, hii ni ushujaa anajua historia kuwa mkoa wa Kagera ulikuwa unaongoza kwa ishomile anataka kurudisha historia.

    ReplyDelete
  6. Hao walimu walitakiwa wachapwe na pipili kabisa. Yaani hawafundishi na kazi kuwatuma wanafunzi kufanya mambo yao tu. Tunahitaji watu kama huyu mkuu wa Wilaya ili Tanzania iendelee

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...