wah. wabunge na viongozi wa taasisi mbalimbali wakimsikiliza JK akihutubia
JK akihutubia katika ukumbi wa Kilimani Dodoma

Wazee wa Dodoma wakimsikiliza JK

HOTUBA YA JK WAKATI AKIWAHUTUBIA WANANCHI WA DODOMA, NA WABUNGE KWENYE UKUMBI WA KILIMANI,
DODOMA TAREHE 10 JUNI, 2009


Waheshimiwa Wabunge;
Ndugu wananchi;
Nawashukuru kwa dhati wazee wangu, Waheshimiwa Wabunge na wananchi wenzangu wa Dodoma, kwa kuitikia wito wangu wa kuja kukutana na kuzungumza nanyi. Nakushukuru Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa na Katibu wa Baraza la Wazee kwa maandalizi mazuri.

Mara kadhaa katika hotuba zangu za siku za nyuma, nimekuwa nikielezea jinsi ambavyo uchumi wa dunia unavyopita katika misukosuko mikubwa na jinsi ambavyo mtikisiko huo unavyoweza kuathiri uchumi wetu pia. Tayari athari zake tumezipata na tunaendelea kuathirika nazo.

Nilifanya uamuzi siku za nyuma wa kuunda kikundi kazi cha
watalaam chini ya uongozi wa Gavana wa Benki Kuu, Profesa Benno Ndulu, kufanya uchambuzi wa hali ilivyo ili kubaini athari tulizopata na kushauri hatua za kunusuru uchumi wetu na kujenga uwezo wa kujihami na kukuza uchumi.

Ndugu Wananchi;
Wenzetu hao wamemaliza kazi yao na taarifa yao imeshajadiliwa na Baraza la Mawaziri na maamuzi kufanywa. Matokeo yake ni kuwepo kwa mkakati wa Kunusuru Uchumi wa Tanzania dhidi ya Msukosuko wa Uchumi wa Duniani. Katika mkakati huo mpango wa utekelezaji wa malengo na hatua mbalimbali za kuchukua zimeanishwa.

Mtikisiko Katika Mfumo wa Fedha Duniani
Ndugu Wananchi;
Uchumi wa dunia unakabiliwa na matatizo makubwa sana ambayo hayajawahi kutokea kwa zaidi ya miaka 60. Mara ya mwisho uchumi wa dunia ulikuwa na matatizo makubwa katika miaka 1930 lakini nayo hayakuwa makubwa kama ilivyo safari hii. Matatizo ya uchumi wa dunia yana sura mbili. Upande mmoja lipo tatizo la kuvurugika kwa masoko na mfumo wa fedha wa kimataifa. Na, upande wa pili kudorora kwa uchumi wa dunia
kulikosababishwa na kuanguka kwa masoko ya fedha na mitaji.

Tatizo hili limeanzia Marekani kutokana na udhaifu katika usimamizi wa mfumo wa fedha na hasa mikopo. Baadae ukaenea Ulaya Magharibi na hatimaye dunia nzima na siye tukiwemo. Kiwango cha athari kinatofautiana kutoka nchi moja na nyingine. Mataifa makubwa kiuchumi ya Marekani, Ulaya na Asia yameathirika zaidi kuliko nchi maskini za Afrika. Hata hivyo, mataifa makubwa yana uwezo mkubwa zaidi wa kukabiliana na athari hizo pamoja na ukubwa wake.

Mataifa maskini kama yetu hayana uwezo wa kukabiliana hata na hizi athari ndogo zinazotukabili. Kinachoonekana kidogo kwao, kwetu sisi ni kikubwa.
Mabenki mengi, makubwa kwa madogo, na asasi za fedha kubwa na ndogo katika mataifa tajiri zimeshashuhudiwa zikianguka kibiashara au kufilisika. Masoko ya hisa na mitaji nayo hivyo hivyo yameanguka kwa kiasi ambacho hakijawahi kufikiwa.
Makampuni mengi madogo na makubwa yameanguka. Watu wengi wenye hisa wamejikuta wakiharibikiwa na hata kuwa maskini bila kutazamia. Makampuni mengi yameanguka kibiashara na kufilisika. Watu wamepoteza ajira kwa
mamilioni na wengi wamepoteza nyumba na mali walizozipata kwa mikopo kwa sababu ya kushindwa kulipa mikopo. Kwa ujumla hali ya kiuchumi na kimaisha katika nchi hizo ni ngumu kwa makampuni mengi na watu wengi.

Kutokana na hali hii, uwekezaji umepungua, biashara ya ndani na nje imeshuka, uzalishaji viwandani umepungua sana na kwingine umesimama, makampuni madogo na hata makubwa na yenye heshima yamefilisika, ununuzi wa bidhaa umepungua, watu kwa mamilioni wakakosa ajira katika nchi kubwa kiuchumi. Athari hizo bado zinaendelea na matokeo yake ni kuzorota kwa ukuaji wa uchumi wa mataifa hayo makubwa na uchumi wa dunia kwa ujumla.

Mwaka 2008, uchumi wa nchi hizi ulikua kwa asilimia 0.9. na mwaka huu inatarajiwa utapungua kwa asilimia 3.8. Hali hii imezilazimisha Serikali za nchi hizo kuingilia kati na kutumia fedha za Serikali kuokoa makampuni binafsi, kinyume kabisa na falsafa ya soko huria.

Vilevile, Serikali za nchi hizo zikalazimika kukopa fedha nyingi kwa ajili ya miradi mingi mikubwa ili kuchochea shughuli za kiuchumi.

Athari kwa Tanzania
Ndugu Wananchi,
Kwa upande wetu hapa nchini mabenki yetu yako salama kwa vile hatujafungamanishwa na masoko ya fedha ya kimataifa. Lakini, kibiashara na baadhi ya shughuli za kiuchumi, tumeathirika hasa zile zinazotegemea masoko ya kimataifa hususan ya mataifa tajiri ya Marekani, Ulaya na Asia. Athari kubwa ya kwanza ni ile ya kupungua kwa bei na masoko ya bidhaa zetu tunazouza nje ya nchi hususan mazao ya kilimo, madini na bidhaa za viwandani. Kadhalika, sekta ya utalii nayo imeathirika na kupungua kwa
watalii wanaokuja nchini. Vilevile uwekezaji wa kutoka nje umepungua.
Kwa upande wa mauzo ya mazao ya kilimo napenda nitoe mifano ya pamba, kahawa na hata maua na karafuu.

Kwa pamba, kwa kipindi kifupi cha miezi minne kuanzia Septemba
2008 bei ya pamba ilianguka kutoka senti 82 za dola kwa paundi moja mpaka senti 40. Hivyo pamba iliyonunuliwa kwa bei ya juu toka kwa wakulima, ghafla ilibidi iuzwe kwa bei ya chini na nyingine kukosa soko kabisa.
hadi mwezi Aprili 2009 marobota 124,344 ya pamba yalikuwa bado hayajauzwa.
Inakadiriwa kuwa hasara iliyopatikana kwa kuuza
pamba nje kwa bei chini ya bei ya kununulia ni kadiri ya shilingi bilioni 15 na 18. Unapochanganya tatizo hili na lile la pamba kutokuuzwa, shilingi bilioni 93.6 zilizokopeshwa na CRDB peke yake (bila kujumuisha riba) hazijarejeshwa. Kati ya madeni hayo, shilingi bilioni 4.6 ni ya vyama vya ushirika na TSh bilioni 81.9 ni ya makampuni 24 makubwa yanayofanya biashara ya pamba.
Vilevile, kwa upande wa zao la kahawa, kutoka mwezi Oktoba, 2008 bei zilianza
kushuka kutoka wastani wa US$ 140 kwa gunia la Arabica hadi wastani wa US$ 104.21. Robusta nayo ilishuka toka wastani wa US$ 91 kwa gunia hadi dola za Marekani 64 ilipofika mwezi Machi 2009, ikiwa ni anguko la bei la asilimia 26 kwa Arabica na asilimia 29 kwa Robusta. Kahawa iliyokumbwa na msukosuko huo ni kiasi cha kilo 26,645,439 za Arabica zenye thamani ya US$ 55,536,099 na kilo 11,981,710 za Robusta zenye thamani ya US$ 15,469,353.

Kutokana na bei za kununulia kahawa hizo kwa mkulima (farm gate price) kuwa za juu kuliko ile ya kuuzia kwenye soko la dunia, vyama vya ushirika vya kahawa na wafanyabiashara walionunua kahawa wamepata hasara inayokadiriwa kuwa TSh bilioni 4.85.

Ndugu Wananchi;
Hasara waipatayo wanunuzi na ugumu waupatao kuuza mazao yao kunasababisha washindwe kulipa madeni yao Benki na kuwaweka kwenye hatari ya kufilisiwa mali zao walizoweka dhamana. Aidha, kwa ukubwa wa mikopo ambayo haijalipwa na ambayo huenda isilipwe itayafanya mabenki yaliyokopesha kupata hasara. Pia mabenki hayo yanaweza kukataa
kuwakopesha wanunuzi wa mazao na kusababisha mgogoro mwingine mkubwa wa mazao ya wakulima kutokununuliwa msimu ujao. Jambo hilo likitokea litafanya wakulima kula hasara na kuwa maskini zaidi.

Shabaha ya mkakati wetu ni kumpunguzia mnunuzi mzigo wa hasara na madeni, kuiepusha benki na hasara na kuwezesha mazao ya mkulima kuendelea kununuliwa.

Kwa upande wa kilimo cha maua na mboga mambo ni hayo hayo. Bei imeshuka kwa asilimia 25 na mauzo yamepungua kwa sababu mahitaji katika masoko ya nje yamepungua kutokana na hali mbaya ya uchumi katika nchi hizo. Kuna hatari kwamba wakulima wa maua watashindwa kulipa mikopo ya mabenki ya Tshs. bilioni 43.4, ajira za watu zitapotea (tayari Mount Meru Flowers imepunguza watumishi 36). Sekta hii inaajiri watu 3,000 na wengi wao ni wanawake. Ni dhamira yetu pia hapa kuwanusuru wakulima, mabenki na ajira.

Madini
Ndugu Wananchi;
Hali ni mbaya pia kwa upande wa bei na masoko ya vito hasa almasi na Tanzanite. Bei ya Tanzanite imeshuka kwa asilimia hamsini na kufikia US$200 kwa karati. Bei ya almasi imeshuka kwa asilimia 26 na kuwa US$8,870 mwezi Septemba. Wachimbaji na wanunuzi wa almasi, Tanzanite na vito vinginevyo wanakabiliwa na tatizo kubwa la madini ambayo wanapata taabu kuyauza.
Bahati nzuri dhahabu haina matatizo hayo. Soko lake ni zuri na bei ni nzuri sana. Mkakati wetu unalenga namna ya kuwasaidia wachimbaji wa vito ambao tusipowasaidia wao na serikali tutaendelea kukosa mapato na wakati huo watu wengine watakosa ajira kwa sababu ya shughuli za uchimbaji kupungua.

Viwanda na Utalii
Ndugu Wananchi;
Viwanda vyetu navyo hasa vya nguo, nyuzi, mavazi na vile vya ngozi vimeathirika na msukosuko wa uchumi wa dunia. Mauzo nje yamepungua sana na kusababisha hasara kubwa. Uzalishaji umepungua, ajira nazo hali kadhalika. Sekta ya Utalii ambayo ndiyo sekta kiongozi kwa mapato ya fedha za kigeni nayo imebanwa pia.
Idadi ya Watalii wanaokuja nchini inapungua. Takwimu zinaonyesha
idadi hiyo kupungua kwa asilimia 10. Mapato yatokanayo na utalii ya mwezi Januari – Aprili, 2009 nayo yamepungua na kufikia US$302.1 kutoka US$388.2 milioni mwaka 2008. Hali hiyo inaathari kubwa kwa wawekezaji na kwa mapato ya Serikali na fedha za kigeni hivyo nayo tumeipa uzito stahiki katika mkakati wa kunusuru uchumi.

Mapato ya Ndani
Ndugu wananchi,
Kutokana na matatizo ya kupungua mauzo nje, utalii, uwekezaji n.k mapato ya ndani ya Serikali nayo yameathirika. Sasa hivi, tunakusanya mapato kutoka ushuru wa forodha, kodi za ndani n.k yako chini ya kiwango tulichotarajia. Kama mwenendo wa makusanyo ya kodi utaendelea kama ulivyo sasa, makusanyo ya kodi kwa mwaka 2008/09 yatakuwa chini ya makadirio ya bajeti kwa asilimia 10. Kwa maneno mengine, tutashindwa kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 472.9 ambazo matumizi yake tulishayapangia kwenye bajeti.

Katika mkakati huo tumeweka mipango ya kuikabili hali hiyo katika mwaka huu wa fedha na mwaka ujao pia ambapo tunadhani athari zitakuwepo au hata kuzidi.

Mapato ya Fedha za Kigeni
Ndugu Wananchi;
Kwa sababu ya kupungua kwa mauzo ya mazao yetu nje, mapato yetu ya fedha za kigeni yatapungua pia. Inakadiriwa kuwa thamani ya mauzo nje itapungua kutoka US$ 2,891 milioni mwaka 2008/09 hadi US$2,860 milioni mwaka 2009/10.

Wakati huo huo mapato ya fedha za kigeni kutokana na utalii yatapungua kwa US$ 186 milioni. Katika mkakati wetu tunayo mipango ya kuziba pengo hilo ili kuepuka matatizo ya upatikanaji wa fedha za kigeni kwa ajili ya manunuzi yetu ya nje.
Uwekezaji kutoka nje
Ndugu Wananchi;
Kwa sababu ya matatizo ya uchumi uwekezaji wa vitega uchumi kutoka nje umepungua. Wawekezaji wamekuwa wanakosa fedha kutoka mabenki na masoko ya mitaji. Matokeo yake ni kuchelewa au kukosa kabisa au kuahirishwa miradi mikubwa ambayo ingetoa mchango muhimu kwa ukuaji wa uchumi wetu na ajira.


Kwa mfano: Mradi wa umeme wa MW 300 kule Mtwara kwa sababu ya Barrick Gold Ltd. kujitoa na Artumas peke yake haina uwezo wa kifedha; mradi wa nickel Kabanga, mradi wa aluminium smelter, Mtwara; mradi wa usambazaji umeme mkoani Mtwara, miradi ya viwanda vya saruji na mbolea Mtwara na uwekezaji katika utafutaji wa madini umepungua kutoka US$90 mpaka
US$40 milioni.

Ajira
Ndugu Wananchi;
Hali ya ajira nchini nayo itakuwa mbaya kutokana na matatizo haya. Mwaka 2009 ni mwaka ambao athari za msukosuko zimeanza kujitokeza kwa nguvu katika masoko ya ajira na kusababisha watu wengi kupoteza kazi na hivyo kuongeza umas wa kipato.

Hadi kufikia Aprili 2009 jumla ya wafanyakazi 48,000 walikuwa wamepoteza ajira zao nchini. Kutokana na kutarajiwa kupungua kwa idadi ya watalii wanaokuja nchini, baadhi ya hoteli zilizotarajiwa kuwapokea watalii hao zimelazimika kupunguza wafanyakazi wao kutokana na kupungua kwa biashara. Kati ya asilimia 20-30 za ajira katika sekta ya utalii Zanzíbar ziko hatarini kupotea kutokana na upungufu wa utalii. Vivyo hivyo, katika sekta ya kilimo, viwanda na madini, watu wengine wanatarajiwa kupoteza kazi zao.

Kupungua kwa ukuaji wa uchumi
Waheshimiwa Wabunge, Ndugu Wananchi,
Matokeo ya athari zote hizi ni kupungua kwa kasi ya ukuaji wa uchumi nchini. Kama mjuavyo, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, uchumi wetu umekuwa ukikua kwa kiwango cha juu cha wastani wa asilimia 7.2. Tulitegemea mwaka huu uchumi wetu ungekuwa kwa zaidi ya asilimia 8 na kufikia asilimia 10 mwaka 2010 kama tulivyoahidi kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2005. Lakini kama wasemavyo Waswahili, ng’ombe wa maskini hazai. Msukosuko wa fedha na uchumi duniani umesababisha ukuaji wa uchumi wa Tanzania kupungua kutoka asilimia 7.4 mwaka jana hadi kati ya asilimia 5-6 mwaka
huu. Kwa upande wa Zanzibar, uchumi wao unategemewa kukua kwa asilimia 4.5 mwaka huu ukilinganisha na asilimia 5.4 mwaka jana.

Mkakati wa Kuhami na Kuunusuru Uchumi
Ndugu Wananchi;
Baada ya kutafakari hali hii, na kuchambua athari hizi nilizobainisha kwa uchumi, ustawi na mipango ya muda mrefu ya maendeleo ya Taifa letu, na kwa kuzingatia azma yangu niliyoitangaza kwenye salamu ya mwaka mpya wa 2009, kwamba mwaka huu ni mwaka wa kuhami na kukuza uchumi, tumebuni na tutatekeleza Mkakati Maalum wa Kuhami na Kuunusuru Uchumi wa Tanzania.

Mkakati huu unazingatia ukweli kuwa msukosuko wa uchumi duniani ni wa kupita. Changamoto ya muda mfupi ni jinsi ya kujinusuru na hatimaye kudumisha juhudi za maendeleo baada ya msukosuko kupita.

Katika kukabili athari hizi nilizozitaja, tunalenga mambo mawili makuu. Kwanza ni kupunguza makali ya msukosuko, na pili, kulinda uwekezaji ambao ni muhimu katika kudumisha ukuaji endelevu wa uchumi katika kipindi cha muda wa kati. Mkakati wetu wa kuhami na kuunusuru uchumi unalenga kukabili matatizo ya mpito na dharura – hasa ya ukwasi (liquidity) na siyo ufilisi (solvency).

Mkakati huu sio mbadala wa mipango ya maendeleo na bajeti ya Serikali ya kila mwaka. Chini ya mkakati huu Serikali imepima matatizo kwa uzito wake na kushughulikia yale tu yaliyojitokeza hivi karibuni kutokana na msukosuko wa uchumi na siyo vinginevyo.

Ndugu Wananchi;
Tumetengeneza Mkakati huu kutimiza malengo makubwa manne:
1. Kulinda ajira na vipato vya wananchi;
2. Kuhakikisha upatikanaji wa chakula;
3. Kulinda uwekezaji muhimu katika miradi ya maendeleo, hususan miundombinu, na
4. Kulinda programu muhimu za kijamii

Ndugu Wananchi;
Kama nilivyosema, lengo kuu la kwanza la mkakati huu ni kupunguza makali au kuhimili shinikizo la msukosuko, hususan kuwalinda wananchi walio katika hatari kubwa zaidi ya kimaisha. Katika kutekeleza hili lengo yako mambo kadhaa ambayo tutayafanya:

(i) Kufidia hasara waliyopata wanunuzi wa mazao msimu wa 2008/09
Serikali imeamua kufidia vyama vya ushirika na makampuni yaliyonunua mazao ya wakulima na kuyauza kwa hasara. Hasara hiyo inayokisiwa kufikia shilingi 21.9 bilioni imepatikana kutokana na bei ya kuuzia mazao hayo kuwa chini sana ya gharama iliyotumika kuyanunua. Serikali italipa madeni yenye thamani ya hasara hiyo, moja kwa moja kwa mabenki yaliyokopesha vyama na makampuni hayo. Lakini tutafanya uhakiki kabla ya kulipa. Napenda kusisitiza kuwa hatutalipa madeni ya zamani ambayo hayahusiki na msukosuko wa uchumi wa dunia.

(ii) Kutoa udhamini wa kuahirisha mikopo ya waathirika
Yapo madeni ambayo wakopaji kwa sababu ya msukosuko wa uchumi wa dunia wanapata matatizo kulipa kwa wakati. Kundi hili linawajumuisha wengi wenye viwanda, wenye shughuli za utalii, kilimo n.k. Madeni hayo yanafikia Shs.270 bilioni. Serikali itayadhamini madeni na kuyataka mabenki kuahirisha ulipaji wa mikopo hiyo na riba yake wa miaka miwili.
Udhamini wa Serikali utatolewa kwa uwiano wa kila shilingi moja kwa shilingi tano na Serikali ikidhamini asilimia 70 ya mkopo. Kwa uwiano huu, fedha zitakazohitajika katika dhamana hiyo ni TSh 45 bilioni. Pamoja na kutoa nafuu kwa makampuni lakini hatua hii pia itayawezesha mabenki kuendelea kutoa mikopo na hivyo shughuli za kiuchumi na biashara hazitaisimama.

(iii) Kutoa mitaji ya uendeshaji (working capital) kwa riba nafuu
Tumeamua vilevile kuchukua hatua za kupunguza upungufu wa mitaji ya uendeshaji (working capital). Kwa ajili hiyo Serikali itayakopesha mabenki fedha kwa riba nafuu ya asilimia 2 ili na wao wawakopeshe wafanyabiashara fedha za mitaji ya uendeshaji kwa riba nafuu.
Lengo ni kusaidia walioko kwenye sekta zinazokumbwa na msukosuko wa uchumi waweze kuhimili vishindo. Kwa kila shilingi moja tutakayotoa sisi Serikali, benki husika itatakiwa itoe shilingi moja na nusu (1:1½).

Kwa madhumuni haya, tutaanzisha mfuko maalumu wenye shilingi bilioni 80 ambao utasimamiwa na Benki Kuu na mabenki yatakayoshiriki yatatakiwa kutoa shilingi 120 bilioni. Viwango vya riba kwa wakopaji vitapangwa kwa maelewano ya pamoja baina ya BoT na mabenki na itategemea sekta na shughuli yenyewe.

(iv) Kuboresha Mifuko ya Dhamana:
Chini ya mkakati huu tutaiboresha na kuiongezea fedha mifuko ya kudhamini mikopo (credit guarantee schemes). Mifuko hiyo ni pamoja na Mfuko wa Udhamini wa Uuzaji wa Mazao Nje ya Nchi (Export Credit Guarantee Scheme -ECGS) na Mfuko wa Udhamini wa Mikopo kwa Wajasiliamali Wadogo na wa Kati (SME Credit Guarantee Scheme).

Tutaongeza mtaji wa shilingi bilioni 10 kwa kila mfuko katika mwaka wa fedha wa 2009/10. Nyongeza hii itawezesha kuongeza dhamana ya mikopo ya shilingi bilioni 65 kwenye Mfuko wa Udhamini wa Uuzaji wa Mazao Nje ya Nchi na shilingi bilioni 60 kwenye Mfuko wa Udhamini wa Mikopo kwa Wajasiliamali Wadogo na wa Kati katika kuchochea mauzo ya bidhaa nje na uzalishaji. Hivi sasa mfuko wa ECGS una mtaji wa Shs.32.5 bilioni na umekopesha Shs.161.5 bilioni na ule wa SME una Shs.500 milioni na umeshakopesha Shs.6.5 bilioni.

(v) Kupunguza gharama za vito vya thamani:
Katika sekta ya vito vilivyoshuka bei kwa kiasi kikubwa, kama vile Tanzanite na almasi, tunaangalia uwezekano wa kuahirisha ulipaji wa mrahaba (royalty) kwa wachimbaji wa vito. Lengo ni kuwapa muda wa kupumua na kujijenga. Chini ya mpango huu Serikali itaahirisha mapato ya kiasi cha US$ milioni 0.5 kutoka almasi na US$ milioni 2.5 kutoka tanzanite.

(vi) Kuongeza uzalishaji wa Chakula

Ndugu Wananchi;
Lengo lingine muhimu la mkakati huu ni kuinusuru nchi kutokana na athari za upungufu wa chakula duniani zilizochochewa na msukosuko. Katika kutekeleza hili, mkakati huu utahakikisha kuwa miradi yote ya kilimo, hususan ile ya uzalishaji wa mazao ya chakula, inaendelea kugharimiwa bila kuathiriwa na msukosuko. Lengo la kwanza ni kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula ili kujitosheleza kwa chakula na kuuza ziada nje na hivyo kutumia ipasavyo fursa inayotokana na kuadimika kwa chakula duniani.

Chini ya mkakati huu, pamoja na kuendelea kuhimiza na kusimamia yale mambo yote ya kuongeza tija na uzalishaji kwenye kilimo, tumeamua katika kipindi hiki kufanya yafuatayo:

(i) kutoa mikopo nafuu na ya muda mrefu ya shilingi 20 bilioni kupitia
TIB kwa sekta binafsi kwa ajili ya kuendeleza kilimo

(ii) kutoa shilingi bilioni 20 kwa ajili ya mkopo wa riba nafuu kwa zana za kilimo kama matrekta madogo kupitia mpango wa karadha (lease finance), ambapo, kwa kila shilingi ambayo serikali itatoa, mabenki yatakayoshiriki katika mkakati huu itabidi nayo yatoe shilingi moja: na

(iii) Kuongeza kiasi na idadi ya wakulima watakaopata mbolea ya ruzuku kwa utaratibu wa vocha. Benki ya Dunia watatupa mkopo wa US$46 milioni na sisi tutatoa kiasi hicho hicho kwenye mfuko wa mbolea katika mwaka ujao wa fedha (2009/10).

Aidha tumeamua sasa tutumie Hifadhi ya Chakula ya Taifa kusaidia kutuliza bei za vyakula kwa walaji. Tunaiboresha sera ya sasa ambapo Hifadhi hungojea ilani ya njaa. Tumesema kupanda sana kwa bei za vyakula vikuu katika soko ni dalili ya upungufu hivyo kupunguza makali kila inapowezekana.

Chini ya mkakati huu, tutatoa shilingi bilioni 20 kwa Hifadhi ya Chakula ya Taifa kwa ajili ya kuongeza akiba ya chakula na kudhibiti mfumuko wa bei.
Miundombinu
Ndugu Wananchi,
Kuhusu lengo la kulinda uwekezaji muhimu, hasa katika miundombinu, ya umeme na reli tumekubaliana kuwa tuendeleze juhudi za kutafuta mikopo kutoka Benki ya Dunia na mashirika mengine ya fedha. Kwa ajili hiyo tutatumia fedha za IMF kukwamua mradi wa usambazaji umeme Mtwara. Zinatakiwa US$ 7 milioni.

Kuhusu Shirika la Reli, sisi tuchangie sehemu yetu, yaani US$43 milioni, kuongezea US$ 40milioni za Benki ya Dunia kuimarisha reli yetu. Wakati huo suala la uendeshaji tulitafutie jawabu muafaka.

Kadhalika tumekubaliana kuwa taendelee kuwekeza katika ujenzi wa barabara na miradi ya elimu, afya na maji. Suala la hati-fungani ambalo liliahirishwa kwa sababu ya matatizo ya soko la fedha tulitafutie vyanzo mbadala.

Ndugu Wananchi;
Tumekubaliana pia katika mkakati huu, kuwa lazima kuhakikisha kuwa utulivu wa uchumi unakuwepo ili kuhimiza ukuaji endelevu wa uchumi na kuvutia sekta binafsi kushiriki. Vilevile tuongeze kasi ya kuharakisha uimarishaji wa TIB na uanzishwaji wa Agricultural Development Bank.

Ndugu Wananchi;
Kuhusu lengo la Mkakati la kulinda programu muhimu za kijamii, Serikali
itahakikisha kuwa mipango yote ya kijamii haitaathirika, hata ile ambayo itakosa fedha za kutosha kutoka kwa wafadhili. Hii inajumuisha mipango ya utoaji wa ruzuku kwa dawa za kurefusha maisha kwa wagonjwa wa UKIMWI, vyandarua vya kuzuia malaria, programu za kifua kikuu, na nyingine za kusaidia juhudi za vijana na kulinda makundi ya wanyonge.

Ndugu Wananchi;
Pia zipo hatua kadhaa nyingine za kisera ambazo Serikali inaziandaa katika
kukabiliana na athari za msukosuko huu. Katika miezi inayokuja, Wizara mbalimbali zitatangaza hatua za kisera zenye nia ya kuzihami sekta hizo na athari hizi na kuchochea ukuaji wa sekta mbalimbali kama vile utalii na viwanda.


Miongoni mwa hatua tunazoziandaa sasa ni kupunguza gharama za visa kwa watalii kutoka dola 100 na 200 na kuwa dola 50. hazina inaangalia uwezekano wa kufanya hivyo.

Namna Serikali Itakavyolipia Gharama za Programu Hii
Ndugu Wananchi;
Kutekeleza Mkakati huu ni gharama kubwa. Zitahitajika kiasi cha shilingi bilioni 1,692.5. Tumetenga pesa hizo katika Bajeti yetu ya mwaka wa fedha utakaoanza Julai, 1, 2009. Sehemu kubwa ni fedha zetu lakini pia tutapata misaada kutoka kwa marafiki zetu wa maendeleo hasa Benki ya Dunia, IMF, EU na India.

Hitimisho
Ndugu Wananchi,
Sasa nimefika mwisho wa hotuba yangu. Nawashukuru tena kwa kukubali wito wangu. Kwa nchi yetu ambayo bado ina safari ndefu katika maendeleo, hatua tuliyochukua hapa ni kubwa na ya kihistoria.

Katika kuchukua hatua hii, tumezingatia mahitaji ya dhamana tuliyopewa na wananchi katika kuwaongoza na kusimamia maendeleo na ustawi wao na wa
nchi yetu. Lakini vilevile, tumezingatia mafundisho ambayo historia ya nchi yetu imetupatia.
Kwa mkakati huu, tumedhamiria kuepuka hali iliyojitokeza miaka ya 1980 ambapo kutokana na kushindwa kukabili kwa dhati na wakati muafaka, athari za kupanda kwa bei za mafuta na hali mbaya ya uchumi wa dunia iliyofuatia, zilisababisha nchi kupoteza miongo miwili ya ukuaji wa uchumi na mafanikio yaliyokuwa yamepatikana katika nyanja za jamii na miundombinu.

Mwisho kabisa, nawasihi viongozi wenzangu na wananchi kwa ujumla, tuwe wavumilivu na tuiunge mkono Serikali katika kutekeleza mkakati huu. Tangu mwaka 2006, mambo hayakuwa mepesi sana, tumepitia misukosuko mikubwa kwa uchumi wetu: mgao mkubwa wa umeme, njaa, bei kubwa ya mafuta na bei kubwa za vyakula na sasa msukosuko huu wa aina yake. Kwa kila tatizo tumepambana nalo kiume na kwa umakini mkubwa na kuvuka
salama. Mshikamano wetu, umoja wetu ndiyo uliotufikisha hapo.

Napenda kuwahakikishia wananchi wa Tanzania kwamba Serikali yao inawajali na inafanya kila lililo ndani ya uwezo wake kutimiza wajibu wake katika kuwatumikia. Sisi katika Serikali tupo kwa ajili yenu na tutaendelea kuwatumikia kwa nguvu zetu zote. Tutaendelea kutengeneza mipango na mikakati ya kukabiliana na matatizo na changamoto zinazowakabili wananchi wa Tanzania walioko katika kila kona ya nchi
yetu.

Tuliyaweza yale naamini na haya tutayamudu!!

Asanteni sana kwa kunisikiliza!
Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!


































Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 32 mpaka sasa

  1. AnonymousJune 10, 2009

    Hali mbaya ya uchumi bongo inatokana na ufisadi,Ningepoteza muda wangu kumsikiliza kama angezungumzia UFISADI.
    I`m just say.

    ReplyDelete
  2. AnonymousJune 10, 2009

    Me-choose,
    Nadhani ungetakiwa kuandika "JK ameshaanza kuhutubia..." na si kuongea kama ulivyoandika. Kuongea ni two-way traffic. Anachofanya JK ni kuhutubia kwani upande wa pili unasikiliza tu bila kutamka neno!

    ReplyDelete
  3. AnonymousJune 10, 2009

    KAKA naona jamaa hon.Jakaya anapendeza.ila samahani kuna mtu mmoja umepiga naye picha hapo chini Dj Choka uwa ni nani mimi naona ni bepari flani kwa Jay anamganda sana mshikaji sio kihivyo ndio maana jamaa kashutuka kamtema tuache kutegemea kebebwa mwanzo mwisho.

    ReplyDelete
  4. AnonymousJune 10, 2009

    hutuba ya mh,rais tunaisubili kwa hamu sana,lakini pia rais inatakiwa arekeze zaidi huduma kwa wanchi siyo kuongea tu,kwani hosptali hazina dawa,vitanda,na hata,hali ya kimaisha ya mtanzania haieleweki,kwani wachache tu ndio wenye uwezo wa kujikwamua,na hasa inatia uchungu hasa ukisika ufisadi unakendea ktk selikali yake,aige mfano wa serikali ya uingereza inavyo wachukulia hatua kali wabunge na hasa wanapobainika kujihusisha na matumizi mabaya ya pesa za uma,ikiwemo na kuzirudisha,tumesikia mengi sana ktk serikali yake watu wanaiba mamilioni ya dolla za,lakini hawashglikiwi at all,tunaomba pia mwelekeo mzuri wa kupambana na rushwa,pesa nyingi zinakuwa zinavuja,kutoka ktk mapato ya serikali,je ataweka mikakati,mzuri ya kuzibiti mfeleji hiyo?.ili watu wawe na imani na serikali yao.kuhusu democrasi rais pia anatakiwa akemee zurugu zinazokuwa zinatokea hasa kwenye chaguzi,za wabunge ktk majimbo.inatia aibu kwa serikali watu kupigana na hata kupoteza maisha ya watu.kisa uchu wa madalaka.marlesa mussa wa 22 hapa.uk

    ReplyDelete
  5. AnonymousJune 11, 2009

    Bw.Michuzi! Kuuliza si ujinga mbona viongozi wetu wakubwa wanapenda kuvaa saa kama aliyovaa JK,je kuna tajiri huwa anawapa hizo saa au ndo mtindo wa viongozi wa kibingo? Atakaye kuwa najibu nitashukuru.
    Kazi njema.

    ReplyDelete
  6. AnonymousJune 11, 2009

    Mbona hajazungumzia bongoflava?

    ReplyDelete
  7. AnonymousJune 11, 2009

    hotuba nzuri kuhusu matatizo ya uchumi yanayoikumba dunia, mimi niliyeko ughaibuni nafarijika kuona hata serikali yetu inafikiria jinsi ya kasaidia waathirika wakubwa wa mtikisiko huu kama wafanyavyo wakubwa huku. Kuhusu mambo ya ufisadi yapo popote duniani lakini suluhisho sio kuyatungia nyimbo bali kila mtu kwa nafasi yake apigane kiume

    ReplyDelete
  8. AnonymousJune 11, 2009

    Si angetuacha tusikilize Bajeti au sifa zingekwenda kwa Mkulo?

    ReplyDelete
  9. mechooze kaka ahasnte kwa hotuba ya mheshimiwa Jk tuipata ila kwa upande wa Mabenki na vyama vya kununua mazao kawapa kipao mbele lakini hayo mabenki hayana riba nafuu kama dhamira ya serikali ilivyo nzuri sasa Mabenki yawe na huruma kidogo kwa wateja wake.ni hayo tu nasubiri, Wasiwasi vs shayo
    waliobobea wahamke ahsante hon.wa Tegeta

    ReplyDelete
  10. AnonymousJune 11, 2009

    Hata Taifa Staaz hawajazungumziwa pamoja na kumpiga mtu bao...

    ReplyDelete
  11. AnonymousJune 11, 2009

    Kinachochelewesha maendeleo ya nchi hii sio mtikisiko wa uchumi duniani bali ufisadi.Rais anatakiwa akamate mali za mafisadi sio kuzungumzia mambo yaliyo juu yetu.Fedha ziko kwa mafisadi na baadhi yao ni wabunge na wanaingia bungeni je ni halali fisadi kuwakilisha wananchi bungeni?

    ReplyDelete
  12. MAJIBU YA HOTUBA YA RAISI KUTOKA KWA MCHUMI WA TEXAS.

    Kwanza nimshukuru raisi kwa kuweka bayana kwamba hali ya uchumi bado ni tete. Na kwamba mpasuko huu bado unaendelea japo kwamba masoko ya hisa na mitaji yameanza kuonyesha dalili za kupona, lakini hali bado si shwari.

    Naomba niweke bayana kwamba muheshimiwa raisi alicho chambua ni kitu kijulikanocho kama " Government Big spending", bila kuchambua sehemu ambazo serikali itakata matumizi. Serikali ya Tanzania imedhamiria kutumia takriban shilling Billion 1,692.5 sawa na 1.7% ya Tanzania GDP. Wakati ukuaji wa uchumi wa Tanzania ni takriban 6% kwa miaka 7iliyopita.

    Cha ajabu ni kwamba muheshimiwa rahisi hajasema kwa undani kwamba tutalipia vipi hudama zote alizozitaja. Kusema kwamba sehemu kubwa itapatikana kutoka kwa marafiki zetu ni kulitazama jambo kwa jicho la pembeni. Wananchi tungependa kujua jee ni asilimia ngapi ya matumizi hayo yatatoka kwa wadhamani na asilimia ngapi itakuwa mkopo? Jee miradi hii itaaingiza Tanzania kwenye deni la shiling ngapi? Na ni mwaka gani au kwa ukuaji gani wa uchumi tutaweza kulilipa deni hilo?

    Niwarudishe nyumba kidogo, Mh. Mkapa aliweza kuisaidia Tanzania ikapunguziwa madeni katika mradi wa HIPC kwa shilling 2,026 billion kwa mwaka 1999 na kwa takribani kiasi hicho hicho kwa miaka ijayo kwenye deni lilokuwa na dhamani ya $7 Billion USD sawa na 44% ya GDP ya Tanzania. Hivyo basi matumizi ya kipindi hichi tuu ni sawa na 84% ya deni zima tulilosamehewa kwa mwaka 1999. Sasa swali langu ni mmoja tuu jee tunakwenda mbele au tunarudi nyuma?

    Tukumbuke kwamba pesa zote hizi tunazotumia leo madhara yake yatakuwa kwa watoto wangu, wako michuzi na wanajamiii wote. Hawa wototo ndio watakimbizana na World Bank, IMF na Paris club, Bank ya Asia na wakopesjaji wengine.

    Nivigumu sana kwa mtu ambae hana historia ya uchumi kuelewa madhara ya deni la taifa (national defecit). Lakini kwa sasa ni imani yangu kwamba kwa kila shilling serikali yetu inayotumia basi zaidi ya centi 40 tumekopa au kupewa msaada. Sasa Jee siku wakitaka madeni tutalipaje? Jee tutaweza kuzuia mianya katika Foreign Direct Investment wakati wao ndio wanao tuweka mjini?

    Nilitegemea muheshimiwa JK atakuja na new agenda ambayo ni kufreeze matumizi yasio na maana ya serikali kama KUTONUNULIA WABUNGE VX, KUKOMESHA SEMINA ZISIZO NA KICHWA WALA MIGUU. Kuwekeza fedha kwenye sector ambazo zina uhitaji mkubwa wa fedha na zinaweza kuzalisha ajira.

    Nadhani tumetumia FDR approch bila kufahamu kwamba US wanazo tools muhumi katika swala zima la kuchachusha uchumi wao. Na sisi ni taifa masikini ambalo kwenye kila shilingi tunayotumia zaidi ya 40% tumekopa au kupewa. Sasa jee tutafika?

    Mwisho muheshimiwa raisi hakuchambua kwamba pesa hizi zitakuwa vipi na transparency ilikuzuia wezi kama wale wa EPA wasitumie kisingizio cha uchaguzi wa 2010 na kujilia chao?

    I expect watu kama Shayo ambao ni Economist by proffesional wanaweza kufanya publication muhumi kaika swala hili... Jee ni madhara gani serikali ya Tanzania inaweza kupata kwa kujiingiza kwenye kisima hichi? Jee serikali imetumia model gani kupata idea kwamba plan hii itasaidia kupunguza kazi ngapi? au kuzalisha kazi ngapi?

    ReplyDelete
  13. AnonymousJune 11, 2009

    Tuwekee picture za waliokua wanamsikiliza walivyo uchapa usingizi.

    ReplyDelete
  14. AnonymousJune 11, 2009

    Tukiangalia kwa undani kuyumba kwa uchumi wa dunia kumeongezewa na ufisadi wa watu wachache, hili lipowazi kwa wenye kuona, na hapa kwetu ni halikadhalika.
    Tatizo hapa kwetu wapo mafisadi wa kimataifa,bila huruma wanakuja kufisidi kile kidogo tulichojaliwa kuwa nacho, na kwasababu ni mafisadi wa kimataifa, ujanja wao ni mkubwa, hatuwezi kirahisi, kuwagindua na kuwakabili, kwani wanazo kila mbinu za kimataifa, ndio maana sisi wenyewe hatuoni, tunaona `kawaida tu' waachie wapite!
    Wajamaa kama kweli tunataka kuwagundua hawa watu tusiwape nafasi za `kisiasa' za muda mrefu, kwani huko ndio njia yao. Tukigundua tu huyu mchafu, tumtoe nje, hata kama ni chama , tusikipe nafasi ya muda mrefu, kama kina uchafu tukitoe nje.Nashangaa watu mumewaona wagombea wana madoa ya uchafu bado mnawapa kura zenu, chama kina madoa ya uchafu bado ...jamani mnataka mpaka mtiwe vidole machoni, ...
    m3

    ReplyDelete
  15. AnonymousJune 11, 2009

    Wadau tujaribu kuijadili hiyo hutuba badala kumjadili Jk kavaa nini,mbona watanzania mambo muhimu kama haya tunayafanyia mzaha?hivi wote tunakubaliana nchi ni masikini lakini yenye rasilimali tele,kwa nini na sisi tusitoe mikakati yetu kuinusuru nchi yetu.mimi wasiwasi wangu ni siasa nyingi kwenye hotuba za jk wakati utekelezaji unakuwa hadithi.Leo tunafikiria kuwalinda wawekezaji kwenye madini,hoteli viwanda wakati miaka yote wamekuwa wakwepa kodi wakubwa kwa visingizio vingi tu.ni bora kuimarisha mabenki yaliokopesha wakulima kuliko hao mafisadi.toka awamu ya kwanza jk aliona kununua mashangingi ya kifahari serikalini ndio maendeleo,leo hii kumekucha tunakumbuka shuka kununua matreka kwa wakulima wetu masikini.wapinzani wamekuwa wakipigia kelele suala la matreka na kupunguza ununuzi wa mashangingi wakaambia wana wivu wa kike.ningepensda kuona mikakati katika hotuba hii inatekelezwa na si kuwa hotuba ya kampeni za 2010 baada ya kuona ufisadi umewashinda.

    ReplyDelete
  16. AnonymousJune 11, 2009

    wakati umefika sasa kwa Katiba ya nchi ifanyiwe marekebisho ili Rais wa Nchi yeye mwenyewe alazimike Kuisoma Hotuba ya Bajeti ya serikali yake katika kikao cha Bunge cha Bajeti badala ya jukumu hilo kuachiwa alifanye Waziri wa Fedha kama ilivyo sasa.Rais wa Nchi ndiye aliyechaguliwa na wananchi kuunda serikali itakayo ongoza nchi kwa kipindi fulani.Na ni yeye aliyepaswa kuwajibika kwa wapiga kura katika kuliomba Bunge Lipokee mapendekezo ya serikali yake kwa mwaka fulani wa fedha,bunge nalo liyachambue mapendekezo hayo,ikibidi Rais apate fursa ya kuyatetea mapendekezo au Bajeti yake hadi hatua za mwisho Mapendekezo hayo yatakapo idhinishwa na Bunge la Bajeti!Utaratibu uliopo sasa unatoa mwanya mkubwa sana kwa Rais kukwepa wajibu wake na kuyaacha mambo yakiendeshwa kizembe kabisa bila ya woga wa kuwajibishwa na Bunge kwa mfano Bunge kuikataa Bajeti nzima hadi ifanyiwe marekebisho upya pale itakapostahili ndipo ipitishwe!Huo ni utangulizi wangu kwa wana Blogger!Lakini nilichotaka kukisemea leo ni kuhusu Sura na Muundo wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2019/10 itakayo somwa Bungeni wiki hii na Waziri wa Fedha.Kwa mujibu wa Muhtasari wa Bajeti hiyo uliosomwa na Waziri huyo kwa vyombo vya habari siku tatu zilizopita ni wazi kwamba Bajeti hiyo siyo nzuri hata kidogo.Ni Bajeti Tegemezi ambayo haitakuwa na uwezo wowote wa kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi.Haya hayo makisio ya Rais ya kukua kwa uchumi kwa aslimia TANO AU SITA ni jambo ambalo halitowezekana hata kidogo.MAPATO YA SERIKALI yanakadiriwa kufikia shilingi Trillioni 9.5;kati yake MIKOPO NA MISAADA YA NJE itachukua asilimia 33.68% ya mapato yote,na wkakati huohuo Bajeti ya Maendeleo(Development Budget)itagharimu asilimia 29.47% ya Mapato yote au Matumizi yote ya serikali katika mwaka ujao wa fedha,2009/10!Theoretically speaking or rather Economically speaking ni kwamba hii ni sawa kabisa na kusema kwamba "Bajeti yetu yote ya Maendeleo au Miradi yote ya Maendeleo kwa mwaka 2009/10 itafadhiliwa au kugharamiwa na Wahisani toka nchi za nje kwa asilimia 100%!,NA BADO ITABAKIA ZIADA ambayo itagharamia sehemu ya Bajeti yetu ya Matimizi ya Kawaida kama mishahara ya watumishi wa serikali na ununuzi wa magari na mahitaji mengineyo!".Hiyo ndiyo taswira halisi ya Bajeti yetu au ya serikali ya Kikwete kwa mwaka huu wa fedha 2009/10,pure and simple!Matumizi ya Kawaida ya BAJETI NZIMA yatachukua asilimia 70.52% ya Mapato yote!THIS IS A HEAVILLY CONSUMPTIOUS BUDGET!Too much wastage and misuse of meager public finance admist grinding poverty amongst the poorest rurals!Mapato ya Serikali yatakayo tokana na Vyanzo vyetu wenyewe vya ndani yatachukua asilimia 53.68% ya makadirio yote ya Mapato!licha ya mzigo mkubwa sana wa viwango vikubwa mno vya kodi walivyobebeshwa watanzania!HEBU NIELEZE UTATARAJIA KITU GANI KATIKA BAJETI DHAIFU NA DUNI KIASI HICHO?No where has President Kikwete talked anything about "HIS INTENTIONAL INCOME REDISTRIBUTION POLICIES!".Watu wachache sana hapa nchini ndiyo waliohodhi sehemu kubwa sana ya PATO LA TAIFA na kuwaacha zaidi ya robo tatu ya watanzania wote SOLEMBA wakiishi katika "Ufukara Uliokithiri!" licha ya utajiri mkubwa wa dhahabu,makaa ya mawe na gesi asilia,utalii na utajiri wa mazingira asilia,kilimo cha mazao ya biashara na mengineyo mengi!Haya ndiyo mambo niliyo tarajia kuyasikia katika hotuba ya "Mtukufu Rais jana!"Lakini wapi?Maswali yangu bado yako palepale hayajapata majibu!Sijui,tumsubiri waziri wake wa fedha tuone lipi jipya,kusuka au kunyoa?Mtu mzima hadanganyiwi Pipi!"papparazzzi economist hunger specialist"

    ReplyDelete
  17. AnonymousJune 11, 2009

    What a day tu unveil your new Rolex mr prezidaa ! Credit crunch, what credit crunch ?
    Ndulu and his team have been in denial all along any way, just wonder what are they doing differently this time around.
    Does any one really know what they are doing here ? Yet macho
    Mdau(UK)

    ReplyDelete
  18. AnonymousJune 11, 2009

    nimefaatilia vizuri hotuba ya mr president,mambo mengi ameongelea,tanzania masikini,u kweli ni kwamba,hayo yote siyakweli,ukilinganisha na utajili tulionao,hii kasumba,ya nchi yetu masikini,nifikili nikutokana na kizazi cha utawala wa nyerere,kwani ndiyo ulikuwa wimbo wa mwalimu,wakati huo.wakati nchi ilikuwa ikihangaika baada ya wakoroni kuondoka.my comment the president he must change hes word this is 2009,we dont need to hear words za wakakati wa mwalim nchi masikni,nchi masikini,q.1 pesa ngapi serikali inapoteza kwa ajili ya matumizi maya,mawaziri wangapi wameshafikishwa mahakani,ntill now no answer kama pesa wamerudisha au kufungu.everybody.anafahamu fika pesa zinazo ibiwa zipo,kwanini,wasirudishe,au ndo kulingana,mr rais anatakiwa abadilishe kauli zake,tanzania siyo masikini,umasikini unaruhususiwa na serikali yake.q 2.mr president amesema anampango wa kupunguza bei ya visa,why.lazima bei ya viza ingebaki kuwa pale pale,nahata ingewezekana kuongezwa,bazi ya barozi hata za mabwana mkubwa bei iko juu sana,why tanzania ipunguze,hili pia mr president hes wrong.we need to be serious about this.tanzania ina madini kibao,TANZANITE.ZAHABU.SAMAKI.KARAFUU,GASE.ALMAS.CHUNVI.ROSE GANET.RUBI.BANDARI.AIRPORT,RELI.TUNA BORDERS,ALL THIS NI MALI TENA HATA NCHI ZINGINE HAZINA,kwa misingi ipi bado tanzania bado wanai put back ground.u must stand up 4 those who come to our country just to make money nasis tupo hapo hapo.wabaya zaidi i ziongozi,hasa waliopewa madaraka,kwani lazima yote watakuwa wanayajuwa,whichs wanakula sahani moja.hawa watu wanakuja nchini kujifanya wema si wema hata kidogo,lazima tuwe imala kusimamia siyo kupunguza gharama,na kujitapa sisi ni masikini neno masikini ni baya sana,hata hao wakisikia tunajiita masiki wanapata sababu ya kuja kumsaidia masikini kumbe wanaondoka na mali zetu,tusitegemee mikopo au misaada,im pleased mr kikwete tu change.not just kuongea na kukemea.kutake action.SOONER THEN LATER.AIBU.MARLESA MUSSA WA 22 HAPA UK.

    ReplyDelete
  19. AnonymousJune 11, 2009

    such a boring speech

    kipindi kifupi cha dk 10 tu nikaondoka wala sikuendelea kusikiliza,na wengi apo tu walikua either bored or kuchapa usingizi.

    so whaaaaaaaaaaaaaaat!!!

    ongea jinsi utavowabana wawekezaji kule migodini,vitalu vya utalii nk nk ili visaidie kujenga infrastructure Tz...

    kero za wanainchi huzijui??credit crunch,credit crunch,hueleweki

    pili sie wa uku vijijini wala hatukuelewa kabisaaaa

    ivi muda woote uo ao watu hawakuwa na kazi kutumikia wanainchi?mana ndo shugli za any leader,hotuba ya MKULLO ingetutosha kupima izo bajeti

    ni hayo tu

    ReplyDelete
  20. AnonymousJune 11, 2009

    HIVI NI KWANINI VIONGOZI WETU WANAPENDA KUHUTUBIA WAKIWA WAMEKAA...OBAMA NA NCHI ZA MAGHARIBI VIONGOZI HUSIMAMAMA WAKATI WA HUTUBA...

    ReplyDelete
  21. AnonymousJune 11, 2009

    Tz sio maskini katu...nakataa kabisaaaaaaa

    sema sera na ao wasimamizi tuliowapa dhamana ya uongozi wanafenyeje kuzitumia kwa manufaa ya wengi???????????????????????????

    adi maneno sina ya kuongea kbs
    jamen

    ReplyDelete
  22. AnonymousJune 11, 2009

    MUSTAPHA MKULLO BADALA YA KUSIKILIZA HOTUBA LIMELALA TU YAANI HUYU JAMAAA ANATIA HASIRA KWELI

    ReplyDelete
  23. AnonymousJune 11, 2009

    Jamani kumbe aliyechapa usingizi ni mzee mwenyewe mtoa mada?Du kweli bongo tambarare.
    Kipanya piga kazi.

    ReplyDelete
  24. AnonymousJune 11, 2009

    Hiyo hotuba inakatisha tamaa kabisa, maana kumbe kuna wakati mwingine mambo yanakuwa mazuri serikalini, lakini sisi akina mwenzangu na mie hatujui wala hatuna habari,Loo nchi imejaa wanyonyaji Makupe na mapapasi, wana madhambi makubwa, Dunia mtaiacha, Nchi itabaki, MUNGU IBARIKI NA KUINUSURU NHI YETUNA MAFISADI. Mwinyi Mpeku.

    ReplyDelete
  25. AnonymousJune 11, 2009

    1.Nunueni matrekta makubwa ya kilimo,ardhi kubwa tunayo,limeni mashamba,wanakilimo wamejaa tele TZ,bila kazi.Nafaka uzeni kwa wanachi kwa bei nafuu,na pia wanafunzi wapewe vyakula bure. mfano mnao,hapa Danmark,kikwete na wafuasi wako mmekuja hapa mmeonyeshwa mifano mizuri sana.

    2.Elimu, madarasa yanayofaa, ombeni misaada ya vitabu siyo pesa kila wakati mpaka tumechokwa"" nakumbuka hapa DK kuna mbunge mmoja alisema tumechoka kutoa pesa all the time mara Africa mara Asia, sasa tuamue either Africa au Asia..maana ni kero

    3. Barabara vijijini, dispensary za maana karibu na wanavijiji, kumbuka muheshimiwa, mkulima anaenda kuuza mazao yake kwa kutumia PUNDA as usafiri tobaaa... vijiji vitano,wanunuliwe hata gari mmoja, wajue siku fulani zamu yetu kupeleka nafaka soko kuu, bushiiit na hayo marenji kruzzzaa ya wabunge, they do nooooothing,focus kwenye kilimo na Elimu, Hospitaly..
    4. Wabunge kuingia na vigeregere bungeni, hilo si bunge la CCM ni bunge la watanzania, kelele huko kwenye mduara, wanywe KAHAWA nyingi b4 kwenda kusikiliza Hotuba.
    Mwisho nduguzanguni CHILD protection na unyanyaswaji wa kina mama ukomeshwe.
    Mdau DK

    ReplyDelete
  26. AnonymousJune 11, 2009

    Nasikia kampuni ya Kagoda imepata hasara kwa kununua pamba ya wakulima. Ni kweli?

    ReplyDelete
  27. AnonymousJune 11, 2009

    Why are you not posting my comment Mr.Michuzi? Can you please upload it? Here it is:-

    "With all the due respect Mr.President, you are not correct! Uongozi wa serikali ya Mh.Kikwete inawapendelea matajiri ambao ni wachache kuliko masikini ambao ni wengi!! Poor Tanzanians!! Shame on you Mr.President! CCM(TZ)==Republicans(USA)!! I mean, how can you skip education strategy? Yaani hukutamka neno kuhusu "walimu", "wanafunzi", "elimu"! What a failing leadership...!! WHAT?? Inauma sana kuona leadership ya nchi haimaindi watu wake. This is 2009 man? Common Mr.President!? You are letting us down, you know? Not good, not good at all!!

    "Elimu ndio msingi wa maendeleo", Mr.President?! We have teachers who takes care of our children daily but goes long ways working without pay and with hard conditions..how can they really deliver qaulity education to the future generation of the nation? We have kids sitting down!? What about free education to machingas, wakulima etc? Why always your boys man? Just remember, we all have an ending day!! Someone else will be PRESDENT, and you will be responsible for lots of issues!!"

    ReplyDelete
  28. AnonymousJune 11, 2009

    "MCHUMI WA MAZINGIRA"[ENVIRONMENTAL ECONOMICS] NITAJIBU HOTUBA YA RAIS KWENYE KIPENGELE CHA UKUAJI WA UCHUMI.

    Environmental ndio bank inayosaidia ukuaji wa uchumi Tanzania na sehemu nyinginezo.Balaa linalotukuta sasa hivi la watalii kutokuja Tanzania,ndio linakuja si muda mrefu.Nasema linakuja kwa sababu zifuatazo.Labda Rais hana washauri wazuri au anapuuzia.Kutokana na serikali yetu kuweza kutoa leseni za kuua wanyama pori ,eti kwa ajiri ya kuingiza pesa,kweli hatuoni kuwa tunaingia shimoniiii jamaniiiiiiiiiiiii.Tuna wanyama pori wangapi hapo.kuna mtu kafanya sensa ya wanayama hapo.Kwa kweli lazima tujifunze kutokana na makosa ya nyuma.Wote tunajua Tanzania ilikuwa na Faru wengi sana,lakini sasa hivi hatuna hata mmoja,mpaka serikali ya south africa ikatupa faru wawili kama mbegu.Kweli jamani hao jamaa wa resource management wapo au wapo kisiasa tu hapo.Na ni nani anayemshauri rais wawekezaji wajenge hotel ndani ya mbuga?.kitendo hiki tayari kitawaweka wanyama wetu wa pori kupotea.Serikali yetu inategemea kwa kiwango kikubwa revenue kutoka katika sekta hii ya utalii.Na tunajua ndugu zetu wanapata kazi kutokana na kazi za hotel na kuwasaidia watalii huko mbugani.swali linakuja kweli kupata pesa za kigeni kwa kuua wanyama pori ni sustanable economy? au ni consumption economy?.Na kitendo cha serikali kuwatoa kwenye ardhi yao wahzabe[yaenda]ni busara jamani.?Eti kwa sababu huyo mwekezaji ana atajenga shule na zahanati.Jamani watanzania wenzangu naomba tusimame sasa hivi.hii nchi si ya rais wetu wala waziri fulani,wala mbunge fulani.Ni nchi ya Watanzania.Tuna haribu future ya ya watoto wetu jamani.Hakuna kitu tutawaachia.SUSTANABLE ECONOMICS INATEGEMEA KWA KIWANGO GANI TUNAVIBORESHA VICHOCHEO UCHUMI HIVYO.KAMA TUNAVIHARIBU HII TAKWIMU YAKO YA UKUAJI WA UCHUMI ITAZIDI KUCHUKA MWAKA HADI MWAKA NDIGU RAIS.NA VILE VILE UNATAKIWA UWE NA BUSARA MWENYEWE VILEVILE,SI KILA KITU UNACHOAMBIWA NA WEWE UNAONA SAWA HAPANA.NINI KIFANYIKE KUHUSU UCHUMI WETU.TUNATAKIWA WATU MUHIMU WAKUTANE HATA WATANZANIA WANAOSOMA NJE NA KUNA WATU SMART HAPO TANZANIA PIA.NA TUULIZANE NINI KIFANYIKE SIO MTU MMOJA AU WAWILI WANAFANYA HII KAZI.HALI NGUMU YA SASA NI KUTOKANA NA UZEMBE ULIOFANYIKA NYUMA.KWA HIYO TUNATAKA TUWE NA UCHUMI ENDELEVI SIO HUO AMBAO RAIS ANAUFAGILIA,BILA YA KUTAZAMA MBELE.WATANZANIA IPO HATARINI KUMALIZA RESOURCES ZAKE MUDA MFUPI UNAOKUJA.NA NINASEMA AMANI ITAPOTEA HAPO HARAKA SANA.KWANI WATU WATAKUWA WANAGOMBEA RESOURCES CHACHE ZILIZOBAKIA.TUNATAKIWA TUWE NA GREEN ECONOMY SIO DEPLETION ECONOMY HAPO.NA VITA ZITAANZIA HAPO KAMA UNAVYOONA HUKO ETHIOPIA NA SOMALIA.TUNATAKIWA TUSIKAE KIMYA SERIKALI TUNATAKIWA TUISAIDIE NA KAMA ITAKAA KIMYA,LAZIMA TUFANYE MAANDAMANO YA AMANI.MUNGU IBARIKI TANZANIA NA WATU WAKE.
    "ENVIRONMENTALIST"
    WASHINGTON DC

    ReplyDelete
  29. Hotuba kwa nani mbona hao wasikilizaji wenyewe wanachapa usingizi hapo? e.g. Mkulo akiwaongoza waliolala

    ReplyDelete
  30. AnonymousJune 12, 2009

    michu ata ukiminya...yani mibaba viongozi tuliowpa dhaman ya nchi yetu MNALALA?wakati wa hotuba ya nchi??nchi gani yenye viongozi wenye akili wanalala rais anapohutubia??SHAME

    ivi kwanini fani ya UALIMU Tanzania inadhalaulika saaaana na ni kitu cha mwisho eti mtu AKIFELI au kakosa la kufanya basi anaingia UALIMU!!!???WHAAAAAT

    ivi ndo mtegemee cream gani ya wanainchi na wasomi/wataalamu??

    lazima tubadilike yan ualimu A++ au km saaan umefeli B.
    Pia mishahara na marupulupu ya waalimu yaongezwe mana mazingira wanayofanyia kazi ni magumu na mbali saaaaaana.

    why wasibane madenti tuition??

    kingine..ni mfumo mzima wa MADAWA MSD asa ya kupunguza makali ya ukiwmi na magonjwa nyemelezi!!hamjui jinsi gani poor adherence ya izi dawa zinavotengeneza USUGU kwa mtu...!!!yani ni kituko ktk nchi Tz...sielewi presidaa umeliangaliaje hili,ukilinganisha majirani zetu tu east afrika

    inaboa sana

    ReplyDelete
  31. AnonymousJune 13, 2009

    KWA NINI RAIS ANAHUTUBIA AKIKAA CHINI KWENYE KITI NA MKULO AKISINZIA.JE HAMUONI MFANO RAIS BUSH ALIVYOKUJA TANZANIA MWAKA JANA JE ALIONGEA AKIWA AMEKAA? TUACHE UVIVU..RAIS SIMAMA HUO NDIO UTARATIBU WA NCHI ZOTE DUNIANI ISIPOKUWA TANZANIA PEKEE..JAMANI HAMUMUONI HATA HUYO OBAMA ANASEMA MASAA MAWILI AKIZUNGUMZA NA KUJIBU MASWALI MBALIMBALI KUTOKA PRESS TOFAUTI,SISI RAIS WETU ANAHUBIRI AKIKAA..HAKUNA MASWALI ZAIDI YA KUSOMA KWENYE KARATASI ANACHOTAKA KUSEMA...MBONA WAKATI WA NYERERE MARA NYINGI ALIKUWA AKISIMAMA.

    ReplyDelete
  32. AnonymousJune 13, 2009

    nyama uzembe,kuvimbiwa,kujibweteka

    no mazoezi,hawataweza kuhimili kusimama masaa 2 nyie watu!!

    ukishiba pesa nene

    ni hayo

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...