Jengo la machinjio la Mji wa Kilosa likiwa limezingirwa na maji ya mafuriko na hivyo kusababisha ng’ombe walioletwa kwa ajili ya kuchinjwa siku hiyo ya Desemba 26, mwaka huu kushindwa kuchinjwa kutokana na eneo hilo kujaa maji .
Ng’ombe walioletwa machinjioni kwa ajili ya kuchinjwa wakiwa wamezingirwa na maji ya mafuriko yaliyotokea asubuhi ya Desemba 26, mwaka huu katika mjini Kilosa.
Baadhi ya vijana wa eneo la Kata ya Kasiki na Mbumi wa Mjini Kilosa ,wakibeba kichwani mwao godoro kuepusha lisiloane na maji ya mafuriko kutoka mto Mkondoa yaliyotokea asubuhi ya Desemba 26, mwaka huu mjini humo kufuatia mvua zilizonyesha katika milima iliyopo Wilayani Mpwapwa na Kongwa, Mkoa wa Dodoma kuanzia wiki ya Christmas.

Baadhi ya vifaa vya wakazi wa Kata ya Kasiki na Mbumi za Mjini Kilosa vikiwa vimetolewa nje ya nyumba zao ili visisombwe na maji ya mafuriko yaliyotokea Desemba 26, mwaka huu mjini humo.
Gari aina ya Fuso lenye namba T 952 ABZ likiwa na magunia ya nafaka zilizookolewa kwenye moja ya nyumba iliyokumbwa na mafuriko Desemba 26, mwaka huu likijaribu kulivuta Gari jingine lililokwama eneo la mitaa ya Kata ya Kasiki, baada ya kutitia kutokana na kujaa kwa maji Barabarani kufuatia mto Mkondoa kufurika.
Diwani wa Kata ya Kasiki katika Mji wa Kilosa, Ahamed Islam ( kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, Ephrem Kalimalwendo, ( kulia) kwa pamoja wakimwongoza Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Issa Machibya ( nyuma kulia) kuweza kuangalia baadhi ya maeneo ya mji wa Kilosa yaliyokubwa na mafurikio ya maji asubuhi ya Desemba 26, mwaka huu.
Mkazi wa Kata ya Mbumi akiwa kabeba mikononi Cherehani yake kuepusha isiharibiwe na maji ya mafuriko yaliyotokea asubuhi ya Desemba 26, mwaka huu mjini humo baada ya mvua kubwa zilizonyesha kwenye milima iliyopo Wilayani Mpwapwa na Kongwa, Mkoa wa Dodoma kuanzia wiki ya sikukuu ya Christmas na kusababisha mto Mkondoa kufurika.
Wakazi wa nyumba moja iliyokumbwa na mafuriko wakiwa nje ya ya nyumba yao wakitafakari jinsi ya kujiokoa pamoja na mali zao zilizokuwemo ndani kama walivyokutwa eneo hilo asubuhi ya Desemba 26, mwaka huu mjini Kilosa.
Habari na picha zote na mdau John Nditi

MAFURIKO ya maji ya mvua ambayo hayajawahi kutokea kwa zaidi ya miaka 18 yameukumba mji wa Kilosa na kuwaathiri mamia ya wakazi wa Kata nne za Wilaya Kilosa, Mkoa wa Morogoro, kufuatiwa mvua za mfululizo kwenye miinuko ya milima ya Wilaya ya Mpwapwa na Kongwa, Mkoa wa Ddodoma na kusababisha Mto Mkondoa kufurika na nyumba 523 kuwa ndani ya maji na nyingine kumi kubomolewa.

Pia majengo mengine ya huduma za kijamii , zikiwemeo Shule mbili za Msingi ya Mkondoa na Madaraka , sambamba na Jengo la Ofisi ya Chama cha Mapinduzi ( CCM) Wilaya ya Kilosa na Machinjio ya Halmashauri ya Wilaya hiyo yamekubwa na mafuriko hayo kwa maji kujaa ndani.

Kufuatia kutokea kwa mafuriko hayo, wakati wa mji wa Kilosa aambao walikuwa wakijindaa kusherekea siku ya kupeana zawadi za Skikukuu ya Christmas ya Desemba 26, mwaka huu walilazimika kuziacha shughuli hizo na kuhangaikia kuokoa mali zao pamoja na maishayao kutokana na mji huyo kuzingirwa na maji .

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Ephrem Kalimalwendo, alisema hayo wakati alipotoa taarifa juu ya mafuriko hayo mbele ya mkuu wa Mkoa wa Morogoro , Issa Machibya, juzi ( Des 26) alipotembelea maeneo yaliyoathiriwa alisema mafuriko hayo ambayo yalitokea asubuhi ya siku hiyo kufuatia Mto Mkondoa kuacha mkondo wake.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji hiyo kuwa, maji hayo yalisababisha sehemu kubwa ya makazi ya watu wanaoishi mjini humo kujaa maji na kuingia ndani ya nyumba kadhaa za watu na kuwafanya mamia ya wakazi wake kukosa mahali pa kuishi.

Kalimalwendo, alizitaja Kata zilizoathiriwa zaidi na mafuriko hayo kuwa ni Mbumi na Kasiki, nyingine zilizokubwa na athari hizo ni Kata ya Mkwatani eneo la Kichangani , Kata ya Magomeni na Kata ya Mabwelebwele , ambayo imetenganishwa kimawasiliano ya barabara na mji wa Kilosa.

“ mafuriko haya ni makubwa na hajayawahi kutokea …wataalamu wetu wamesema ni ya ujazo wa sentimita 75 na yameanza asubuhi ya saa 12 ya Desemba 26, mwaka huu ambayo ni wiki ya sikukuu ya Christmas na yameathiri sehemu kubwa nyumba za watu binafsi “ alisema Mkurugenzi Mtendaji huyo .

Hata hiyo aliongeza kusema “ pia mafuriko haya yameathiri maeneo ya huduma za umma nayo yameethirika , kuwa chini ya maji ambayo ni Ofisi ya CCM ya Wilaya , Machinjio, Shule mbili za msingi na nyumba 523 zipo kwenye maji na kati ya hizo kumi zimedondoka chini kutokana na mafuriko haya …lakini tunashukuru hakuna kifo hadi sasa” alisema.

Alisema Serikali ya Wilaya hiyo kufuatia mafuriko hayo, imetenga maeneo ya kuwahifadhi kwa muda wote waliokubwa na athari hizo kwa nyumba zao kujaa maji kwa kuwapangia maeneo ya Kilosa Klabu, Shule ya Msingi Mazinyungu, Ofisi ya Mamlaka ya Mji Ndogo Kilosa na kwenye majengo mawili ya Ofisi za Kata za CCM ya Mbumi na Kasiki.

Kata hizo mbili zilizoathirika zaidi na mafuriko hayo kutokana na takwimu iliyotolewa na Diwani wa Kata ya Kasiki , Ahamed Islam , kuwa Kata hiyo ina wakazi zaidi ya 5,400 , ambapo Diwani wa Kata ya Mbumi, Mwanaisha Mbaruku kuwa Kata yake ina jumla ya wakazi wapatao 4,200.

Hata hivyo alisema, hatua mbalimbali zimechukuliwa zikiwemo za huduma za kijamii pamoja na kuweka tahadhari ya kuweza kujitokeza kwa magonjwa ya mlipuko , sambamba na kuwahimiza wakazi wa Mji wa Kilosa kuhakikisha wanaiweka mijereji ya maji katika mazingira ya usafi wakati wote.

Nao baadhi ya wananchi waliokubwa na mafuriko hayo walisema kwa nyakati kuwa maji yaliyotokana na mvua zilizonyesha kwenye milima ya Wilaya ya Mpwapwa na Kongwa , Mkoa wa Dodoma ndiyo kiini cha mafuriko hayo baada ya mto Mkondoa unaokatika katikati ya mji huo kujaa kupita kiasi.

Mkazi wa Kata ya Mbumi , Mariamu Mbonde, ambaye ni kati ya walioathiriwa na mafuriko hayo, pamoja na Farida Kajua , walisema kwa nyakati tofauti kuwa , mafuriko hayo hayajawahi kutokea kwa kipindi kirefu tangu mwaka 1992 ambapo yalisababisha nyumba nyingi kubomolewa.

Naye Bibi Kizee Mariamu Hassan , ambaye aliweza kuokolewa na ndugu zake wakaribu , alisema kuwa maji yalianza kuingia katika nyumba yake saa 12 asubuhi ya Desemba 26, mwaka huu na kuendelea kujaa na kusababisha ukuta mmoja wa nyumba yake kuanguka na hivyo kuhifadhiwa na majirani zake pamoja na mjukuu wake.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Machibya , baada ya kuwatembelea waathirika hao waliwapa pole na kuhahidi kuwa Serikali ya Mkoa itakuwa bega kwa bega katika kuhakikisha misaada itakayotakiwa kutolewa ina tolewa yakiwemo mahema kwa watu ambao nyumba zao zimebomolewa na mafuriko hayo.

“ tayari tumezungumza na Jeshi la Wananchi wa Tanzania ( JWTZ) wamekubali kutoa mahema na wengine ni wenzetu wa Chama cha Msalaba Mwekundu ..wameahidi kutisaidia pia Mahema na misaada mingine ya kibinadamu” alisema Machibya.

Hata hivyo aliutaka uongozi wa Wilaya ya Kilosa kuhakikisha unachukua tahadhari zote ili kuzuia kujitokeza kwa magonjwa na mlipukio na kuwazuia wakazi wale ambao nyumba zao zipo katika hatari ya kubomoka wasiendelee kuishi ndani ya nyumba hizo kwa lengo la kuepusha madhara ya kibinadamu.

Kwa mujibu wa baadhi ya wananchi wa mji huo wa Kilosa, kuwa mafuriko hayo yamekuwa yakitokea kila mara na yanasambishwa na kina cha mto Mkondoa kuhama na kuelekea kwenye makazi ya wananchi na mvua zinaponyesha nyingi maeneo ya uwanda wa juu wa milima ya Kilosa, Mpwapwa na Kongwa husababisha mafuriko hayo.







Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 4 mpaka sasa

  1. daha bongo africa tambarare jamano waungwanio ee.tsunami tena badaa ya miakaa mitano sasa

    mdau beijum

    ReplyDelete
  2. POLENI SANA, LAKINI TUITUMIE HIYO MVUA VIZURI KWA NA KWA USAHIHI KWA AJILI YA KILIMO. PIA SERIKALI INAPASWA KUSAIDIA HAO WATU, KWANI HAPO SIONI CHOMBO CHOCHOTE CHA SERIKALI JAMANI, HUO NDO UTAWALA BORA!

    ReplyDelete
  3. Pole sana diwani wa kasiki ahmed a.k.a kabuma jitahidi kuwaelimisha waishio mabondeni kama kwa behewa nk
    mlosa orginal ugaibuni

    ReplyDelete
  4. BASI HAPO SERIKALI ITATOA VIJISENTI MBUZI,LAKINI IKIFIKA KWENYE UJENZI WA NYUMBA YA GAVANA HAKUNA LIMIT YA KU-SPEND NI OVER 1.4 BILLION..HAO WALIOKUMBWA NA MAFURIKO NI WATANZANIA WANAOSTAHILI MSAADA WA KUTOSHA TOKA KWA SERIKALI YAO..MUNGU IBARIKI AFRICA NA UIPONYE NA GONJWA HILI BAYA LA WIZI NA UONEVU KWA WANYONGE

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...