Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt. Hadji Mponda.

Na. Aron Msigwa –MAELEZO.

Serikali imesema hali ya maambukizi na idadi ya wagonjwa wa Ukoma nchini inaendelea kupungua mwaka hadi mwaka kutokana na juhudi mbalimbali zinazochukuliwa kukabiliana na ugonjwa huo.

Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es salam na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Hadji Mponda wakati akitoa Tamko kuhusu maadhimisho ya Siku ya Ukoma Duniani ambayo kitaifa itafanyika mkoani Lindi.

Amesema idadi ya wagonjwa wa Ukoma imepungua kutoka wagonjwa 35,000 mwaka 1983 hadi kufikia wagonjwa wapatao 2,600 kwa mwaka 2009 huku takwimu za mwaka 2009 zinaonyesha kuwa ,asilimia 11 ya wagonjwa wapya waliogunduliwa tayari walikuwa wamekwishapata ulemavu wa kudumu.

“Wagonjwa wengi wamekuwa wakipata madhara ya ugonjwa wa Ukoma kutokana na kuchelewa kwenda kwenye vituo vya afya kwa uchunguzi na matibabu” Amebainisha.

Ameeleza kuwa takwimu za mwaka 2009 zinaonyesha kuwa hali ya maambukizi ya ugonjwa wa Ukoma bado ni kubwa katika mikoa ya Lindi wagonjwa 176, Rukwa wagonjwa 376, Dar es salaam wagonjwa 386 na mkoa wa Mtwara ambao una wagonjwa 175.

Amesema kuwa serikali kwa kutambua athari za ugonjwa huo na umuhimu wa kuzuia ulemavu utokanao na ukoma imeweka msisitizo kupitia kauli mbiu ambayo ni “Pambana na Ulemavu Utakanao na Ukoma” ili kuhimiza ushiriki wa jamii nzima katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukoma.

“Ninapenda kuwahimiza wananchi wote kuwa wakiona dalili za ugonjwa wa ukoma ambazo ni baka au mabaka kwenye ngozi yasiyo na hisia ya mguso ambayo huambatana na ganzi kwenye mikono na miguu wawahi kwenye vituo vya tiba kwa ajili ya uchunguzi na kupatiwa matibabu sahihi ya ugonjwa wa ukoma ambayo hutolewa bila malipo”

Dkt. Mponda ameongeza kuwa serikali imekuwa ikiwahudumia waathirika wa ugonjwa wa ukoma ikiwemo kugharimia jozi za viatu maalum 7000 kila mwaka kwa wale walioathiriwa na ukoma bila malipo ili kuzuia athari na kupunguza ulemavu utokanao na kuharibiwa kwa mishipa ya fahamu, huduma za marekebisho ambazo ni pamoja na huduma za upasuaji, viungo bandia, magongo na viti mwendo .

Aidha ametoa wito kwa jamii kutowanyanyapaa wala kuwatenga wagonjwa wa ukoma kutokana na mila potofu na ukosefu wa uelewa kuhusu ugonjwa huo huku akisisitiza kuwa mtu ambaye yupo kwenye matibabu hata kama ana ulemavu hawezi tena kuambukiza ugonjwa huo na anastahili kuishi katika jamii.

Kwa upande wake Meneja wa Programu ya kupambana na Ugonjwa wa Ukoma nchini Dkt.Said Egwaga amefafanua kuwa wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inaendelea kupambana na ugonjwa huo huku akibainisha kuwa dawa za matibabu kwa ajili ya wagonjwa zinapatikana tofauti na miaka ya nyuma ambapo wagonjwa waliwekwa kwenye kambi maalum.

“Miaka ya nyuma hakukuwa na tiba ya ukoma tulikuwa na kambi maalum kwa ajili ya waathirika lakini sasa wagonjwa wa ukoma hawapelekwi tena kwenye kambi isipokuwa hupewa dawa ambazo huzitumia majumbani mwao”

Ameongeza kuwa Wizara kupitia kitengo cha Ustawi wa jamii imekuwa ikiwaangalia waathirika wa ukoma wakiwemo walemavu kwa kuwapatia misaada ikiwemo ujenzi wa makazi yao na kuwasaidia katika shughuli za kilimo.

Siku ya Ukoma Duniani iliasisiwa takribani miaka 56 iliyopita kwa lengo la kuielimisha jamii kuhusu ugonjwa wa ukoma na huadhimishwa ulimwenguni kote kila jumapili ya mwisho wa mwezi januari kila mwaka.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...