Wakati Kamati ya utendaji ya Simba ikimsimamisha mwenyekiti wake Ismail Aden Rage, imewafungashia virago makocha wake Abdallah Kibadeni 'King' na msaidizi wake Jamhuri Kiwehlo 'Julio' kuinoa timu hiyo yenye maskani yake mtaa wa Msimbazi.

Akizungumza na Makao Makuu ya klabu hiyo mchana wa leo, Kaimu Mwenyekiti wa Simba Joseph Itang'are 'Kinesi' alisema kikao cha kamati ya utendaji kilichokaa jana usiku kimefikia uamuzi wa kumsimamisha mwenyekiti wao kwa kile walichoeleza kutokuwa na imani nae baada ya kushindwa kuitisha mkutano mkuu wa mabadiliko ya katiba.

Hii itakuwa mara ya pili kwa Rage, kusimamishwa ndani ya klabu hiyo,awali alisimamishwa mapema mwezi Machi, baada ya wanachama kufanya mapinduzi ya kumuondoa Rage akiwa kwenye matibabu nchini India hata hivyo aliporudi alisema hatambui mapinduzi hayo na kuitisha mkutano alioufanya kwenye ukumbi wa Bwalo la Polisi Oyestabay huku akiadi kuitisha mkutano mkuu wa dharura wa mabadiliko mapema mwezi Agosti hata hivyo aliharisha kwa kile alichoeleza ni kupisha mwezi mtukufu wa Ramadhani.


Lakini jana Kinesi alisema "Mkutano mkuu wa mwaka ulikuwa ufanyike mwezi huu wa Novemba na ajenda kubwa ni mabadiko ya katiba, lakini cha kushangaza Rage amewambia wanachama hakuna mkutano mpaka mwakani na ameondoka yupo nje ya nchi.


"Sasa hii ni ukiukwaji wa katiba, hatuna imani naye na hata kama angekuwepo tungemueleza wazi kitendo chake hatukiafiki na hatuna imani naye, tumemsimamisha mpaka Desemba Mosi na hii ni kwa mujibu wa katiba ya Simba kifungu cha 30.


Kinesi alisema Desemba Mosi ndio utafanyika mkutano mkuu wa wanachama na hatma ya Rage itajulikana kwenye mkutano huo iwapo wanachama wataridhia kumuondoa au wataamua adhabu yake ya kumsimamisha iendelee au arejeshwe kundini kumaliza muda wake ambao unafikia ukingoni Aprili Mwakani.


Mbali na Rage, pia rungu hilo la Kamati ya utendaji limeangukia benchi ya ufundi la klabu hiyo baada ya kuwafungashia virago Abdallah Kibadeni 'King' na Jamhuri Kiwehlo 'Julio' kutokana na mwenendo mbovu wa timu yao iliyomaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi ikiwa inashika nafasi ya nne ikiwa na pointi 24.

Kinesi alisema nafasi ya Kibadeni itachukuliwa na aliyekuwa kocha wa timu ya Gor Mahia Zdravko Logarusic raia wa Crotia akisaidiwa na Seleman Matola. Alisema kocha huyo atatua nchini Desemba Mosi na timu itaanza rasmi mazoezi Desemba 2 kujiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi.

Kibadeni alipoulizwa kuhusiana na suala hilo alisema "Nashukuru nimeacha timu kwenye nafasi nzuri, kilichofanyika ni demokrasia naheshimu hilo, bado nitaendelea kuwa mwanachama wa Simba, na bado nina mkataba na klabu hiyo, nitafatilia nipate haki yangu.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 3 mpaka sasa

  1. Hee! We Mzee Kinesi! wewe si unaikaimu hiyo nafasi uliyopo!sa umeanza kutimua waliochaguliwa na wanachama! Mnatuletea fujo hatupendi ujue!!!Nenda hata pale tandale sokoni pana timu pale waombe uongoze SIO SIMBA SC.Simba tunachaguana kidemokrasia baada ya mtu kujieleza,la subiri Uchaguzi!!!!

    ReplyDelete
  2. Jamani Bongo tuache masiala na mchezo, kweli mpira utaendelea namna hii. Na jamaa Bongo wasanii mno kwa nini mnangojea mpaka Rage yuko nje' ya nchi ndiyo mnapindua timu?!! Yaani hii hizi sinema za Bongo zinanishinda kabisa. Nilikuwa napanga kurudi nyumbani kufundisha mpira, lakini kwa style hii nashindwa kuelewa kabisa na siwezi. Samahani jamaa zangu Bongo muendelee kusema jamaa wa Bongo wakifika majuu "wanalinga tu". Nitakuja kuwapa moyo na support lakini mtu naitaji stability.

    ReplyDelete
  3. Mhhhhh mpira ni mtihani mkubwa sana ukiwa kiongozi mkifungwa unafukuzwa. Makubwa tumeona makocha wengi sana wakifukuzwa kwa ajili ya magozi. Jamani kwani magoli ni nini. Wajipande kwa mengine sasa.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...