Na Miza Othman Maelezo Zanzibar
Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu amesema ucheleweshwaji wa kesi katika Mahakama za Zanzibar unasababishwa na mambo mengi ikiwemo kukosekana mashahidi na kutokamilika kwa upelelezi na ukosefu wa vitendea kazi. 
Hayo ameyaeleza leo huko Ofisini kwake Vuga wakati alipokuwa akizungumza na waaandishi wa Habari juu ya sherehe ya siku ya sheria Zanzibar ambayo itaadhimishwa tarehe 10 Februari 2014. Amesema kaulimbiu ya maadhimisho hayo mwaka huu ni “Saidia mahaka kutenda haki “ ikiwa na lengo wadau wote wa mahakama kutoa mchango wao kuiwezesha mahakama kutenda haki. 
“Kesi sio mahakama pekee wadau wengi wanahusika na kila mmoja anapaswa kutekeleza wajibu wake katika utolewaji wa haki lakini inayolaumiwa zaidi ni Mahakama kwa sababu utoaji wa haki unamalizia hapa” alisema Jaji Mkuu. 
Amesema kesi za jinai mara nyingi huanzia Polisi na baadae kupelekwa kwa Mkurugenzi wa Mshtaka na hatimae kuwasilishwa mahakamani kwa mashtaka lakini mahakama hushindwa kumaliza kesi kwa haraka kutokana na kukosekana mashahidi na kutokamilika upelelezi. Kwa upande wa kesi za madai Jaji Mkuu amesema zimekuwa na changamoto nyingi baadhi ya wakati mdaiwa hajulikani alipo na mdai anashindwa kuwa na mawasiliano naye. 
Jaji mkuu wa Zanzibar ameongeza kuwa baadhi ya wakati bajeti nayo inakuwa ni kikwazo kwani imekuwa haitoshi na haipatikani kwa wakati. 
Amesema siku ya sheria Zanzibar itatoa nafasi kwa wadau wa mahakama ikiwemo Polisi Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka na serikali kukaa pamoja kutafakari njia zilizobora za kuendesha kesi kwa haraka. 
Akizungumzia malalamiko ya rushwa katika mahakama, amesema suala hilo linachangamoto nyingi kwani rushwa hutolewa kwa njia ya siri lakini amewashauri wananchi wanaoombwa rushwa kutoa taarifa kwa Mamlaka ya Kuzuia Rushwa kwa hatua zaidi. 
Hata hivyo amekumbusha kuwa suala la rushwa ni kosa linalowahusu mtoaji na mpokeaji hivyo amewataka wananchi kutokuwa tayari wanapoombwa rushwa ili kuepuka kuingia kwenye makosa. Jaji Makungu amesema kabla ya kilele cha sherehe hiyo kutakuwa na harakati mbali mbali ikiwemo mdahalo wa wanafunzi utakaozungumzia umuhimu wa heria na vipindi vya Televisheni na Radio ambavyo vitahusu juu ya siku hiyo.
Jaji Mkuu wa Zanzibar Mhe. Omar Othman Makungu akizungumza na waandishi wa habari juu ya sherehe ya siku ya sheria Zanzibar ambayo itaadhimishwa tarehe 10 Februari 2014.  Mkutano huo ulifanyika  Ofisini kwake Vuga, Mjini Zanzibar.
 Mwandishi wa habari wa Idara ya Habari Maelezo Ramadhani Ali akimuuliza swali Jaji Mkuu wa Zanzibar (hayupo pichani)  wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari.
 Jaji Mkuu wa Zanzibar Mhe. Omar Othman Makungu akitoa ufafunuzi wa jambo wakati wa mazungumzo yake na waandishi wa habari yaliyofanyika ofisini kwake Vuga mjini Zanzibar.
Baadhi ya watendaji wa Mahakama ya Vuga mjini Zanzibar na waandishi wa habari wakimsikiliza Jaji Mkuu wa Zanzibar Mhe. Omar Othman Makungu (hayupo pichani) wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika ofisini kwake Vuga, Mjini Zanzibar leo.
(Picha na Makame Mshenga wa Maelezo Zanzibar).

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...