Mitaji ya ubia imetajwa kama mpango unaoweza kuongeza nguvu katika miradi ya wafanyabishara nchini na kuchangia uchumi na ustawi wa jamii.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji, Dkt. Mary Nagu aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam hivi karibuni kuwa kukubalika kwa mpango wa mitaji ya ubia ni moja ya utayari wa serikali katika kuweka mazingira ya kuifanya sekta binafsi kuwa injini ya uchumi hapa nchini.
“Hiki ni chanzo mbadala cha mitaji ya biashara...kwa sasa bado mazingira ya upatikanaji wa mitaji kwa wafanyabiashara sio rafiki,” alisema.
Alisema watanzania wanapenda kuwekeza lakini hawana sehemu nzuri ya kupata mitaji kuendeleza biashara zao, hivyo ni jambo jema kama mpango wa mitaji ya ubia utaimarishwa hapa nchini.
Dkt. Nagu alikuwa akifungua mkutano wa siku moja uliokuwa ukiongelea jinsi sekta binafsi inavyoweza kufaidika na mitaji ya ubia.
Mkutano huo ulitayarishwa na Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF) kwa kushirikiana na TMS Consultants Ltd.
Waziri Nagu aliipongeza TPSF kwa juhudi zake za kuleta na kuimarisha upatikanaji mitaji kwa watanzania.
Aliwataka watanzania kuchangamkia fursa mara mpango huo utakaposhika kasi ili wasiwe watazamaji katika uchumi bali wawe washiriki kamili katika kujenga nchi yao.
“Uchumi wetu unahitaji kuondoka kwenye ukuaji wa asilimia 6.7 na kufikia asilimia 10 hadi 11...na hiyo inawezekana kama tutaongeza kasi ya uwekezaji,” alisema.
Naye Mwenyekiti TPSF, Dkt. Reginald Mengi alisema watu nchini wanaotaka kuingia katika biashara na waliopo kwenye biashara wana tatizo kubwa la kupata mitaji ya kifedha.
“Tunayo mitaji mingine kama ya rasilimali za nchi lakini kikwazo ni mitaji fedha,” alisema.
Alisema taasisi yao imeona umuhimu wa kupata mitaji nje ya benki ili watanzania waweze kushirikina na wabia kutoka ndani na nje ya nchi wenye mitaji ili kwa pamoja waweze kushirikiana kutekelea miradi mikubwa.
Pia alisema watu wanahitaji kuondokana na dhana kuwa watanzania hawawezi kufanya biashara kubwa, bali kinachotakiwa ni kuwa na mawazo mapana ya kibiashara na hatimaye kuitimiza ndoto.
Alisisitiza kuwa watanzania wanauwezo wa kufanya biashara kubwa kama wanavyofanya mataifa mengine, kikubwa ni kujiamini na kuwa na malengo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Bw. Godfrey Simbeye alisema mfumo huu wa mitaji ya ubia unatoa fursa kwa wenye mitaji mikubwa kuingiza mitaji yao, ujuzi na teknolojia kwenye miradi au kampuni ambazo zina miradi lakini zinashindwa kufikia malengo.
Alisema muda umefika kwa wafanyabiashara nchini kuingia katika soko la mitaji ya ubia kwa kuwa mitaji hiyo siyo mikopo.
Bw. Simbeye alisema tatizo la kukosa mitaji ni kubwa sana kutokana na masharti magumu katika mifumo ya kibenki hapa nchini kwa maendeleo ya sekta binafsi.
Alisema Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano na Dira ya Taifa ya maendeleo 2025 zinaelekeza kuimarisha uwekezaji kama moja ya kufikia ustawi wa jamii na kuwa mfumo huo wa mitaji ya ubia unauwezo mkubwa wa kufanikisha hilo.
Akitoa mfano alisema nchi za Afrika ambazo zimenufaika na mitaji ya ubia ni pamoja na Kenya, Nigeria na Afrika Kusini na kusema hakuna sababu kwanini Tanzania isifanikiwe kupitia mpango huo.
“Mfumo huu unatumika hapa nchini, ingawa ni kwa kiwango kidogo, sasa tunaona kuwa wakati wa kufaidika na fursa hizi kwa kiwango kikubwa ni sasa,” alisema.
Mwenyekiti
wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Dk. Reginald Mengi akiongea wakati
wa semina iliyoongelea jinsi ya kuimarisha mitaji ya ubia Tanzania jijini Dar
es Salaam hivi karibuni. Kulia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Waziri Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji, Dkt. Mary Nagu na Mkurugenzi Mtendaji wa
TPSF, Bw. Godfrey Simbeye.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu,
Uwekezaji na Uwezeshaji, Dkt. Mary Nagu akipungia
wajumbe baada ya kufungua semina iliyoongelea jinsi ya kuimarisha mitaji ya ubia
Tanzania jijini Dar es Salaam hivi karibuni.
Kushoto ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Dk.
Reginald Mengi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...