Mkurugenzi Mtendaji wa T-Marc Tanzania Diana Kisaka akizungumza na wadau kuhusu majukumu ya T-Marc.
Mkurugenzi Mtendaji wa T-Marc Tanzania Diana Kisaka akiwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu, mgeni rasmi wa uzinduzi wa mradi wa kuhamasisha jamii kuhusu huduma za uchunguzi wa Saratani ya Shingo ya Kizazi uliondaliwa na taasisi isiyo ya Kiserikali ya T- Marc Tanzania katika mkutano na wadau mbalimbali wa afya mkoa wa Iringa uliofanyika katika ukumbi wa chuo cha Veta.
Baadhi ya wadau waliohudhuria uzinduzi wa mradi wa kuhamasisha jamii kuhusu huduma za uchunguzi wa Saratani ya Shingo ya Kizazi uliondaliwa na taasisi isiyo ya Kiserikali ya T- Marc Tanzania katika mkutano na wadau mbalimbali wa afya mkoa wa Iringa uliofanyika katika ukumbi wa chuo cha Veta.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu
======== ======= ========
ASILIMIA 25 YA WANAWAKE WAKO HATARINI KUPATA SARATANI YA SHINGO YA UZAZI.
Na Denis Mlowe,Iringa
IMEBAINIKA asilimia 25 ya wanawake nchini Tanzania wako katika hatari kubwa ya kupata ugonjwa wa Saratani ya shingo ya Uzazi katika maisha na kusababisha vifo kwa wanawake nchini.
Kwa mujibu wa takwimu asilimia 80 ya wagonjwa wanaogundulika na aina hii ya saratani hugundulika katika hatua kubwa ya ugonjwa ambapo hakuna tiba wala kinga.
Hayo yamebainishwa na Katibu Tawala wa mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu wakati wa uzinduzi wa mradi wa kuhamasisha jamii kuhusu huduma za uchunguzi wa Saratani ya Shingo ya Kizazi uliondaliwa na taasisi isiyo ya Kiserikali ya T- Marc Tanzania katika mkutano na wadau mbalimbali wa afya mkoa wa Iringa uliofanyika katika ukumbi wa chuo cha Veta.
Alisema asilimia kubwa ya wanawake nchini Tanzania wanatakiwa kujitokeza kwa wingi kuangalia afya zao na kupima saratani ya shingo ya uzazi kuweza kubaini kama wameathirika na kupata matibabu mapema.
Wamoja alisema takwimu kutoka taasisi ya Saratani ya Ocean Road inaonyesha kati ya wagonjwa wa saratani wanaopelekwa katika taasisi hiyo kila mwaka zaidi ya wagonjwa 5000 wanatatizo la saratani ya shingo ya kizazi.
“Kwa kutambua hilo serikali ya Tanzania kupitia wizara ya afya na ustawi wa jamii inafanya juhudi mbalimbali katika kupambana na saratani ya mlango wa uzazi kwa wanawake kwa sababu saratani ya mlango wa kizazi inatibika ila tu ili iweze kutibika ni muhimu kwanza igundulike katika hatua zake za awali” alisema Ayoub
Aliongeza kuwa wataalamu wa mambo ya saratani wamegundua kuwa kuna uhusiano mkubwa kati ya saratani ya mlango wa kizazi na maambukizi ya virusi vya Ukimwi.
Alisema kutokana na tatizo la saratani ya mlango wa kizazi mkoani Iringa serikali imewataka wadau mbalimbali kujitokeza na kuunga mkono ili kuhakikisha wanawake wanakuwa salama kutokana na tatizo hilo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa T- Marc Tanzania,Diana Kisaka alisema kuwa kila mwaka wanawake 6000 hugundulika kuwa na saratani ya mlango wa kizazi Tanzania.
Alisema wanawake 4000 wa kitanzania hufa kila mwaka kutokana na saratani ya mlango wa kizazi sawa na wanawake 11 wanaofariki kila siku nchini kutokana na tatizo hilo.
Kisaka alisema takwimu za hospitali ya Ocean Road zinaonyesha asilimia 40 ya vifo vinatokana na matatizo ya saratani ni wagonjwa saratani ya mlango wa kizazi.
“Takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 80 ya wagonjwa wote wanaokwenda kwenye matatibu ya saratani ya shingo ya uzazi hufanya hivyo wakiwa wamechelewa, hii ina maana kuwa wagonjwa hawa hutafuta huduma za tiba wakati saratani yao tayari imefikia kiwango ambacho haiwezi kutibika” alisema Kisaka.
Alisema ugonjwa wa Saratani ni tatizo kubwa sana ulimwenguni na hasa katika nchi zinazoendelea ambapo takwimu za kimataifa zinaonyesha kuwa kila mwaka zaidi ya watu milioni 5 hugundulika kuwa na saratani na kufanya tatizo hilo kufikia asilimia 29 huku kati yao hupatikana na saratani ya mlango wa kizazi na kwa bahati mbaya Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye tatizo kubwa la ugonjwa huo
Alisema moja ya sababu zinazochangia tatizo la saratani ya shingo ya uzazi ni ukosefu wa taarifa sahihi kuhusu umuhimu wa watu kuchunguza afya zao mara kwa mara, Imani potofu na kukosa taarifa halisi kuhusu saratani na matibabu ya mionzi.
Kisaka alisema kwa kutambua tatizo hilo T-MARC kama asasi isiyo kuwa ya kiserikali ambayo inajishughulisha na uboreshaji wa afya ya watanzania kwa kushirikiana na serikali kupitia wizara ya Afya na ustawi wa jamii pamoja na wadau mbali mbali wa sekta ya umma ,sekta binafsi ,wadau wa kimataifa ,asas za kijamii na watanzania wote kwa ujumla kwa kuanza kupambana na tatizo hilo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...