UTAMADUNI huu ulioanza wa waamini licha ya kusali, pia wakaenda kusherehekea sikukuu hizi za kiroho ni mgeni na mzuri kwa kuwa unawajenga watu kiroho, na kuwaepushia uwezekano wa kutumbukia katika matatizo kwa kwenda katika maeneo mbalimbali ya sterehe; Amesema Askofu Method Kilaini.
Mhashamu Kilaini ambaye ni Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, ameyasema hayo alipozungumza na Gazeti hili kuhusu Tamasha la Pasaka linalotarajiwa kufanyika katika jiji la Dar es Salaam, Aprili 20 mwaka huu ambayo ni Sikukuu ya Pasaka.
Mwaka huu Sikukuu ya Pasaka inaangukia Jumapili ya Aprili 20, Tamasha la Pasaka linatarajiwa kufanyika katika mikoa mbalimbali nchini kwa siku tofauti kuanzia Siku hiyo ya Pasaka. Akifafanua faida za Tamasha la Pasaka na mengine ya kidini kama Tamasha la Krismasi, Mhashamu Kilaini amesema yanasaidia kuifanya dini isiishie kanisani pekee kwa siku za sikukuu mfano Pasaka na Krismasi, badala yake kuifanya iende hata katika maeneo ya starehe yanayozingatia usafi wa kimwili na kiroho.
“…Wakienda kwenye matamasha kama hili la Krismasi, watu waanze kwa sala, maombi na hata mahubiri kidogo ili waendeleze moyo wa kumpenda Bwana (Yesu Kristo) maana katika matamasha kama haya, hakuna ulevi, uzinzi wala ufuska,” amesema Mhashamu Kilaini.Akaongeza, “Utamaduni huu wa kusherehekea siku za Sikukuu katika Jina la Bwana katika matamasha ni mpya, lakini pia ni mzuri maana unawaondoa watu katika vishawishi vya kuhangaikia katika mambo yanayowatia hatarini kimwili na kiroho na kulazimisha matumizi ya pesa yasiyo ya lazima….”
Amesema ili kushirikishana neema na baraka katika matamasha kama hilo la Pasaka, ni vema waamini wakajitokeza na kwenda kwa pamoja kama familia ili wafurahie kwa kufahamiana vema zaidi na Wakristo wenzao. Hata hivyo amesema katika sikukuu kama hizi, ni vema pia kuzingatia suala la usalama wa familia kwa kuhakikisha kuna ulinzi ili kuepusha uwezekano wa kufanyika vitendo vya kihalifu. “…Kwa yule anayependa kukaa na familia yake nyumbani, akae nyumbani, badala ya kwenda katika baa na sehemu nyingine zinazohatarisha imani, amani na usalama wake,” amesema. Tamasha hilo linatarajiwa kuwashirikisha wadau mbalimbali wakiwamo waimbaji maarufu wa muziki wa Injili toka ndani na nje ya nchi.
Kampuni ya Msama Promotions inayoandaa Tamasha la Pasaka mwaka 2014 imekuwa ikiendesha upigaji kura kwa njia ya ujumbe mfupi za maandishi za simu za mkononi (sms) ili waumini na wapenzi wa Tamasha la Pasaka wamchague mgeni rasmi, waimbaji wanaotaka watumbize katika tamasha hilo pamoja na mikoa wanayoitaka. Zoezi la upigaji kura linaendelea.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Tamasha hilo, Alex Msama amenukuliwa na vyombo vya habari akiutaarifu umma kuwa, kupitia upigaji kura huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete anaendelea kuongoza kwa kura za kuwa mgeni rasmi katika Tamasha hilo zilizofikia milioni 6.9 idadi ambayo haijafikiwa na kiongozi mwingine yeyote.
Habari zinasema katika kura hizo, Rais Kikwete anafuatiwa na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania Edward Lowassa, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe na Waziri wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta, Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe, Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP, Regnald Mengi na Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Ufunuo na Uzima, Josephat Gwajima. Kwa upande wa muziki wa Injili, waimbaji kadhaa wamekwishachomoza miongoni mwao wakiwa ni Upendo Nkone, Upendo Kilahiro, Voice Acapela na Sarah Kiare kutoka Kenya.
Hivi karibuni, waimbaji Rose Muhando na John Lisu wamewashukuru mashabiki wa Tamasha la Pasaka kwa kuwapigia kura nyingi zilizowahakikishia kushiriki katika Tamasha hilo. Mchuano mkali kumpata mgeni rasmi kwa upigaji kura huo ulikuwa hasa baina ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Regnald Mengi, Mwangalizi Mkuu wa WAPO Mission International Askofu Mkuu Sylvester Gamanywa na Mchungaji wa Kanisa la Maombezi (GRC), Anthony Lusekolo maarufu kama “Mzee wa Upako”.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...