KANISA la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) mkoa wa Morogoro limetoa wito kwa jamii kuungana na Mkurugenzi wa Msama Promotions, Alex Msama katika kipindi hiki cha Pasaka kutumia kidogo ambacho Mungu amewajalia kuwakumbuka wenye mahitaji maalum kama vile walemavu, wajane na yatima.Wito huo umetolewa na Mchungaji Raymond Dunia wa kanisa hilo akiwa na nia ya kuwakumbusha Wakristo kuwa na moyo wa kujitolea hasa kwa wenye mahitaji maalum.
Anasema kuwa lengo la Msama kusaidia jamii kupitia matamasha ya nyimbo za injili ni lengo zuri kwa kipindi hiki cha Pasaka, kwani ni wakati wa ukombozi kwa waliokandamizwa, Pasaka ni furaha kwa walio wahitaji, pia Pasaka ni amani kwa watu wenye mashaka ya maisha yao.
Anaongeza kwa kusema kuwa kupitia matamasha ya nyimbo za injili watu wengi wanaokolewa, hivyo ni njia mojawapo ya kusababisha watu waokolewe. “Wapo watu wenye mipango bora ya kusaidia jamii, lakini wanapofanikiwa wanajihudumia wenyewe. Msama awe mfano mwema katika kuisaidia jamii ili kutimiza lengo la Kristo aliyesema, “Wenye afya hawahitaji tabibu ila walio hawawezi,”” alisema.
Hata hivyo mchungaji Dunia amesema kuwa wapo wanaotumia fedha nyingi kwa kuandaa sherehe katika sikukuu ya Pasaka huku wengine wakihangaika kutafuta angalau mlo mmoja wa siku, hata katika kipindi cha sikukuu kama hiyo, lakini wakumbuke kuwa ni vyema kwenda kuwatia moyo kuwafariji wale wanaolea wenye uhitaji maalum vituoni.
Aliongeza kwa kumtia moyo Msama aendelee na moyo huo wa imani wa kuwasaidia wasiojiweza kwa kuwa anayetoa atazidishiwa mara dufu, kwa kuwa yeye yu miongoni mwa wachache wenye moyo wa kusaidia wahitaji hao.
Anatoa wito kwa mashabiki na waumini wajitokeze kwa wingi kuhudhuria matamasha hayo kwa kuwa kupitia nyimbo za injili watabarikiwa na hata kujifunza neno la Mungu. Pia aliwapongeza waimbaji wa nyimbo za injili kwa kuwa wao wamekuwa ni njia nyingine ya kutangaza neno la Mungu na kupitia wao watu wengi wanaokolewa. Hivyo wajue kuwa wao pia ni kioo cha jamii, jamii inahitaji kujifunza kutoka kwao
.
Matamasha hayo ambayo hufanyika kila mwaka katika mikoa tofauti yamekuwa ni moja ya njia pekee ya kupunguza uhalifu na kuongeza kipato cha wafanyabiashara wanaofanya biashara maeneo ya karibu na yanapofanyika matamasha hayo.Hata hivyo Msama ana nia ya kujenga kituo cha kusaidia wahitaji hao ambacho kitasaidia maeneo mbalimbali kama kuwasaidia wahitaji wenye kipaji cha uimbaji.
Pamoja na hayo Msama anaiomba jamii, ikae tayari kusubiri matamasha hayo yanayosubiriwa kwa hamu katika mikoa mbalimbali ya Tanzania na mashabiki wa nyimbo za injili kujitokeza kwa wingi kwa kipindi hicho cha matamasha ili kuweza kumsapoti kutimiza lengo lake la kusaidia wahitaji hao.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...