Kituo cha Uwekezaji Nchini (TIC) na Kampuni ya Tanga Fresh Ltd pamoja na wajasiriamali wapatao 60 kutoka katika vituo mbalimbali vya kupoozeshea maziwa katika mkoa wa Tanga wametiliana saini mkataba wa ushirikiano kwa ajili ya kuwajengea uwezo wajasiriamali hao ili waweze kukua kibiashara.
Utiaji saini huo umefanywa na Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Bi. Juliet Kairuki; Meneja Mkuu wa Tanga Fresh Ltd, Bw. Michael Karata na mwakilishi wa wajasiriamali hao, Bi. Asnat Mbwambo.
Tukio hilo lililofanyika mwishoni mwa wiki mjini Tanga lilishuhudiwa na Mkuu wa mkoa huo, Bi. Chiku Gallawa.
Akizungumza wakati wa makubaliano hayo, Bi. Kairuki alisema pamoja na shughuli mama za kituo cha uwekezaji za kutangaza fursa za uwekezaji ndani na nje ya nchi, serikali inatambua umuhimu wa kuwajengea uwezo wajasiriamali wadogo.
“TIC kama moja ya taasisi za serikali tunatambua uwepo wa wajasiriamali wadogo na umuhimu wao kwa uchumi , tunatambua kuwa wanahitaji kukua kibiashara, hivyo kwa kufanya hivi tunatimiza azma ya serikali katika kuwainua watu wetu,” alisema mkurugenzi huyo.
Aliisifu kampuni ya Tanga Fresh Ltd kwa kukubali kugharamia asilimia 50 katika kuendesha mafunzo ya program hiyo pamoja na huduma nyingine katika kipindi chote kuanzia Machi 2014 hadi Machi 2015.
“Napenda kuchukua fursa hii kutoa wito kwa makampuni mengine kuiga mfano wa Tanga Fresh Ltd na kuwa na moyo wa kujitolea katika kusaidia wajasiriamali kupata elimu ambayo itasadia kuwajengea uwezo,” alisema.
Alisisitiza kuwa kituo hicho kitaendelea kushirikiana na serikali ya mkoa wa Tanga na wadau wengine katika kuhakikisha kuwa shughuli za uwekezaji zinaendelea kukua katika mkoa huo.
“Mkoa wa Tanga una fursa nyingi, hivyo ni jukumu letu kushirikiana na taasisi nyingine pamoja na serikali ya mkoa katika kukuza uwekezaji,” alisema.
Kwa upande wake, Bi. Gallawa, alisema TIC pamoja na kampuni ya Tanga Fresh wamefungua milango kwa wajasiriamali wa mkoa wake, hivyo ni jukumu la wafanyabiashara hao kuzingatia kwa umakini kile watakachofundishwa.
“Tanga Fresh na TIC wamejitoa sana, nawaomba muwe makini katika kufuatilia na kuweka katika matendo kile mtakachofundishwa,” alisema.
Aliongeza kuwa mkoa wake umefarijika sana na utiaji saini wa makubaliano hayo kwani ni njia mojawapo ya kuona wajasiriamali wanaanza safari ya kuelekea katika mafanikio ya kweli.
“Sasa njia inaanza kuonekana, si kwenu ninyi tu wajasiriamali bali hata sisi viangozi wenu, hii inatupa moyo kuwa yapo makampuni binafsi na taasisi za umma ambazo zipo mstari wa mbele kusaidia watu wa chini katika biashara,” aliongeza.
Awali, Bw. Karata alisema kampuni yake itaendelea kutoa ushirikiano pale serikali itakapokuwa tayari, hasa katika kusaidia watu walio katika sekta za kilimo na ufugaji.
“Sisi tumekuwa tunafanya kazi moja kwa moja na wafugaji pamoja na wakulima wanaotuzunguka, hivyo ni jukumu letu kuwaangalia na kuwainua kiuchumi ili waweze kuboresha maisha yao,” alisema Bw. Karata.
Aliongeza kuwa pamoja na kununua maziwa kutoka kwa wafugaji hao wadogo bado wamekuwa wakitoa elimu hasa ya ufugaji pamoja na kilimo ili waweze kufuga kisasa zaidi.
Mbali na ofisi ya mkuu wa mkoa kushuhudia zoezi hilo la utiaji saini makubaliano hayo, wadau wengine waliofika katika sherehe hizo ni benki za NMB, CRDB, na EXIM pamoja na TCCIA.
Mkuu wa Mkoa wa
Tanga, Bi. Chiku Gallawa (katikati)
akikata utepe kuashiria kuzinduliwa rasmi kwa programu ya mwaka mmoja
ya kutoa elimu ya biashara kwa
wajasiriamali wadogo wapatao 60 kutoka katika vituo mbalimbali vya kupoozeshea maziwa
katika mkoa huo mwishoni mwa wiki mjini Tanga.
Programu hiyo itaendeshwa na Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC) kwa
kushirikiana na kampuni ya Tanga Fresh Ltd.
Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Bi. Juliet Kairuki na Meneja Mkuu
wa kampuni ya Tanga Fresh, Bw. Michael Karata (kulia).
Mkuu wa Mkoa wa
Tanga, Bi. Chiku Gallawa ( katikati )
akionyesha mikataba kwa waandishi wa habari mara baada ya Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC) na Kampuni
ya Tanga Fresh ltd pamoja na wajasiriamali wapatao 60 kutoka katika vituo mbalimbali
vya kupoozeshea maziwa katika mkoa wa Tanga kutiliana saini mkataba wa
kuwajengea uwezo kibiashara wajasiriamali hao mwishoni mwa wiki mjini Tanga.
Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa TIC Bi. Juliet Kairuki na kulia ni Meneja
Mkuu wa Tanga Fresh Bw. Michael Karata.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC) Bi. Juliet Kairuki akitia saini
mkataba wa ushirikiano wa pamoja na Kampuni ya Tanga Fresh Ltd pamoja na
wajasiriamali wapatao 60 kutoka katika vituo mbalimbali vya kupoozeshea maziwa katika mkoa wa Tanga mwishoni mwa wiki
iliyopita ili kuwajengea uwezo wajasiriamali hao. Wa pili kulia ni Meneja Mkuu wa Tanga Fresh Ltd, Bw. Michael
Karata, mwakilishi wa wajasiriamali hao, Bi. Asnat Mbwambo (kushoto) na Mkuu wa
Mkoa wa Tanga, Bi. Chiku Gallawa (kulia).
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...