WATU 19 wakiwemo askari Polisi wanne wamepota maisha katika ajali ya barabarani, wakati basi linalomilikiwa na Kampuni ya Sumry, lilipopamia watu hao wakati wakimsitiri mtembea kwa miguu, aliyekufa kwa kugongwa na gari lisilofahamika. Ajali hiyo ilitokea usiku wa kuamkia jana katika Kijiji cha Utaho, kilometa 20 nje ya Mji wa Singida katika Barabara Kuu ya Singida Dodoma. 



Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Singida, Kamishina Msaidizi Mwandamizi, Geofrey Kamwela, alisema jana kuwa mbali na askari hao, wengine waliokufa papo hapo ni viongozi watatu wa kijiji hicho na wananchi wanaowaongoza na wengine wanne ambao hawajatambulika. 
Kwa mujibu wa Kamanda Kamwela, askari waliokufa katika ajali hiyo ni Koplo Boniface Magubika, PC Jumanne Mwakihaba, PC Novatus Tarimo na PC Michael Mwakihaba na wote wanatoka katika kituo kimoja cha kazi. 
Viongozi wa Kitongoji na Kijiji cha Utaho waliokufa ni Ramadhan Mjengi, ambaye ni Ofisa Mtendaji wa Kijiji, Paul Hamis, ambaye ni Mwenyekiti wa Kijiji na Ernest Salanga ambaye ni Mwenyekiti Kitongoji. 


Wananchi wanaowaongoza katika kijiji hicho waliokufa ni Saidi Rajabu, Ushirika Itambu, Chima Mughenyi, Salim Juma, Abeid Ramadhan, Mwinyi Hamis na Issaha Hussein. 
Kwa mujibu wa Kamanda Kamwela, miili ya watu wengine wanne haikuwa rahisi kutambulika mara moja na wote wamehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa mjini Singida. 

Kamanda Kamwela alisema ajali hiyo ilisababishwa na basi la abiria lenye usajili namba T.799 BET aina ya Nissan, mali ya Kampuni hiyo ya Sumry, inayomilikiwa na Mohamed Abdallah wa Sumbawanga, lililokuwa likienda jijini Dar es Salaam likitokea Kigoma. 

Alisema kuwa basi hilo lililokuwa likiendeshwa na Paul Njilo, mkazi wa Dar es Salaam, liliwagonga waenda kwa miguu hao waliokuwa wamekusanyika kando ya barabara wakisaidiana na askari Polisi kuondoa mwili wa marehemu Gerald Zephania, aliyekuwa amegongwa na lori lisilofahamika juzi saa moja usiku. 

Katika ajali hiyo kwa mujibu wa Kamanda Kamwela, watu wengine wanane walijeruhiwa na wamelazwa katika Hospitali ya Misheni Puma ya mjini Singida. 

Habari kutoka eneo la tukio zinasema kilichosababisha ajali hiyo huenda ni kuegeshwa vibaya kwa gari la Polisi, wakati likipakia mwili wa marehemu Gerald, aliyekuwa amegongwa na lori mapema kabla ya basi hilo kufika hapo. 

Akizungumzia ajali hiyo katika Makao Makuu ya Polisi Dar es Salaam jana, Kamishna Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonja, alitoa pole kwa wananchi wote waliofiwa na ndugu zao na kuwaombea majeruhi kupona haraka. 

Alisema Askari wa Usalama Barabarani hawatakuwa na muhali na dereva yeyote atakayekwenda kinyume na Sheria ya Usalama Barabarani. Kutokana na hilo, ametoa mwito kwa madereva kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za usalama barabarni, ili kuepusha ajali zinazoweza kuzuilika. 

“Polisi iko imara kuchukua hatua zozote za kisheria, kwani kuna baadhi ya watoa huduma wa usafiri hugoma pale wanapotaka kuchukuliwa hatua kwa sababu mbalimbali matokeo yake ni uvunjaji wa sheria kwa makusudi,” alisema. 

Alisema Jeshi la Polisi limeanzisha msako mkali wa dereva wa basi hilo ambaye alitoroka ili kufikishwa mahakamani, na kuwaomba wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa za wahalifu wa aina yeyote ile, ili wakamatwe na kufikishwa mahakamani. 

Chanzo:HabariLeo

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 2 mpaka sasa

  1. Kuna haja ya serikali kuweka sheria ya kuwalazimu madereva wote wa magari ya abiria pamoja na askari wanaoendesha magari ya polisi kupitia kozi maalum ya usalama barabarani isiyopungua miezi 3 na kuhakikisha kuwa wanarudi barabarani tu endapo kama watahitimu na kufaulu hiyo kozi. Kama kuna siri kubwa ya wenzetu nchi zilizoendelea inawasaidia katika kupunguza ajali, ni kozi ya theory ya uendeshaji magari barabarani ambayo ukiijua hii na kuisoma vizuri na kufaulu kwa kiwango cha 35/40 (ufaulu maswali 35 kati ya 40 yaliyoulizwa), ndio tu utaruhusiwa kuendesha gari. Hii inahusisha kutumia muda wa angalau masaa 3 au 4 kwa wiki kufanya revision kwa kuenda driving school na kusoma na kujibu maswali 40 kila session, inahusisha kutambua michoro ya alama mbali mbali barabarani na picha mbali mbali zinazohusu scenario za kila aina barabarani, zinzzohusihsha wapita njia, magari, taa za barabarani, ku-overtake, speeding or slowing down na dangers za kila aina na ukiwa na sekunde 30 tu, za kuamua ufanye nini katika hali kama hiyo, na kujibu kwa kila swali unaloulizwa. Sielewi kwa nini hiyo ajali itokee kama paliwekwa alama za kutosha barabarani kumuarifu dereva wa basi kuwa kuna danger mbele yake na apunguze mwendo. Na kama zilikuwekpo ina maana huyo dereva hajui wala haelewi hizo sheria za barabarani ama umuhimu wake. Watu wataendelea kufa namna hii hadi lini jamani? Serikali inafanya nini kuhusu kupunguza ajali hizi mbaya zisizokuwa na kichwa wala miguu?? So saddened by this situation ambayo inatufanya wengine tufikirie kweli kabla ya kuingia safari ndefu. Tumejaliwa barabara nzuri sasa Tanzania lakini sisi wenyewe tunazi-abuse. Basi bora kuwa na mbarabara za mashimo mradi tuwe salama.

    ReplyDelete
  2. Asante sana kwa mtoa maoni hapo juu. Muda umefika tamko litolewe rasmi na utawala wa juu kuwa ajali za barabarani ni janga la kitaifa. Mada zianizishwe kuhusu suala hili. Pia jopo la wanasheria litafute sheria kali dhidi ya madereva wazembe ambao tunaweza kuwaita wauwaji. Maana hata madaktari kama ugonjwa ukiwa sugu, huketi pamoja na kutafuta suluhu. Ajali za barabarani ni TATIZO SUGU. Watanzania tunateketea na ajali hizi. Wanaoteketea ni WATU na si WANYAMA. Kwa nini serikali imekaa kimya? hata bungeni hili suala sijawahi kusikia likijadiliwa. it is indeed very sad

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...