Wamiliki wa mabasi ya usafiri wa abiria jijini Dar es Salaam na wadau wengine muhimu wanatarajia kukutana kwenye Ukumbi wa Karimjee jumamosi asubuhi kujifunza fursa na kufahamu jinsi wanavyoweza kuwa washiriki katika mradi wa mabasi yaendayo haraka (BRT) unaotarajiwa kuanza baadaye mwaka huu.

Waratibu wa mkutano huo, wakala wa mabasi yaendayo haraka, DART Agency, watatumia pia mkutano huo kuelezea mkutano mwingine wa kimataifa unaotarajiwa kufanyika tarehe 3-4 mwezi ujao kujadili kuhusu kuanza kwa awamu ya kwanza ya mradi huo jijini Dar es Salaam.

Mtendaji Mkuu wa wakala wa DART, Bi. Asteria Mlambo amewaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Said Meck Sadiki atakuwa mgeni rasmi katika mkutano huo muhimu.

“ Mkutano huo wa kesho unalenga kuwaelezea wamiliki wa mabasi ya abiria maarufu kama daladala na wale wa UDA fursa za mradi wa mabasi yaendayo haraka na jinsi wanavyoweza kuwa wadau,” alisema na kuongeza kuwa wadau wataelezea faida na fursa za mradi huo mpya na jinsi wanavyoweza kuwa wadau,” alisema.Mkutano huu pia unalenga kupata maoni ya wadau hao wa usafiri na kuyatumia kama mchango katika mkutano wa kimataifa wa mwezi wa Sita.

“Mkutano wa mwezi huu ni nafasi muhimu kwa wamiliki wa mabasi hayo ya abiria, wahudhurie kwa wingi na kushiriki kikamilifu,” alisema.Mwezi uliopita, wakala wa DART ulikamilisha zoezi la kusajili mabasi ya daladala yanayopita katika barabara ya Morogoro au kukatiza katika njia hiyo.

Hatua hiyo ya kuandikisha mabasi hayo ilikuwa moja ya matayarisho ya kupisha mradi huo wa mabasi yaendayo haraka.

Kwa sasa wakala huo uko kwenye mchakato wa kuwezesha upatikanaji wa watoa huduma kwenye mfumo mpya wa mabasi yaendayo haraka awamu ya kwanza ambayo inajumuisha barabara ya Morogoro, Kawawa na mtaa wa Msimbazi kwa njia kuu na nyingine za kiungo. 

Kulingana na mpango wa uendeshaji wa mfumo wa DART, barabara zinazohusika zitapaswa kutumiwa na mabasi ya mfumo huo pekee.Jumla ya njia 64 jijini Dar es Salaam zitakoma kutumika kutokana na kuanza kwa mradi huo.

Mradi wa mabasi yaendayo haraka unalenga kutatua tatizo sugu la foleni na msongamano wa magari katika jiji hilo kubwa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...