Na Frank Mvungi- Maelezo 
Serikali inatarajia kuanza kutoa huduma za awali (interim services) katika mradi wa Mabasi yaendayo Haraka (DART) Kutoka Kimara mwisho hadi Kivukoni jijini Dar es salaam mwaka 2015 baada ya miundombinu yake kukamilika. 
 Hayo yamesemwa na Meneja Uhusiano wa Wakala wa mabasi yaendayo haraka (DART) Bw.William Gatambi wakati wa mkutano na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam. 
Bw. Gatambi alisema kuwa mara baada ya kukamilika kwa miundo mbinu ya mradi huo awamu ya kwanza mwishoni mwa mwaka 2014 itasadia kufanikisha usafiri wenye tija kwa wakazi wa jiji la Dar es salaam na vitongoji vyake. 
Miundombinu hiyo, inajumuisha barabara ya kilomita 20.9 kuanzia Kimara Mwisho hadi Kivukoni,Barabara ya Kawawa kutoka Morocco hadi Magomeni na Barabara ya Msimbazi hadi eneo la Gerezani Kariakoo.
 Aliongeza kuwa ina vituo vidogo 27,vituo vikuu vitano, vituo mlisho vine na karakana mbili. 
Pia inajumuisha njia za waenda kwa miguu na baiskeli. Akifafanua Gatambi alisema mradi wa majaribio utaanza na mabasi 20 yatakayokuwa na uwezo wa kuchukua abiria kati ya 145 hadi 160 kwa wakati mmoja hali itakayosaidia kuondoa kabisa kadhia ya usafiri kwa wakazi wa jiji la Dar es salaam. 
Aidha, katika mradi huo wa majaribio Gatambi amesema kutakuwa na mabasi mengine 10 yenye uwezo wa kuchukua abiria kati ya 50 na 60 ambayo yatatumika kuchukua abiria kutoka pembezoni mwa jiji la Dar es salaam kuja katika vituo vikuu vya mabasi yaendayo Haraka. 
Kwa upande wake Meneja Usimamizi wa Barabara wa DART Mhandisi Mohamed Kuganda amesema mradi huo utasaidia kuondoa tatizo la foleni Jijini Dar es salaam na kuwafanya wananchi kupata huduma ya usafiri yenye kukidhi viwango vya Kimataifa. 
Pia Kuganda alisema DART kwa kushirikiana na Halmashauri za Jiji la Dar es salaam inafanya maandalizi ya kuboresha barabara mlisho (feeder roads) katika maeneo yatakayotumiwa na mabasi mlisho. Katika mradi wa mabasi yaendayo haraka kutakuwa na Vituo Vikuu (terminals) vitano 5 katika, maeneo ya Kimara, Ubungo, Morocco, Kariakoo na Kivukoni ambapo vituo hivi ndiko mabasi yatakapokuwa yanaanzia na kumalizia safari kubadilishana abiria kati ya njia kuu na njia mlisho (feeder roads) ambapo vituo hivyo vikubwa vinatoa nafasi ya kuweza kuanzishwa kwa huduma muhimu kwenye vituo hivyo kama maeneo ya kukatia tiketi na vyoo. Mwisho

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...