Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Dkt. Servacius Likwelile (kulia) akisaini
mkataba wa msaada wa sh. Bilioni 134 kwa niaba ya Serikali ya Tanzania leo jijini
Dar es salaam. Kushoto ni Balozi EU nchini Filberto Sebregond.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Dkt. Servacius Likwelile (kulia)
akibadilishana hati ya mkataba wa msaada wa sh. Bilioni 134 waliosaini kwa niaba
ya Serikali ya Tanzania leo jijini Dar es salaam. Kushoto ni Balozi EU nchini
Filberto Sebregond.
(Picha na Wizara ya Fedha)
Na Eleuteri Mangi-MAELEZO
SERIKALI ya Tanzania imetiliana saini mkataba wa msaada wa zaidi ya Shilingi
Bilioni 134 sawa na Euro milioni 59.5 kutoka Umoja wa Ulaya (EU) kusaidia
sekta ya kilimo na usafirishaji nchini.
Mkataba huo ulisainiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Dkt. Servacius
Likwelile kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Balozi wa EU nchini Filberto
Sebregond leo jijini Dar es salaam.
Akizungumza baada ya kutia saini mkataba huo, Dkt. Likwelile alisema kuwa
sehemu ya msaada huo ambao ni Shilingi Bilioni 82.4 ambazo ni sawa na Euro
milioni 36.5 utatumika kuendeleza sekta ya kilimo na kukuza uchumi nchini
kwa kupitia kituo maalum cha uendelezaji kilimo ukanda wa Kusini Tanzania
(SAGCOT) na kuboresha miundombinu ya barabara za ukanda huo.
Vilevile Dkt. Likwelile alisema kuwa sehemu iliyobaki ya msaada huo ambao ni
Shilingi Bilioni 51.9 ambazo ni sawa na Euro milioni 23 itatumika kuimarisha
biashara na ushirikiano katika jumuiya kwa kuanzisha kituo cha pamoja cha
ukaguzi mipakani (OSIS).
“Vituo hivyo vya ukaguzi mipakani vitakuwa na manufaa si kwa Tanzania tu, bali
hata katika nchi mbalimbali zinazopakana na Tanzania” alisema Dkt. Lkwelile.
Alifafanua kuwa msaada uliosainiwa unamanufaa kwa wananchi kwa kuboresha
miundombinu vijijini na kusambaza umeme vitu ambavyo vitasaidia kukuza
uchumi na kupunguza umaskini nchini.
Naye Balozi wa EU nchini Filberto Sebregond alisema kuwa anaamini msaada huo
utasaidia juhudi za Serikali ya Tanzania katika kuongeza nafasi za ajira, kupungua
kwa bei za bidhaa mbalimbali na kuendelea kukuza uchumi nchini.
Balozi huyo alisema kuwa EU inaamini kuwa ushirikiano wake na Tanzania
utaendelea kuimarika kwa kuhimiza maendeleo kwa pande zote mbili na amani ya
watu wake.
Hafla hiyo ya kusaini mkataba ilihudhuriwa na wawakilishi kutoka Wizara ya
Fedha, Nishati na Madini, Uchukuzi na Ujenzi, EAC, DFID, SAGCOT, wajumbe
kutoka EU, Shirika la maendeleo ya Ufundi kutoka Ubelgiji na washirika wa
maendeleo.
Zungu anadesa!
ReplyDelete