WAZIRI MKUU Mizengo Pinda ameutaka uongozi wa mkoa wa Rukwa uhakikishe unamaliza tatizo la upungufu wa madawati ili watoto wa shule za msingi wasiendelee kukaa chini.
Ametoa agizo hilo jana usiku (Jumamosi, Mei 24, 2014) wakati akizungumza na viongozi na watendaji wa mkoa wa Rukwa mara baada ya kupokea taarifa ya Mkoa huo, Ikulu ndogo, mjini Sumbawanga.
Waziri Mkuu amewasili mkoani Rukwa jana jioni akitokea Dodoma ambapo atamwakilisha Rais Jakaya Kikwete kwenye ibada ya kumuweka wakfu Askofu Mteule Conrad Nguvumali wa Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Rukwa itakayofanyika leo (Jumapili, Mei 25, 2014) kwenye Uwanja wa Nelson Mandela, mjini Sumbawanga.
Akifafanua kuhusu tatizo la madawati, Waziri Mkuu alisema: “Lazima mjipange kama mkoa ili muweze kusaidia juhudi za Serikali kupunguza tatizo la madawati kwa watoto wetu wa shule za msingi”.
“Lazima mje na mpango maalum… mathalani kwenye Halmashauri zenu huko, angalieni hizo mbao zinazokamatwa. Badala ya kuziuza, hizo mbao ziende kutengeneza madawati na yakikamilika yaamuliwe kabisa haya yanakwenda shule fulani, na utaratibu uendelee hadi shule zimalizike,” aliongeza.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...