Na Mwandishi Wetu,
Malabo
MPANGO wa Afrika
Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM) umempata Mtendaji wake Mkuu mpya
atakayeongoza ofisi ya taasisi hiyo katika ngazi ya Bara la Afrika iliyoko
mjini Midrand, Afrika Kusini.
Uamuzi huo umefikiwa katika
Mkutano wa 21 wa Wakuu wa Nchi za APRM uliofanyika mjini hapa, ambapo aliyekuwa
Mtendaji Mkuu wa Mpango wa NEPAD, Dkt. Ibrahim Assane Mayaki kutoka Niger ndiye
amehamishiwa APRM.
Mabadiliko hayo
yamekuja wakati ambapo wakuu wa Nchi za APRM waliokutana mjini hapa wakiwa
wamesisitiza umuhimu wa mageuzi na APRM kutekeleza majukumu yake kwa wakati
katika kufanya tathmini za utawala bora Barani Afrika.
Dkt. Mayaki ambaye
kabla ya uteuzi huo alipata kuisimamia APRM ilipokuwa taasisi moja na Nepad
anaingia katika APRM akichukua nafasi ya Bw. Assefa Shifa raia wa Ethiopia.
Akizungumza mjini hapa,
Katibu Mtendaji wa APRM Tanzania, Bi. Rehema Twalib anayehudhuria mikutano
hiyo, alithibitisha kufanyika kwa uteuzi huo. Tanzania ni miongoni mwa nchi 35
za Umoja wa Afrika zilizokwishajiunga na APRM.
Kitaaluma Dkt. Mayaki anashahada
ya umahiri Kutoka Chuo Kikuu kiitwacho National School of Public Administration
(Enap), Quebec, Canada na pia ana shahada ya uzamivu (PhD) katika sayansi za
utawala kutoka Chuo Kikuu cha Paris I.
Kati ya mwaka 1996 na
2000 alitumikia nafasi mbalimbali katika Baraza la Mawaziri nchini mwake kabla
ya kuhamia katika masuala ya utafiti na uhadhili.
Akizungumza katika
ufunguzi wa mkutano huo uliofanyika juzi, Rais wa Liberia Mama Ellen
Johnson-Sirleaf ambaye ndiye Mwenyekiti wa APRM katika ngazi ya Afrika,
aliziasa nchi wananchama kutekeleza Mpango huo kwa umakini na kutaka mageuzi
makubwa.
Katika mkutano huo pia
wakuu wa nchi walipitisha wazo la kuwa na semina mbalimbali za uhamasishaji
ambapo Tanzania iliteiuliwa kuwa mwenyeji wa semina itakayohusisha nchi za
Afrika Mashariki.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...