Wananchi wanaoishi kando ya maeneo ya ardhioevu na sehemu ambazo mito inakutana na bahari wamehimizwa kuzingatia matumizi bora ya maeneo hayo ili yasiweze kuleta madhara ya mali, uhai wao na uharibifu wa viumbe hai vilivyopo katika sehemu hizo. 
Naibu Waziri, Wizara ya Maliasili na Utalii, Bw. Mahmoud Mgimwa, alisema hayo wakati akifunga mkutano wa wanasayansi toka Afrika na nje ya bara hilo mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam. Kongamano hilo lililojulikana kama Afrideltas liliangalia na kuchambua mabadiliko yanayotokea sasa katika maeneo ya ardhi oevu na makutano ya mito na bahari. 
Waziri Mgimwa alisema serikali imeyachukua mapendekezo ya wanasayansi hao kwa kuwa yanalenga kulinda maeneo hayo yaweze kutumika kwa kwa faida ya sasa na vizazi vijavyo. 
Pia alisema kuwa serikali itahakikisha sera, sheria na kanuni mbalimbali zinafuata maelekezo ya kitalaamu kama yaliyotolewa katika kongamano hilo kwa vile maeneo hayo yanafaida kubwa za kiuchumi. 
“Katika kuhakikisha jambo hili linafanikiwa, wadau wote wanatakiwa kushiriki katika kutoa elimu ya mazingira kwa wakazi wa maeneo hayo,”alisema. 
Alisema Tanzania ina changamoto ya kulinda aina mbalimbali za viumbe katika maeneo ya ardhioevu ambavyo vipo katika hatari ya kutoweka kutokana na shughuli za kibinadamu. 
Naye, mjumbe wa kamati ya maandalizi ya Kongamano hilo, Prof. Amos Majule ambaye pia ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Uthamini Raslimali (IRA) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) alisema kongamano hilo lilikuwa na faida kubwa kwa washiriki hao wa kimataifa.
“Kila mmoja alijifunza toka kwa mwenzake na kubadilishana uzoefu na kutoa mapendekezo tuliyoona yanafaa,” alisema. 
Alisema moja ya mapendekezo hayo ni kuona elimu mbadala inatolewa zaidi kwa jamii jinsi ya kutumia na kulinda rasilimali zilizopo katika maeneo ya ardhioevu na maeneo mito inapokutana na bahari. Pia alisema watunga sera na watoa maamuzi wameshauriwa kutoa elimu zaidi kwa wananchi ili rasilimali zinazopatikana katika maeneo hayo ziweze kutumika kwa faida ya sasa na vizazi vijavyo. 
Alisema changamoto iliyojitokeza ni kwamba kuna njia zisizo endelevu za matumizi ya madawa ya mbolea katika Kilimo, ukataji misitu na ujenzi wa makazi katika maeneo hayo na kuleta athari za kimazingira. Aliongeza kusema kuwa kutokana na mabadiliko ya tabia nchi, maeneo hayo pia yanakumbwa na mafuriko na kuathiri mazao ya Kilimo, uvuvi na makazi yao jambo ambalo ni hatari kwa uhai wao. 
Naye Mradibu wa Kenya Wetlands Biodiversity, Dk. Wanja Njingi alisema kutokana na tafiti zilizowasilishwa katika mkutano huo, nchi za Africa zimefaidika na mawazo na taarifa mpya ya jinsi ya kushughulikia na kulinda maeneo ya ardhioevu.
 “Kupitia tafiti hizi sasa tunaweza kurekebisha mambo yaliyoharibika katika nchi zetu,” aliongeza kusema. 
Kongamano hilo lilijumuisha wanasayansi kutoka nchi mbalimbali zikiwemo Kenya, Afrika Kusini, Ethiopia, Sudan, Senegal, Nigeria, Uholanzi, Ufaransa, Ubelgiji na mwenyeji Tanzania. Pia wanasayansi hao walitembelea Bonde la Mto Rufiji kujionea hali ya bonde hilo na shughuli zinazoendelea.
 Naibu Waziri, Maliasili na Utalii, Bw. Mahmoud Mgimwa (katikati)akiongea wakati wa kufunga kongamano la kimataiafa la wanasayansi lililofanyika jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.  Wengine katika picha ni, Mkurugenzi wa Taasisi ya Uthamini Raslimali (IRA) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Prof. Amos Majule (kulia) na Kaimu Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa wizara hiyo, Dkt. Iddi Mfunda.
Naibu Waziri, Maliasili na Utalii, Bw. Mahmoud Mgimwa (katikati) akifurahia jambo wakati wa kufunga kongamano la kimataifa la wanasayansi lililofanyika jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.  Wengine katika picha ni, Mkurugenzi wa Taasisi ya Uthamini Raslimali (IRA) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Prof. Amos Majule (wa pili kulia), Kaimu Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa wizara hiyo, Dkt. Iddi Mfunda (kushoto) na Dk. Catherina Masao wa IRA (kulia) .

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...