Na Mwene Said wa Blog ya Jamii

MKURUGENZI wa Shirika la Viwango Nchini (TBS), Charles Ekerege, amekiri mahakamani kwamba Menejimenti ilikosea kutoa msamaha wa kodi kwa Kampuni ya Jaffar Mohamed Ali Garage na Kampuni Quality Motors na hivyo, na kwamba Bodi ya Wakurugenzi ilitoa onyo kali na kuitaka isirudie kosa hilo.

Aidha, ameeleza kuwa hakutoa msamaha huo yeye binafsi bali menejimenti iliyoketi chini ya wakuu wa idara sita za shirika hilo ilipitisha na kwamba kutokana na kampuni hizo mbili kukosa uaminifu waliisababishia TBS, hasara ya Dola 42,543 za Kimarekani.

Kadhalika alidai kuwa katika upelelezi wake alibaini kwamba hakukuwa na kikao chochote cha menejimenti kilichojadili na kupitisha msamaha wa kodi kwa kampuni hizo mbili.

Ekerege ametoa madai hayo leo katika ushahidi wake wa utetezi mbele ya Hakimu Mkazi Augustina Mmbando anayesikiliza kesi hiyo.

Akiongozwa na wakili wa utetezi Majura Magafu, shahidi huyo wa kwanza wa utetezi alidai kuwa siyo kweli kwamba alitoa msamaha wa kodi kwa kampuni hizo bali menejimenti ilihusika kwa asilimia 100.

Alidai kuwa menejimenti ilitoa msamaha huo bila kujua kwamba kampuni hizo hazikuwa na uaminifu na hivyo kufanyakazi kinyume cha sheria ya shirika hilo.

“Menejimenti ya shirika ilikuwa na utaratibu wa kukaa vikao vya asubuhi na kwamba walijadili mambo mbalimbali pamoja na kuhusu kutoa msamaha kwa kampuni hizo na tulikubaliana tukapitisha msamaha huo,” alidai na kuongeza kwamba.

“Baada ya kutoa msamaha huo menejimenti ilibaini kwamba imefanya makosa tukaamua tuitishe kikao cha Bodi ya Wakurugenzi ili kujadili misamaha ya kampuni hizo… bodi iliridhia misamaha hiyo bada ya kubaini kwamba haikutolewa kwa makusudi  na haikuwahi kutokea, lakini ilitoa onyo kali kwa menejimenti” alisema Mkurugenzi huyo ambaye alisimamishwa kazi kupisha upelelezi tangu Mei 21, mwaka 2012.

Katika kesi ya msingi, Ekelege anadaiwa kuwa kufanya matumizi mabaya ya madaraka kwa kutoa asilimia 50 ya punguzo la tozo ya utawala kwa kampuni hizo mbili.

Pia, ilidaiwa kuwa Machi 28, mwaka 2008 na Agosti 7, mwaka 2009, katika ofisi za TBS zilizopo wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam, kwa nia ovu Ekerege alitumia madaraka yake vibaya.

Ilidaiwa kuwa mshtakiwa huyo alitumia madaraka yake vibaya kwa kutoa punguzo la asilimia 50 ya ada ya utawala kwa kampuni hizo bila idhini ya baraza la utendaji la TBS kinyume cha sheria namba 2 kifungu kidogo cha (3) ya TBS ya mwaka 2005.

Ilidaiwa kuwa kitendo hicho kiliziongezea kampuni hizo faida ya Dola 42,543 za Kimarekani sawa na (kwa wakati huo) Sh. Milioni 68,068,800.

Ilidaiwa kuwa, shitaka la pili, katika tarehe na mahali pa tukio la kwanza, mshtakiwa alilisababishia shirika kupata hasara ya fedha hizo.

Mshtakiwa alikana mashitaka yote mawili na yuko nje kwa dhamana.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...