Waziri katika Ofisi ya Rais Kazi Maalum, Mheshimiwa Prof. Mark Mwandosya alifanya ziara ya kutembelea Mamlaka za Udhibiti wa huduma za umma na shughuli zingine za kiuchumi kwa nia ya kufahamu utendaji, mafanikio na changamoto zinazowakabili katika kutekeleza majukumu waliyokabidhiwa na Serikali kuyafanya. Ziara hiyo ambayo ilianza tarehe 21 hadi 23 Julai, 2014 ilihusisha Mamlaka za udhibiti za SUMATRA, EWURA, TCAA, TCRA, TIRA na SSRA.

Katika ziara yake hiyo Waziri Prof. Mwandosya alieleza kuwa madhumuni ya ziara yake ilikuwa ni kujifunza na kubalishana uzoefu katika shughuli za udhibiti hapa Tanzania. Waziri Prof. Mwandosya alieleza kuwa shughuli za udhibiti Tanzania zilianza rasmi kwa kuanzisha Mamlaka za Udhibiti kwa kujibu wa sheria zilizopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania takriban miaka 10 iliyopita.

Waziri Prof. Mwandosya alieleza kuwa pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika kutekeleza majukumu yao, Mamlaka za Udhibiti hapa nchini bado zina changamoto nyingi ambazo inabidi kukabiliana nazo kwa kujifunza na kubadilisha uzoefu. Kipindi cha miaka 10 kinatosha kuweza kutathimini tulikotoka, tulipo na tunakoelekea. Hii ni pamoja na kuweka malengo ya kukabiliana na changamoto za kuwa na uchumi mzuri kwa miaka kumi ijayo.

Waziri Prof. Mwandosya aliendelea kueleza kuwa Mamlaka za Udhibiti zinapaswa kujiuliza kuwa zimefanya nini katika kutekeleza majukumu waliyokabidhiwa na Serikali, nini kimesababisha wao kushindwa kutekeleza baadhi maeneo yao ya udhibiti na kwa kiwango gani mahusiano yao na Serikali yamesaidia au kuathiri utendaji wa mamlaka hizo. Na mwisho ili kupata suluhu mamlaka zinashauri nini kifanyike ili mahusiano yao na Serikali yaweze kuboresha utendaji wao.

Aidha Waziri Prof. Mwandosya alitoa ujumbe kwa watendaji wa Mamlaka za Udhibiti kuwa pamoja na kwamba vyombo vya udhibiti vilianzishwa kwa ajili ya kusimamia huduma za umma (utilities) lakini kimsingi vyombo hivyo vilianzishwa kwa lengo kuu la kuchangia katika maendeleo ya kiuchumi katika nchi. 

Waziri Prof. Mwandosya alitoa angalizo kuwa kuna haja ya kuongeza wigo kutoka kwenye udhibiti huduma za umma na kushirikisha pia udhibiti wa shughuli za kiuchumi zikiwemo za bima na hifadhi ya jamii. Pamoja na mamlaka hizi kusimamia sekta tofauti lakini zinakabiliwa na changamoto zinazofanana. Kutokana na hali hiyo Waziri Prof. Mwandosya alishauri kuna haja kuwa na chombo kimoja ambacho kitajumuisha vyombo vyote vya udhibiti kwa ajili ya kujadiliana na kubadilishana uzoefu katika kutekeleza majukumu yao.

Waziri Prof. Mwandosya pia aliwaasa Mamlaka hizi za udhibiti kufanya kazi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo badala ya kufuata maelekezo au kufanya maamuzi ya kuwafurahisha wanasiasa. Muelekeo ni kwamba kunakuwepo na huduma kwa umma ili wananchi waweze kuchangia ipasavyo katika uchumi wa nchi.
Mheshimiwa Prof. Mark Mwandosya akizungumza na Uongozi wa Mamlaka ya Udhibiti Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) alipotembelea ofisi za Mamlaka hiyo katika ziara yake tarehe 21 Julai, 2014. Kushoto kwa Waziri Prof. Mwandosya ni Mkurugenzi Mkuu wa SUMATRA Bwana Gilliard Ngewe. 
Baada ya majadiliano na Uongozi wa SUMATRA Mheshimiwa Prof. Mark Mwandosya alimkabidhi Mkurugenzi Mkuu wa SUMATRA Bwana Gilliard Ngewe kitabu cha Udhibiti wa Huduma za Kiuchumi Tanzania alichokiandika Prof. Mwandosya.
Mheshimiwa Prof. Mark Mwandosya katika picha ya pamoja na Uongozi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) alipotembelea ofisi za Mamlaka hiyo katika ziara yake tarehe 21 Julai, 2014. Kulia kwa Waziri Prof. Mwandosya ni Mwenyekiti wa Bodi ya EWURA na kushoto kwake ni Mkurugenzi Mkuu wa EWURA Bwana Felix Ngamlagosi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...