VIONGOZI na watendaji mkoani Pwani wametakiwa kuhakikisha kuwa miradi yote ya maendeleo inayozinduliwa katika kipindi cha mbio za mwenge iwe endelevu ili iwasaidie wananchi na si kwa ajili ya mbio hizo.

Baadhi ya miradi imeonekana kuzinduliwa na viongozi wa mbio za mwenge lakini baada ya muda inakufa jambo ambalo si malengo ya miradi hiyo ambayo imekuwa mkombozi kwa wananchi katika kutatua changamoto za kupata huduma za kijamii.

Hayo yamesemwa na kiongozi wa mbio za Mwenge Kitaifa Rachel Kasanda kwenye kijiji cha Bungu wakati wa kuweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa stendi ya mabasi ya Ikwiriri wilayani Rufiji mkoani humo.

Kasanda amesema kuwa miradi hiyo inapaswa kuwa endelevu ili jamii iweze kunufaika na si kuwa ya muda kwa ajili ya mwenge kwani hiyo ni michango ya wananchi, wahisani na serikali hivyo lazima iwe na manufaa.

Amesema kuwa Viongozi wanapaswa kuhakikisha kuwa miradi hiyo inafanya kazi baada ya kuzinduliwa kwa kuwa endelevu na kutoa matunda ambayo yanatarajiwa na wananchi kutokana na ujenzi wake.

Amesema kuwa baadhi ya viongozi wamekuwa wakifanya miradi hiyo kwa muda tu ambapo ikishazinduliwa inaachwa hapo hapo pasipo kuendelezwa na kusababisha kufa jambo ambalo halipaswi kuendelea kufumbiwa macho.

Aidha viongozi na watendaji ndiyo watu wa kuwaonyesha njia wananchi kwa hivyo wanapaswa kuhakikisha miradi hiyo inakuwa na mafanikio kwa wananchi ili kuwaondolea changamoto za upatikanaji wa huduma za kijamii.

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Rufiji mkoani Pwani Nurdin Babu amesema kuwa yeye kama kiongozi kwa kushirikiana na watendaji, viongozi na wananchi watahakikisha miradi hiyo inakuwa endelevu ili iwe na manufaa kwa wananchi.

Babu amesema kuwa wamejipanga kuhakikisha miradi hiyo inaleta manufaa kwa walengwa ambao ni wananchi kwani wamekuwa na changamoto nyingi ambazo zinatatuliwa hatua kwa hatua kwa kuwashirikisha wadau wa maendeleo. Mbio hizo za mwenge leo zitakuwa wilaya ya Kibaha.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...