Mkuu wa Shule ya Sekondari
Mwembetogwa, Kevin Mlengule
SHULE ya Sekondari ya Mwembetogwa ya Mjini Iringa imepongezwa na wadau wake baada ya hivikaribuni kuwafukuza kazi walimu wanne wa kiume waliobainika kuwa na mahusiano ya kimapenzi na wanafunzi wao wa kike maarufu  kama mafataki

“Tunataka shule nyingine ziige mfano wa shule hii, tumefarijika kusikia imechukua uamuzi huo na kwa kufanya hivyo tunaamini shule hiyo itakuwa salama kwa watoto wetu wa kike,” alisema mmoja wa wazazi wenye watoto wanaosoma shuleni hapo, Joachim Mwaikambo.

Mwaikambo alisema katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, kumekuwa na mabadiliko makubwa katika shule hiyo ambayo wanafunzi wake “tuliozoea kuwaona wakizurula mitaani wakati wa masomo.”

Naye Jacob Basil aliupongeza uongozi wa shule hiyo akisema; “unadhibiti nidhamu ya wanafunzi na watumishi wake jambo linalotupa faraja wazazi wenye watoto shuleni hapo.”

Akitetea uamuzi huo, Mkuu wa shule hiyo, Kevin Mlengule alisema pamoja na walimu hao shule iliwafukuza wanafunzi wa kike wawili waliobainika kukubuhu kwa ngono.

Alisema walimu na wanafunzi hao, walibainika kujihusisha na vitendo vinavyobomoa maadili ya watumishi na wanafunzi baada ya kura ya siri kupigwa dhidi yao.

“Katika kuboresha nidhamu kwa watumishi na wanafunzi wawapo shuleni jambo moja lililokuwa linatusumbua na tukaamua kulitafutia dawa kali ni la mahusiano ya mapenzi kati ya walimu na wanafunzi, na wanafunzi na watu wa mitaani,” alisema.

Alisema miaka mitatu iliyopita lilikuwa ni jambo la kawaida kwa wanafunzi wa kike kujihusisha katika mapenzi na walimu wao pamoja na watu wengine kutoka mitaani.

Hali hiyo ilipelekea baadhi ya wanafunzi wenye tabia hiyo kufuatwa “na wanaoitwa mabwana zao” shuleni muda wowote na kutoroshwa.

Alisema hali hiyo ilichangia kuporomosha taaluma shuleni hapo na kufanya matokeo ya wanafunzi wanaomaliza shule hiyo kuwa mabaya kwa muda mrefu.

Mlengule alisema matokeo hayo yaliwafanya baadhi ya wazazi kuwahamisha watoto wao kutoka katika shule hiyo na kuwapeleka shule nyingine.

“Shule ilikuwa na wastani wa wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha sita 2,500 kila mwaka, matatizo hayo na mengine yaliyokuwepo yaliifanya ibakiwe na wanafunzi wasiozidi 600.” Alisema.

Alisema katika kukabiliana na utovu wa nidhamu; “hatuna mzaha hata kidogo, mwalimu na mwanafunzi atakayebainika akijihusisha na ngono katika mazingira yoyote yale wote kwa pamoja tunawafukuza.”


Aliwataka wazazi waliohamisha wazazi wao shuleni hapo kutoihofia tena hali hiyo kwani imedhibitiwa vya kutosha.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...