Wahandisi wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO) wameanza kunolewa katika kutambua nguzo bora za kusambazia umeme majumbani katika kukabiliana na matumizi ya nguzo zisizo na ubora na ili kuongeza ufanisi na usalama katika zoezi la kusambaza umeme nchini.

Mafunzo hayo ya wiki mbili yanayofanyika mkoani Iringa kujumuisha wahandisi wakuu wa umeme, maafisa mipango na maafisa usalama wa TANESCO yana lengo la kuwawezesha wataalamu hawa kuwa na weledi wa hali ya juu katika kutambua nguzo zenye sifa na umadhubuti na salama katika zoezi la usambazaji umeme nchini.

Akifungua mafunzo hayo Kaimu Meneja wa Mkoa wa Iringa Mhandisi Seraphine Lyimo alisema anaamini mafunzo haya yatawawezesha washiriki kufanya vizuri zaidi katika utendaji wao wa kazi na kuongeza kuwa Shirika halitapata tena nguzo ambazo hazina viwango na kuwataka washiriki kuendelea kujisomea zaidi na kuzielewa nguzo ili kuokoa rasilimali chache za Shirika.

Mhandisi Lyimo aliongeza kuwa mafunzo hayo yana faida kubwa kwa TANESCO kwani yatasaidia Shirika kuepuka kununua nguzo feki na hivyo kuweza kuliepushia Shirika hasara zisizo za lazima.

“Nawaomba muzingatie mafunzo haya ili muje kutumia utaalamu huu katika kulisaidia Shirika wakati wa manunuzi ili kuweza kuwapatia Watanzania huduma bora na salama ili kukidhi kiu yao ya hupatikanaji wa umeme,” alisema Mhandisi Lyimo.

Kwa upande wake, Mkufunzi wa Mafunzo hayo, Prof. Reuben Mwamakimbullah kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo (SUA), alisema kuwa baadhi ya vitu vinavyochangia kuharibu ubora wa nguzo ni pamoja na kutoboa nguzo matundu wakati imeshawekewa dawa; na kuongeza kuwa maji nayo huchangia kuzuia uwezo wa dawa kupenya kwenye nguzo na ujazo wa hewa ndani ya nguzo ambayo inatakiwa nayo itolewe ili dawa iweze kupata nafasi.

Prof. Mwamakimbullah aliwasihi washiriki wa mafunzo hayo kuwa waangalifu katika utambuzi wa nguzo za matumizi ili kuokoa uwezekano wa kuhatarisha maisha ya watumiaji na pia kuliokolea Shirika hasara.

“Nawaomba muzingatie ubora wa nguzo kwa kuzingatia unaandaaje nguzo zako, unatumia dawa gani na unatumia njia gani kuingiza dawa katika nguzo,” aliwasihi Prof. Mwamakimbullah.

Prof. Mwamakimbullah aliwataka washiriki kufanya kazi kwa pamoja na kushirikiana akiwasihi ili kufikia malengo ya Shirika wataalamu hao hawana budi kushirikiana na wengine ili kuwezesha TANESCO huduma bora na bidhaa bora.

Naye msimamizi wa mafunzo hayo Meneja wa kitengo cha usalama kazini wa TANESCO, ambao ndio waandaji Mhandisi Majige Mabulla alisema: “Tunategemea kuona ufanisi katika utendaji kutokana na mafunzo haya mkayoyapata, kwa faida ya kwako mshiriki na pia kwa faida ya Shirika.”

Kwa mujibu wa taratibu za usalama, nguzo inatakiwa kwa kawaida ikae sio chini ya miaka 40 na takwimu zinaonesha kuwa nguzo zisizo na ubora kwa wastani wa hazifiki miaka zaidi ya saba.
Msimamizi wa mafunzo hayo Meneja wa Kitengo cha Usalama Kazini ambao ndio waandaji Mhandisi Majige Mabulla akiwakaribisha washiriki na kuelezea namna ambavyo mafunzo hayo yataendeshwa kwa nadharia na vitendo.
Prof. Reuben Mwamakimbullah kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo (SUA) akionesha kwa vitendo namna kuangalia maji kwenye nguzo kwa kutumia kifaa kinachoitwa ‘Electrical Resistance Metter’.
Kaimu Meneja wa Mkoa wa Iringa Mhandisi Seraphine Lyimo akifungua mafunzo hayo awamu ya pili.
Washiriki wakifuatilia mafunzo kwa umakini Picha zote na Henry Kilasila.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. AnonymousJuly 22, 2014

    Ankali,
    Shukrani kwa kutuletea habari za kutia moyo kuhusu msisitizo wa kuhakikisha ubora wa nguzo za TANESCO.

    Ila pia uweke usimamizi wa karibu katika uandiakaji wa habari ili viwango vya Globu ya Jamii visiporomoke. Mfano kusema Chuo Kikuu cha Kilimo (SUA), hapa uandishi hauna viwango.

    Chuo Kikuu cha Kilimo (SUA) ni Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine a.k.a Sokoine University of Agriculture (SUA), mkoani Mrorogoro.

    Globu ya Jamii lazima ijitofautishe na magazeti 'Pendwa' katika kuandishi wa habari.

    Mdau
    Christos Papachristou
    Diaspora.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...