Soko la Hisa Dar es Salaam (Dar es
Salaam Stock Exchange), kwa udhamini wa benki ya NMB, Selcom na FSDT, linapenda
kuwajulisha wanafunzi wa elimu ya juu nchini walioshiriki katika shindano la
elimu ya uwekezaji kwa mwaka 2014 (DSE Scholar Investment Challenge 2014) kuwa
maandalizi yote ya kuhitimisha shindano hili kwa sasa yamekamilika.
Mchakato wa kutambua nafasi ya kila
mshiriki wa shindano umemalizika. Majina ya wanafunzi 50 wanaoongoza katika
shindano hilo yamebandikwa katika mtandao wa DSE (www.dse.co.tz) kwenye kipengele cha
Investment Challenge.
(sehemu ya
umati wa wanafunzi walioshiriki katika elimu ya uwekezaji kwenye hisa na masoko
ya mitaji nchini iliyoendeshwa na DSE kwa wanazuoni).
Shindano la elimu ya uwekezaji kwa
wanazuoni (DSE Scholar Investment Challenge) lilianza tarehe 01/04/2014 na
kumalizika tarehe 30/06/2014. Wanafunzi washiriki walipewa nafasi ya kutumia
simu zao za mkononi ili kununua na kuuza hisa zinazouzwa katika soko la hisa
(DSE) la Dar es Salaam. Kila mshiriki alipewa mtaji (virtual capital) wa
shilingi milioni moja. Ushiriki kwa shindano hili ulikuwa ni bure na huru kwa
yeyote aliyependa.
Nia kubwa ya shindano hili ni
kuwapatia vijana walio katika vyuo vya elimu ya juu nchini fursa ya kuwekeza
katika soko la hisa kwa majaribio na kuangalia mitaji yao ikikua. Elimu hii pia
ni muhimu katika kujenga utamaduni wa utunzaji fedha na uwekezaji miongoni mwa
vijana walio vyuoni (ambao ni viongozi, wawekezaji, wahasibu, wachumi, na
washauri watarajiwa).
Washiriki walitegemewa kushindana
kukuza mitaji waliyopewa kwa kipindi cha miezi mitatu. Mafanikio ya shindano na
elimu hii ni makubwa sana. Mwanafunzi anayeongoza amekuza mtaji wake kutoka shilingi
milioni moja aliyopewa na kufikisha shilingi milioni nne (kwa kipindi cha miezi
mitatu tu).
DSE inawapongeza zaidi ya wanafunzi
5,000 walioshiriki katika shindano na elimu hii muhimu kwao na taifa kwa ujumla.
Shindano na elimu hii imepangwa kufanyika
tena mwakani na kuwahusisha wanafunzi wengi zaidi ya elfu tano walioshiriki
mwaka huu. DSE imepanga kuwawezesha wanafunzi na vijana nchini kutumia simu
pamoja na intaneti mwakani ili kuwapa uwanja mpana zaidi wa kushiriki. Mipango
ya baadaye ni kuwashirikisha wanafunzi walioko kwenye shule za sekondari pia.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...