Kituo cha Radio 5, kimepongezwa na wadau wa sanaa kwa mchango wake wa kukuza sanaa za vichekesho vya majukwaani hapa nchini.

Wadau hao wa sanaa za vichekesho vya majukwaani waliipongeza Radio 5, wakati wa burudani ya wachekeshaji wa majukwaani iliyofanyika mwishoni mwa wiki hii katika ukumbi wa Golden Tulip. Burudani hiyo ambayo ilifana sana iliwajumuisha mchekeshaji kutoka Uganda, mwanadada Anne Kansiime, Fred Omondi kutoka Kenya na Pilipili wa Tanzania.

Akizungumzia onyesho hilo, mmoja ya mashabiki waliohudhuria onyesho hilo, amesema sanaa ya vichekesho vya majukwaani nchini haijapewa kipaumbele kama aina nyingine za sanaa. ‘Watu wengi bado wanaamini sanaa za kuchekesha majukwaani sio kazi rasmi kama kazi nyinginezo, lakini hii imeanza kubadilika hapa nchini, na tutarajie mabadiliko zaidi kama wadau wengine kama radio 5 wakijitokeza kusaidia’ alisema Farida Akida.

Akijibu swali aliloulizwa na waandishi wa habari kuhusiana na anavyoiona tasnia ya vichekesho vya majukwaani Afrika Mashariki, mchekeshaji Anne Kansiime anasema anaamini sanaa ya vichekesho vya majukwaani inaanza kujijengea heshima kubwa miongoni mwa wananchi.  ‘Mimi sio mbunge au mwanasiasa, lakini nimepata mapokezi makubwa, kwa kazi hii tu ya kuchekesha watu, hivyo naona hii tu pekee ni dalili ya kukua kwa tasnia hii hapa Afrika Mashariki’ alisema Anne.

Ikiwa ni mara ya kwanza kwa mwanadada Kansiime kuja Tanzania kutoa burudani, hasa baada ya kujijengea umaarufu mkubwa kupitia vipande vyake vya vichekesho vilivyo mtandaoni, tiketi za burudani yake ziliisha wiki moja kabla hajawasili.  Katika usiku huo wa burudani ulioitwa, Cheka Kwa Nguvu, mchekeshaji toka Tanzania, Pilipili aliwatoa kimasomaso mashabiki waliofurika kwa vichekesho vyake vilivyoonekana kuwagusa mashabiki moja kwa moja.

Huku mashabiki wengi wakiwa hawamfahamu vyema, Pilipili ambaye kitaaluma ni mwalimu, anasema aliacha kazi ya ualimu ili awe mchekeshaji, hivyo kwake yeye, kuchekesha ni kazi kama kazi nyingine. ‘Kwangu mimi hii ni kazi ambayo najivunia, na naamini nitaweza kuwawakilisha watanzania vyema kimataifa kupitia uchekeshaji, na naishukuru Radio 5 kwa kunipa fursa ya kuonyesha kwamba ninaweza’ alisema Pilipili.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa kituo cha Radio 5, Robert Francis amesema huu ni mwanzo tu wa kuwaandalia watanzania burudani za kipekee na watarajie mengi zaidi kutoka Radio 5. ‘Sanaa ya uchekeshaji jukwaani bado haijapewa nafasi kubwa hapa nchini, lakini kama mlivyoona, mashabiki wamejitokeza kwa wingi sana kwenye burudani yetu, hivyo watu watarajie burudani za aina hii nyingi zaidi kutoka kwetu’ alimaliza Francis.
 Sehemu ya washabiki na wapenzi wa fani hiyo wakivunjika mbavu kwa kucheka.
 mwanadada Anne Kansiime kutoka nchini Uganda akitoa burudani ya vichekesho kwa watazamaji (hawapo pichani),ndani ya moja ya ukumbi wa hotel ya Golden Tulip jijini Dar hivi karibuni

Wasanii wa fani ya Uchekeshaji mahiri kutoka nchini Uganda,Kenya na Tanzania wakitoa burudani kwa washabiki na wapenzi wa fani hiyo ,iliofanyika kwenye moja ya ukumbi wa hotel ya Golden Tulip Jijini Dar,pichani shoto ni Fred Omondi kutoka Kenya,mwanadada Anne Kansiime kutoka nchini Uganda na Mc Pilipili wa Tanzania.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...