Na Mwene Said wa Blogu ya Jamii
Aliyekuwa Mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Bandari (TPA), Ephraim Mgawe amekiri katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa aliusaini mkataba wa kibiashara kati ya TPA na Kampuni ya China Communications Company Ltd (CCCCL).
Mgawe amekiri kuusaini mkataba huo wa kibiashara leo wakati akisomewa maelezo ya awali (PH) na Wakili wa Serikali, Pius Hilla mbele ya Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Isaya Arufani.
Akisomewa maelezo ya awali yanayohusiana na shtaka la matumizi mabaya ya madaraka Mgawe alikubali wadhifa wake huo na kwamba aliusaini mkataba huo wa kibiashara siyo kwa ajili ya ujenzi wa ghati namba 13 na namba 14 katika Bandari ya Dar es Salaam bali ni kwa minajili ya kuiwezesha kampuni hiyo kupata mkopo nchini mwake China.
Mgawe pia alikubali mahakamani hapo kuwa mwaka 2008 kulikuwepo na mpango wa upanuzi wa bandari wa mwaka 2009-2028 kwa ajili ya upanuzi wa bandari na ujenzi wa ghati na Agosti 9,2009 walikaribisha maoni ya kupata washauri na wataalam wakufanya upembuzi yakinifu wa mradi huo.
Akiendelea kusomewa maelezo ya awali, Mgawe alikiri kuwa kampuni tano ziliwasilisha mialiko yao ya kutaka tenda hiyo ambazo ni kampuni ya MTBS ya Nethelands, Scott Wilson ya Uk, Ecorys ya Germany, Mott MacDonald Maritime Consultants ya Uk, HPS Humburg ya Ujerumani, SCEC International PTY Limited ya Australia na CPCS Transcom ya Canada.
Mshtakiwa huyo pia alikiri kuwa kampuni ya nchini Canada ya CPCS na kutaja gharama yao kuwa ni dola 323 za kimarekani ndiyo iliyoshinda zabuni lakini iliyopewa kazi ya upanuzi wa bandari ni Kampuni ya China Communications Company Ltd ya China ambayo ilitaja gharama zake kuwa ni dola 523,131,015.97.
Hata hivyo mshtakiwa huyo alikana kuwa baada ya kupewa taarifa hiyo ya gharama za mradi na kampuni ya China ya CCCL alikaa kimya bila ya kutoa kwenye bodi ya wakurugenzi.
Mgawe na mwenzake Hamad Mussa Koshuma ambaye alikana kuwa na cheo cha Naibu Mkurugenzi Mkuu mahakamani hapo na kudai kuwa yeye ni Mkurugenzi Mkuu Msaidizi kwa pamoja wanadaiwa kutenda makosa hayo Desemba 5, 2011.
Ilidaiwa kuwa washtakiwa hao wakati wakiwa kwenye Mamlaka ya Bandari Tanzania, jijini Dar es Salaam, wakati wakitekeleza majukumu yao ya utumishi wa mamlaka hiyo kwa nafasi ya mkurugenzi mkuu na naibu wake walitumia vibaya madaraka ya kuingia mkataba wa kibiashara kati ya TPA na Kampuni ya China Communications Company Ltd, kwa ajili ya ujenzi wa ghati namba 13 na namba 14 katika Bandari ya Dar es Salaam.
Kwa pamoja washtakiwa hao wanadaiwa kuingia mkataba na kampuni hiyo bila kutangaza zabuni hiyo, kinyume cha masharti ya kifungu cha 31 cha Sheria ya Ununuzi wa Umma, namba 21 ya mwaka 2004, kwa lengo la kuinufaisha kampuni hiyo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...