UZINDUZI wa msimu wa sita wa mbio za Rock City Marathon 2014
zilizoanza mwaka 2009, zikiwa na lengo la kukuza Utalii wa Ndani
kupitia michezo, unatarajia kufanyika Septemba 10, kwenye Hoteli ya
New Afrika, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mratibu wa mbio hizo, Bi. Grace
Sanga, alisema kuwa baadhi ya wanariadha, viongozi wa vyama vya
riadha, viongozi wa Baraza la Michezo Tanzania na wadau mbali mbali wa
mchezo wa riadha nchini wanatarajiwa kuhudhuria uzinduzi huo.

Bi. Grace alisema kuwa pamoja na maandalizi ya mbio za mwaka huu za
Rock City Marathon kuboreshwa zaidi  ukilinganisha na miaka
iliyotangulia, wawakilishi wa wanariadha na viongozi mbali mbali
watapata fursa ya kuzungumzia changamoto zinazokumba mchezo wa riadha
nchini na jinsi ya kukabiliana nazo.

“Tuko tayari kwa mbio za Rock City Marathon 2014, zitakazofanyika
Oktoba 26. Kamati ya Maandalizi imeweka mikakati mizuri ili
kuhakikisha mbio za mwaka huu zinakuwa bora na zenye mafanikio
kulinganisha na misimu iliyopita,” alisema Bi. Grace.
Mratibu huyo alisema kuwa kwa kutokana na uendeshaji wa kuridhisha wa
mbio hizo, wadhamini wengi wamejitokeza kuwezesha kuzifanya mbio hizo
kuwa bora zaidi mwaka huu.

“Baada ya kufanya maandalizi ya Rock City Marathon kwa mafanikio kwa
miaka tano mfululizo na kuweza kupandisha kiwango chake, makampuni na
mashirika mengi yamejitokeza kudhamini mbio za mwaka huu kwa lengo la
kuiboresha zaidi. Miongoni mwa wadhamini wetu mwaka huu ni pamoja na
NSSF, TSN Group, African Barrik Gold, IPTL, TTB, TANAPA, New Mwanza
Hotel, Nyanza Bottling Company, Sahara Communications, New African
Hotel, Continental decoders, ATCL, PPF, Umoja Switch, and Bank M,”
alisema Bi. Grace.

Rock City Marathon zinaandaliwa na Kampuni ya Capital Plus
International (CPI), kwa ushirikiano na Chama cha Riadha Tanzania
(RT), pamoja na Chama cha Riadha mkoa wa Mwanza (MRAA), ambazo
zimewavutia washiriki wengi wa ndani na nje ya nchi.

Bi. Grace aliongeza kwamba, mbio hizo zitakuwa na vipengele vitano kwa
msimu huu, ambavyo ni mbio za kilometa 21 (wanawake na wanaume) na
zile za kilometa tano kwa wakimbiaji kutoka makampuni mbalimbali,
kilometa tatu kwa watu wenye ulemavu, kilometa tatu kwa watu wazima
(zaidi ya miaka 55) na kilometa mbili kwa watoto walio kati ya miaka 7
mpaka 10.

“Tunatarajia watu wengi kujitokeza mwaka huu, kwa kuwa tumejipanga
vizuri kwa msimu huu. Tumejifunza kupitia mbio za mwaka jana, hivyo
Kamati ya Maandalizi imekuja na mpango madhubuti utakaoboresha mbio
zetu kwa mwaka huu,” alisema Bi. Grace.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...