Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban ki Moon akizungumza na waandishi wa habari ( hawapo pichani) siku ya jumanne ambapo alitumia fursa hiyo kuainisha masuala mbalimbali yatakayopewa kipaumbele wakati wa Mkutano wa 69 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa unaoanza wiki ijayo hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, jijini New York, Marekani. Mlipuko wa Ugonjwa wa Ebola ni moja ya suala litakalopewa kipaumbele cha pekee wakati wa mkutano huo utakaohudhuriwa na wa viongozi zaidi ya 140 wakuu wa nchi na serikali, viongozi wa asasi za kiraia, na wakuu wa mashirika mbalimbaliya Kimataifa.
====== ======= =======
UMOJA WA MATAIFA KUJADILI UGONJWA WA
EBOLA-BAN KI MOON
Na
Mwandishi Maalum, New New York
Viongozi Wakuu wa Nchi na Serikali zaidi ya 140 kutoka mataifa mbalimbali duniani
wamethibitisha kuhudhuria na
kushiriki majadiliano ya jumla wakati wa Mkutano wa 69
wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa unaoanza wiki ijayo.
Akizungumza na waandishi wa habari hapo siku ya Jumanne, Katibu Mkuu wa Umoja wa
Mataifa, Ban Ki Moon, amesema, viongozi hao pamoja na kujadili
changamoto mbalimbali zinazoikabili dunia hivi sasa, watautumia mkutano huu kujadiliana kwa kina
kuhusu mchango na ushiriki wa jumuiya ya
kimataifa katika kuukabili mlipuko wa
ugonjwa hatari wa Ebola. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete ni
miongoni wa viongozi hao 140 na anaongoza
ujumbe wa Tanzania katika Mkutano huu.
Akizungumzia zaidi kuhusu mlipuko wa ugonjwa
hatari wa Ebola na athari zake kwa uhai wa mwanadamu na kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii, Ban ki
Moon amewaeleza waandishi hao,
kuwa Jumuiya ya kimataifa haiwezi kuendelea kuufumbia macho na kwamba kadiri
inavyochelewa kuutafutia ufumbuzi ndivyo
hatari yake inavyozidi kuongezeka.
“Tutatoa kipaumbele cha peke kuhusu
ugonjwa wa Ebola ambao umeleta athari kubwa kwa baadhi ya nchi za Afrika ya
Magharibi na maeneo mengine. Siku mbili zijazo ( Alhamisi) Baraza Kuu la
Usalama la Umoja wa Mataifa litakutana kwa dharura kuzungumzia mlipuko wa
Ebola. Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani Margaret Chan na Mimi
tutazungumza katika mkutano huo” akasema Ban Ki Moon.
Akaongeza kwa kusema wiki ijayo
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa litakuwa na mkutano wa kilele kuhusu mahitaji ya
watu na nchi zilizokabiliwa na ugonjwa wa Ebola. Pamoja na kujadili
na kutafuta mkakati wa pamoja wa kukabiliana na Ebola, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anasema
viongonzi hao wakuu wa nchi na serikali pia wanatarajiwa kujadili na kubadilishana mawazo kuhusu
changamoto za mabadiliko ya tabia nchi katika mkutano utakaofanyika septemba 23.
Mhe. Rais Jakaya Kikwete ni kati ya Viongozi
walioalikwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhudhuria na kuzungumza katika mkutano huu
muhimu kuhusu suala zima la mabadiliko
ya tabia nchi na athari zake.
Akielezea zaidi kuhusu mkutano huo wa
mabadiliko ya tabianchi, Ban Ki Moon anasema
mkutano huo utakuwa na malengo mawili, kwanza ni kukusanya utashi wa
kisiasa ili kufikia makubaliano ya
pamoja hapo mwakani katika mkutano utakaofanyika huko Paris , Ufaransa. Na pili
kuchukua hatua madhubuti za kupunguza
uzalishaji wa gesi chafu.
Akiainisha zaidi kuhusu ajenda mbalimbali zitakazojadiliwa
wakati wa Mkutano wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa, Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa, amesema, majadiliano ya Baraza Kuu ( General Debate) yatakayoanza
septemba 24 yatatumika kukusanya nguvu za pamoja za kuushinda umaskini, na kupitisha ajenda za
malengo mapya ya maendeleo endelevu .Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete
atalihutubia Baraza Kuu Septemba 25.
Masuala mengine ambayo pia yanatarajiwa kutawala mkutano huo wa
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa mujibu wa
Ban Ki Moon, ni pamoja na
migogoro na machafuko yanayoendelea katika nchi za Syria, Iraq, Libya, Mali, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Ukraine, Sudan ya
Kusini ukiwamo pia mgogoro kati ya Palestina na Israel.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...