Warembo wataoshiriki fainali za Miss Tanzania Jumamosi katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es salaam
Kutoka maktaba: Hashim Lundenga akiwa na mshirika wake
Prashant Patel katika moja ya mashindano ya urembo yaliyopita

Na Mwene Saidi, Kisutu
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam imeamuru mashindano ya urembo Tanzania yaliyopangwa kufanyika Oktoba 11, mwaka huu kuendelea baada ya kutupilia mbali maombi ya dharura yaliyowasilishwa na Prashant Patel dhidi ya Hashimu Lundenga ya kuzuia kuendelea kuendesha kinyang'anyiro hayo kwa madai ya kukiuka mkataba wa makubaliano yao. 
 Kadhalika mahakama hiyo imesema maombi ya hati ya dharura yaliyowasilishwa na Patel hayana mashiko ya kisheria na kwamba kuzuia kufanyika mashindano hayo ambayo madhamini mbalimbali wamewekeza fedha zao itasababisha mgangano wa kimaslahi. 
 Uamuzi huo ulitolewa jana na Hakimu Mkazi Frank Moshi baada ya kusikiliza hoja za mawakili wa pande zote mbili kuhusu maombi hayo ya dharura ya kuzuia mashindano hayo kufanyika Oktoba 11, mwaka huu. Hakimu Moshi alisema mlalamikaji amefungua kesi mahakamani hapo pamoja na maombi ya hati ya dharura akiitaka mahakama yake kuzuia mashindano kufanyika kutokana na mlalamikiwa kuvunja haki dhidi ya mwanzilishi mwenzake Patel. 
 Alisema Patel kupitia hoja za maombi yake, amedai kuwa Lundenga alivunja mkataba huo kwa kufanya mawasiliano moja kwa moja na mawakala bila kumshirikisha. Hata hivyo, mahakama bila kuacha shaka imeona hakuna sababu za msingi katika hati hiyo ya kusababisha mashindano hayo yasifanyike na kwamba hayawezi kuathiri kesi ya msingi iliyofunguliwa na mlalamikaji huyo. 
 “Mahakama imeona hakuna sababu ya kuzuia mashindano hayo kwa sababu wadhamini na washiriki wametumia gharama zao na kwamba kwa kufanya hivyo kutasababisha mgongano wa kimaslahi” alisema Hakimu Moshi wakati akitupilia mbali hati hiyo ya dharula. 
 Akifafanua zaidi alisema hati ya dharura ya mlalamikaji haina mashiko kisheria kwa sababu kesi yake ya msingi ipo mahakamani na kwamba haina uhusiano na mashindano yatakayofanyika Oktoba 11, mwaka huu. Mapema juzi, mahakama hiyo ilitupilia mbali pingamizi la awali la Lundenga lililotaka hati hiyo ya dharura kutupiliwa mbali.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. Kuna kila dalili ya mchezo mchafu!

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...