Fundi wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA)
akifanyia marekebisho moja ya mabasi ya shirika hilo.
Wakazi wa Dar es Salaam wataanza kupokea huduma
zilizoboreshwa zaidi kila watakapotumia mabasi yanayomilikiwa na Shirika la
Usafiri Dar es Salaam (UDA), hii inatokana na mafunzo ya mwezi mmoja
yanayotolewa na shirika kwa madereva, makondakta pamoja na wafanyakazi wengine
wa shirika hilo.
Akizungumza wakati wa ziara fupi ya waandishi wa
habari katika makao makuu ya UDA jijini Dar es Salaam Jana, Mkuu wa kitengo cha
mahusiano ya umma wa UDA, Bw. George
Maziku alisema kuwa miongoni mwa mambo mengine, kampuni yake imejikita katika
utoaji wa mafunzo madhubuti kwa wafanyakazi wake ili kuboresha huduma zote
zinazotolewa kwa wateja wa UDA.
“Uongozi wa UDA unalichukulia kwa uzito mkubwa
sana suala la usalama. Tumeupitia mtaala wa utoaji elimu kwa wafanyakazi wetu
lengo likiwa ni kuboresha usalama na kufanya wateja wetu wafurahie huduma
zinazotolewa na shirika. Tunatoa mafunzo haya kwa madereva wetu ili kuinua hali
yao ya uzingatiaji wa usalama,” alisema Maziku.
Mbali na
masuala ya usalama, mkuu huyo wa kitengo cha uhusiano aliahidi uboreshaji wa
huduma kwa ujumla ikiwa ni pamoja na kuwajali wateja, suala ambalo limekua
likizua mjadala mkubwa.
Bw. Maziku alisema kuwa kampuni yake ina mabasi yapatayo 400 jambo
linayoifanya UDA kuwa kampuni ya kwanza Tanzania kuwa na magari mengi
yanayofanya kazi kwa mkupuo, hivyo kuna uhitaji mkubwa sana wa kuweka viwango
thabiti ambavyo vinaweza kuigwa na makampuni mengine.
“Tunalenga kuwa na mabasi 3000 ifikapo mwakani lakini kikubwa zaidi
kabla hata ya kupata idadi hiyo ya mabasi ni kuwapa mafunzo madereva wetu ili
wawe na elimu ya kutosha na uzoefu wa kutosha katika sekta ya usafirishaji wa
umma.
“Kwa kulitambua hili, kampuni imeajiri wakufunzi kutoka ndani na nje ya
nchi, ili kutoa mafunzo kwa madereva wetu na wafanyakazi wengine wanaojihusisha
na usafirishaji, mafundi na wafanyakazi wote (hasa makondakta) katika kuwajali
wateja,” alisema.
Bw. Maziku alisema kuwa mbali na mafunzo hayo, kampuni imekuwa ikifuatilia
kwa karibu sana tabia na mienendo ya
madereva na makondakta wake mara kwa mara kwa kuwatumia wasimamizi ambao
hupanda mabasi ya kampuni hiyo bila ya makondakta na madereva kupewa taarifa.
Kwa sasa, mafunzo yaliyokuwa yakitolewa na kampuni hapo awali, yameonyesha
kuzaa matunda yaliyotarajiwa kwa kuwabadilisha baadhi ya madereva na makondakta
wa kampuni hiyo.
Hii ilibainika baada ya mkazi wa Dar es Salaam, ambaye amekuwa akitumia
huduma za UDA kwa nyakati tofauti, Bw. Andrew Sanga , kukiri kuwa madereva wa
UDA wapo tofauti ukilinganisha na madereva wengine wa mabasi ya abiria.
“Ilikuwa ni adha kubwa kutumia usafiri wa umma kutokana na huduma mbovu
ambazo abiria tulikua tukikumbana nazo. Madereva wengi wa abiria hawazingatii
suala la usalama barabarani. Wanaendesha hovyo
bila kujali kuwa kuna watumiaji wengine wa barabara. Lakini nina furaha
kusema kuwa madereva wa UDA wapo tofauti sana na wenzao,” alifafanua.
Hongereni sana, kwa mtindo huo mtapunguza ajali za makusudi na vifo vya makusudi. Ningependa zaidi kama mungepata mabasi mazuri ya kusafilia toka mkoa kwa mkoa kama shirika lenu ili kupunguza msongamano wa mabasi ya watu binafsi yaliyochoka na kusababisha ajali mara kwa mara. Pateni hata mabasi makubwa mawili mawili kila mkoa yaani linalokwenda na linalorudi kama wafanyavyo wenzetu wa nchi za nje.
ReplyDelete