Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Kimataifa Mhe. Bernard Membe amewataka Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania
katika mataifa mbalimbali ulimwenguni kuhakikisha kuwa wanatangaza vivutio vya
utalii vilivyopo nchini ikiwa ni njia mojawapo ya kutekeleza diplomasia ya
uchumi.
Waziri Membe aliyasema hayo wakati
akizindua zoezi la kupanda Mlima Kilimanjaro linalofanywa na mabalozi
mbalimbali wanaoiwakilisha Tanzania nje ya nchi kwa lengo la kuutangaza Mlima
Kilimanjaro ili uweze kuvutia watalii wengi zaidi.
“Bado idadi ya watalii wanaofika nchini
kupanda mlima hairidhishi na jitihada kubwa zinahitajika kufanywa na mabalozi
kuhakikisha kuwa wanautangaza vema mlima kwa kuwa ni hazina ya pekee tuliyonayo
inayopaswa kuwa kitega uchumi kizuri kwa uchumi wan chi yetu” alisema Membe.
Jumla ya mabalozi
14 wanashiriki zoezi hili ambalo litakuwa likifanyika kila mwaka kwa lengo la
kuutangaza Mlima Kilimanjaro. Mabalozi hao ni pamoja na Adadi Rajabu
(Zimbabwe); Ramadhani Mwinyi (Umoja wa Mataifa); John Kijazi (India); Batilda
Burian (Kenya); Shamim Nyanduga (Msumbiji); Grace Mujuma (Zambia); na Patrick
Tsere (Malawi).
Wengine ni pamoja
na Mbarouk Mbarouk (Saudi Arabia); Joseph Sokoine (Mkurugenzi Bara la Amerika);
Ladislaus Komba (Uganda); Azizi Mlima (Malaysia); Radhia Msuya (Afrika Kusini);
Daniel Ole Njoolay (Nigeria) na Charles Sanga (Balozi mstaafu na Mwenyekiti wa
Bodi ya Utalii ) .
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe. Bernard Membe (kulia) akimkabidhi Bendera ya Taifa Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe Adadi Rajabu ambaye ndiye kiongozi wa Timu ya Mabalozi wa Tanzania walioanza zoezi la kupanda Mlima Kilimanjaro kwa lengo la kuutangaza mlima na kuvutia wageni wengi zaidi nchini.
Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe Adadi Rajab pamoja na timu ya mabalozi anayoiongoza kupanda Mlima Kilimanjaro akinyanyua juu bendera ya taifa pamoja na kushangilia ikiwa ni ishara ya kuuthamini Mlima Kilimanjaro ambo ni chachu muhimu ya utalii nchini.
Baadhi ya Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania nje ya nchi wakisikiliza kwa makini hotuba zilizokuwa zikitolewa kabla ya uzinduzi rasmi wa zoezi lao la kupanda Mlima Kilimanjaro kwa lengo la kuutangaza ili uweze kuvutia wageni wengi zaidi nchini.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe. Bernard Membe akizungumza na Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania nje ya nchi muda mfupi kabla ya kuzindua safari yao ya kupanda Mlima Kilimanjaro kwa lengo la kuutangaza ili kuvutia watalii wengi nchini.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dk. Adelhelm Meru akitoa neno la ukaribisho kwa Mabalozi kupanda Mlima Kilimanjaro. Kulia ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe. Bernard Membe na kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA Ibrahim Mussa.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA Ibrahim Mussa akitoa maelezo ya Mlima Kilimanjaro kwa Waheshimiwa Mabalozi wa Tanzania.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...