WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema Watanzania watanufaika na kipato na maarifa ya teknolojia ya kisasa kutokana na ajira ambazo watapata katika nchi ya Qatar baada ya mkataba kusainiwa hivi karibuni. 
 Ametoa kauli hiyo leo mchana (Jumapili, Desemba 20, 2014) jijini Doha, Qatar wakati akizumgumza na waandishi wa habari ili kuwapa taarifa fupi juu ya mambo yaliyojiri kwenye mazungumzo yake na Waziri Mkuu wa Qatar, Sheikh Abdulla Nasser Al Thani. 
 Katika mazungumzo hayo ambayo yalifanyika ofisini kwa Sheikh Abdulla, Waziri Mkuu Pinda amesema wamekubaliana kutoa ajira kwa Watanzania kwa sababu nchi hii inahitaji wafanyakazi wengi kwenye sekta mbalimbali na raia wake ni wachache. 
 “Hivi sasa wapo Watanzania wanaofanya kazi hapa lakini ni wachache mno. Mazungumzo yalishaanza siku za nyuma. Tukisaini mkataba katika muda mfupi ujao, tutajua ni idadi gani wanahitajika na wanaweza kuja kila baada ya muda gani,” alifafanua Waziri Mkuu. 
 “Hapa Qatar kuna uwekezaji mkubwa umefanyika, kwa hiyo wanahitaji watu wa kufanya kazi... kwenye mahoteli, viwandani, na kikubwa hapa ninachokiona watu wetu watapata kipato lakini pia watapata ujuzi kwa maana ya maarifa yanayoendana teknolojia ya kisasa,” aliongeza. Akeleza mambo mengine ambayo wamekubalina kushirkiana kama nchi rafiki, Waziri Mkuu alisema kuna mambo makuu manne likiwemo hilo la ajira. 
“La kwanza ni Kilimo. Hapa Qatar ni jangwa kila mahali. Wamekubali kuja kuwekeza kwenye kilimo, ufugaji na uvuvi kwa sababu sisi tuko karibu nao zaidi kuliko Marekani au Brazil.
“Wanaweza kupata mchele, matunda, nyama kwa maana ya machinjio na viwanda vya kusindika nyama lakini pia katika uvuvi wa samaki. Tunayo bahari ila mitaji yetu ni midogo. Kwa hiyo wamekubali kuangalia eneo hilo pia,” alisema. 
 Alisema eneo la pili ni la gesi na mafuta. “Wamekubali kutusaidia utaalmu ili tushirikiane nao katika namna kutumia gesi kwenye ngazi ya chini hasa viwanda kwa sababu wenzetu wana uzoefu wa muda mrefu. Hata kwenye mafuta wameonyesha kuwa wako tayari,” alisema. 
Eneoa la tatu alilitaja kuwa ni kutoa fursa ya ajira kwa Watanzania na la nne ni TEHAMA. 
“Hawa wenzetu wamechanganya TEHAMA na sayansi na sasa wana Jiji la Sayansi na Teknolojia. Chini ya makubaliano tutakayofikia, watu wetu watakuja kujifunza masuala ya gesi na mafuta.” Alisema wamekubaliana na Sheikh Abdulla al Thani kuunda timu ya pamoja baina ya nchi zao ili ifanye kazi ya kuainisha ni maeneo gani wanataka waanze nayo kwanza kulingana na mahitaji. “Nimemuahidi nikifika nyumbani nitaandika barua ili mchakato wa kuunda timu uanze rasmi,” alisema. 
 Mchana huu, Waziri Mkuu Pinda atakuwa na mazungumzo ya Kiserikali na Mawaziri wa Kazi na Ustawi wa Jamii; Uchukuzi; Miundombinu na Uwekezaji wa Qatar. Naibu Mawaziri atakaokutana nao ni wa Uchumi na wa Nishati. 
 Jioni Waziri Mkuu amepangiwa kukutana na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Qatar (Qatar Business Community), wajumbe wa Chama cha Wafanyabiashara cha Qatar (Chamber of Commerce of the State of Qatar) na pia atakutana na Watanzania waishio Qatar. 
Kesho (jumatatu, Desemba 22, 2014) atatembelea Mamlaka ya Bandari ya Qatar na makao makuu ya kampuni ya uchimbaji gesi ya Qatar. 
 Waziri Mkuu amefuatana na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Titus Kimani; Waziri wa Kilimo na Maliasili wa Zanzibar, Dk. Sira Ubwa Mamboya; Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Mahadhi Maalim; Naibu Waziri wa Nishati, Bw. Charles Kitwanga; Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Bw. Godfrey Zambi. 
 Wengine ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Bw. Abbas Kandoro, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Bi. Halima Dendego, wabunge wawili Bi. Amina Makilagi na Bw. Aeshy Hilali, Dk. Gideon Kaunda wa TPSF na Bw. Shigela Malocha kutoka TPDC.
 IMETOLEWA NA: 
OFISI YA WAZIRI MKUU,
 DAR ES SALAAM. 
JUMAPILI, DESEMBA 21, 2014
 Waziri Mkuu Mhe.  Mizengo Pinda akiwa na Mwenyeji wake Waziri Mkuu wa Qatar Sheikh Abdullah Nasser Al Thani baada ya kuwasili kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu wa Qatar  iliyopo Doha kwa mazungumzo ya kiserikali akiwa katika ziara ya kikazi nchini humo leo. 
 Waziri Mkuu Mhe. Mizengo Pinda  akiongozwa na Waziri Mkuu wa Qatar, Sheikh  Abdullah Nasser Al Thani  kwenda  kwenye chumba  cha mikutano  baada ya kuwasili kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu huyo  iliyopo Doha  kwa mazungumzo ya kiserikali akiwa katika ziara ya kikazi nchini humo leo
 Waziri Mkuu Mhe. Mizengo Pinda akizungumza na Waziri Mkuu wa Qatar,  Sheikh Abdullah  Nasser Al Thani kwenye Ofisi ya  Waziri Mkuu huyo iliyopo Doha leo
Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Titus Kamani (kulia) akizugumza na Waziri wa Mazingira wa Qatar, Ahmed bin Amir Al Humaidi , kwenye Hoteli ya Sheraton iliyopo Doha nchini Qatar leo Desemba 21, 2014. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...