Na Hussein Makame, MAELEZO, Dodoma
KAMATI za Bunge za Serikali za Mitaa (LAAC) na ile ya Hesabu za Serikali (PAC), zimeridhishwa na mafanikio na hatua zilizochukuliwa na Serikali kwa kuongeza mapato yake na kushughulikia changamoto zinazoikabili katika kutekelza majukumu yake.
Kufuatia hali hiyo, Bunge limepitisha taarifa za kamati hizo na nyingine tatu, huku Serikali ikiahidi kufanyia kazi yale yote yaliyopendekezwa kwenye taarifa hizo ili kulipeleka Taifa kule kunakotakiwa.
Taarifa za Kamati ambazo Bunge limezipitishwa jana na juzi usiku ni za Kamati ya Bajeti, Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Hesabu za Serikali (PAC), Miundombinu na Nishati na Madini.
Akihitimisha hoja yake, Mwenyekiti wa Kamati ya LAAC Mhe. Rajabu  Mbarouk aliipongeza Serikali na Waziri wa TAMISEMI, Hawa Ghasia kwa hatua alichokua kwa watendaji wa Serikali waliobainika kutumia vibaya fedha za umma.
“Mimi ni mpinzani lakini kwa hili, kwa kweli nimpongeza Waziri kwa sababu jana aliniletea list (orodha) karibu ya halmashauri zote nchini ambazo wakurugenzi amewachukulia hatua, kilichobaki ni mimi kuichukua ile taarifa na kumpelekea kwa CAG kwa ajili ya kuihathibitisha” alisema Mbarouk.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya PAC, Zitto Kabwe aliipongeza Malmalaka ya Bandari Tanzania (TPA) kwa kuongeza mapato na kwamba wameiomba iongeze mapatao katika miaka ijayo ili kuifanya mamlaka hiyo iwe na tija kwa taifa.
“Ni lazima tuwe wakweli, Mamlaka ya Bandari imeongeza sana sana ufanisi katika kazi zake, mapato yameongezeka kutoka shilingi Bilioni 320 mpaka shilingi Bilioni 537 katika kipindi cha miaka miwili” alisema Zitto.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba aliithibitishia kamati na wabunge waliotoa michango yao kuwa wamepokea michango yao na wataifanyia kazi.
“Kwanza nisema ndugu Mwenyekiti, tumewasikia wabunge, tumepokea waliyoyasema na tutayafanyia kazi, tupo kwa ajili hiyo” alisema Naibu Waziri Nchemba.
Alisema tangu mwaka wa fedha ulipoanza, mkakati wa Wizara chini ya usimamizi wa Waziri wa Fedha ilikuwa ni kuhakikisha kila fedha inapokusanywa inakwenda pale ilipokusudiwa.
Alifafanua kuwa hata hoja za baadhi ya wabunge kuwa kuna miradi imepata mgawo sifuri, inawezekana hiyo sifuri ni ya fedha zile zinazotoka nje.
“Naongea hili kwa uhakika, mwaka wa fedha uliooanza tu tulitoa Bilioni 500 kwa ajili ya miradi ya maendeleo na mpaka wizara zingine wakashangaa wakauliza hizi fedha mmekosea au ndivyo kweli zinatakiwa zije” alisema na kuongeza:
“Walidhani ni za mishahara, haikuzoeleka kutokea fedha nyingi ndani ya mwezi wa kwanza wa bajeti kwa ajili ya shughuli za maendeleo”
Hivyo aliwaomba wabunge wazingatie mambo mamwili, moja Waziri ameweka utaratibu kwamba kila taasisi inapopokea fedha za maendeleo  ni lazima ipeleke mrejesho imetumia fedha zile kwa shughul gani na mradi ule uonekane kabla fedha zingine hazijakwenda.
Alisema jambo la pili ni nia ya Serikali kuhakikisha kwamba fedha zilizotengwa kwa ajili ya mifuko na matumizi maalum ya miradi ya maendeleo na kwamba kuanzia mwezi Februari wanarekebisha utaratibu wa kutengeneza mchanganuo wa fedha kuhakikisha fedha hizo zimekwenda kwenye miradi ya maendeleo.
Mkutano wa 18 wa Bunge la Jamhuri unatarajiwa umeahirishwa hadi Jumatatu ambapo bunge hilo linataraji kupokea taarifa za Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira na Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji.

 Spika wa Bunge la Jamhuri, Mhe Anne Makinda akieleza jambo leo Bungeni mjini Dodoma ambapo mkutano wa 18 wa Bunge hilo unaendelea.
 Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji George Masaju akitoa ushauri kwa Bunge la Jamhuri.
 Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti Dkt. Festus Limbu, alijibu hoja za wabunge waliochangia kwenye taarifa yake.


 Naibu Waziri wa Fedha, Mhe Mwigulu Nchemba akijibu hoja za kamati zilizoelekezwa katika wizara yake.
Mbunge wa Kawe, Mhe Halima Mdee akitoa mchango wakati wa kujadili taarifa za kamati za Bunge, bungeni mjini Dodoma. Picha zote na Hussein Makame-MAELEZO, Dodoma

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...