Na: A. Othman

Mshairi nguli na mwalimu mzoefu wa Kiswahili ambaye pia ni mwanasiasa mkongwe kutoka nchini Kenya, Bwana Abdilatif Abdalla amemtembelea mwandishi chipukizi kutoka Zanzibar, Bwana Yussuf Shoka ofisini kwake jijini London mapema wiki hii. Katika ziara yake hiyo fupi Bwana Abdalla alifanya mazungumzo mafupi na mwandishi huyo kuhusu kitabu chake kipya cha ‘Paka wa Binti Hatibu’.

Gwiji huyo ambaye ametumia muda mwingi kufundisha Kiswahili nchini Uingereza na Leipzig, Ujerumani amejinyakulia umaarufu mkubwa zaidi katika tasnia ya ushairi kwa kazi yake iitwayo ‘Sauti ya dhiki’ (1973)’.Sambamba na kazi hiyo Bwana Abdilatif Abdalla ambaye ni Profesa mstaafu wa chuo kikuu cha Leipzig Ujerumani, kwa sasa amekuwa akitembelea sehemu mbali mbali duniani na kutoa mihadhara yake kufuatia mialiko anayoipata.

Bwana Abdalla alifika chuo kikuu cha London, SOAS majira ya mchana wa Jumatatu (5-01-2015) na kukaribishwa na mkuu wa Idara ya lugha na Tamaduni za Afrika ambaye pia ni mwalimu wa Fasihi ya Kiswahili Chuoni hapo, Dr. Alena Rettova ambapo pia alikutana na kufanya mazungumzo mafupi na Mwalimu wa Lugha ya Kiswahili na Tafsiri wa chuo hicho Dr. Chege Githiora.

Katika ziara yake hiyo fupi, Bwana Abdalla alikutanishwa na kutambulishwa kwa mwandishi wa ‘Paka wa Binti Hatibu’ na mwenyeji wake Dr. Rettova ambapo kimsingi mwalimu huyo alitaka kujua kwa kina fasili ya msemo huo na jinsi mwandishi huyo alivyoutumia katika kazi yake hiyo ya sanaa.

Naye, Mwandishi wa kitabu hicho ambaye pia ni mwalimu wa lugha na Fasihi chuoni hapo, Bwana Yussuf Shoka alijadiliana na mtaalamu huyo kwa kina juu ya fasili ya msemo huo na kuhitimisha kwa kusema; ‘Unajua katika utangulizi wa kitabu hiki, mwandishi wa utangulizi Bi Asha Khamis Hamad amesema – ukitaka kujua uhondo wa ngoma ingia ucheze, na ukitaka kujua uhondo wa kitabu hiki kisome’.

Wakati huo huo, Bwana Abdilatif Abdalla alitumia fursa hiyo kumshauri mwandishi huyo chipukizi kuandika kwa kutumia lugha yake ya kawaida yaani lugha ya kimazungumzo:

‘Hakuna haja ya kung’ang’ania usanifu. Andika Kiswahili unachokizungumza katika mazingira ya kawaida. Kiswahili unachozungumza nyumbani na watu wako’. Akiongezea na kutetea hoja yake, Bwana Abdalla alitoa mfano wa Profesa Said Ahmed Muhammed kwa kusema;

‘Watu wengi wanashindwa kufahamu uandishi wa Said Ahmed eti kwa sababu anaandika kwa lugha ya kawaida. Lugha ya kwao. Nami siku zote humwambia endelea kuandika hivyo hivyo, kwani hicho ndicho Kiswahili kinachotumiwa na watu wako.’

Bwana Abdalla pia alimalizia kwa kusema kuwa Kiswahili kimekuwa lugha ya watu wote. Hivyo hakuna haja ya kusema huyu hivi na huyu vile kwani wenye lugha ni watumiaji wa lugha yenyewe.

Mwandishi huyo pia atatembelewa na mwalimu mkongwe na gwiji wa uandishi wa tamthiliya za Kiswahili visiwani Zanzibar, Bwana Farouk Topan mapema wiki hii. Bwana Topan ni profesa mstaafu wa Kiswahili wa chuo kikuu cha London, SOAS ambaye anajulikana zaidi kwa kazi zake za sanaa ya maigizo kama vile Mfalme Juha (1971), Aliyeonja Pepo (1973) na Siri (2000).
Profesa Abdilatif Abdalla akiwa pamoja na Bwana Yussuf Shoka. Kushoto ni Mhadhiri wa Kiswahili na Tafsiri, SOAS Dr. Chege Githiora.
Bwana Yussuf Shoka (Kushoto) akijadiliana jambo na Profesa Abdilatif
Profesa Abdilatif Abdalla akiwa pamoja na Mkuu wa Idara ya Afrika, SOAS Dr. Alena Rettova. Kushoto ni mwandishi wa Paka wa Binti Hatibu Bwana Yussuf Shoka.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 10 mpaka sasa

  1. Sasa huyu Paka wa binti Hatibu si aje atusaidie na tatizo la Panya road jamani.

    ReplyDelete
  2. Leo nimefurahi sana kuona picha ya nguli huyu Bw Abdillatif.

    Alikuja kututembelea Lumumba mwaka 1976 na kutupa maelezo kwa urefu kuhusu kitabu chake cha 'Sauti ya Dhiki' na maana ya baadhi ya mashairi.

    Mfano: kuna mamba mtoni metakabari, ajigamba na kujiona hodari, yuwaamba kwamba taishi dahari.

    Akumbuke siku yake ikifika, roho yake ajue itamtoka... (beti nyengine nimesahau)

    Na Farouk Topan tulisoma kitabu chako 'aliyeonja pepo' enzi zile.

    Tunashukuru sana kwa michango yenu kwenye lugha hii adhimu.

    ReplyDelete
  3. Hongera Sana. Jamaa kafanana na Yusuf Hamad jamani. Nilisoma naye kulee University of Zanzibar.

    ReplyDelete
  4. Mdau wa mwanzo kabisa hapo juu, usinipe kucheka sasa. Laitani ungejuwa hali ya huyo 'Paka wa binti Hatibu' hata nzi awe mbele yake hawezi kumuinga ataweza wapi kuja kutusaidia hilo tatizo la hao Panya Road watu,...lol




    ReplyDelete
  5. Yussuf Shoka ndiye huyo huyo Yussuf Hamad. Kule ulaya anajulikana kama Yussuf Hamad na huku ni Yussuf Shoka ila jina lake kamili ni Yussuf Shoka Hamad

    ReplyDelete
  6. Yusuf Hamad mwalimu yangu ya Kiswahili. Yeye hajui fundisha. Yeye mbaya mwalimu.

    ReplyDelete
  7. How great to see Chege with a small Afro now! Alena is a great philosophical teacher. When I was there I was taught translation by Ida. Where is she? Great topic! Kiswahili oyeeee.

    ReplyDelete
  8. daahh namkumbuka mwalimu wangu wa BE
    Hongera sana

    ReplyDelete
  9. daah hongera saana mwalimu wangu

    ReplyDelete
  10. Shukrani gwiji Abdilatif Kwa kuchangia malezi na makuzi ya Kiswahili. Naienzi diwani ya sauti ya dhiki.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...