Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Halima Dendegu (aliyenyoosha mkono), akimwonyesha Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene, jinsi maji ya bahari yalivyoathiri eneola MnaziBay, karibu na kampuni ya kuzalisha umeme ya Maurel & Prom.

Athari ya mmomonyoko wa ardhi katika eneo la MnaziBay inavyoonekana pichani. Mmomonyoko huo umetishia usalama wa Kiwanda cha kufua umeme unaotumiwa na wakazi wa Lindi na Mtwara cha Maurel & Prom.

Na Veronica Simba aliyekuwa Mtwara Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Halima Dendegu ameushukuru uongozi wa Wizara ya Nishati na Madini kwa ushirikiano ilioonyesha katika zoezi linaloendelea kudhibiti kasi ya maji Pwani ya Mnazi Bay, yaliyosababisha mazingira ya hatari kwa bomba la gesi na kiwanda cha kuchakata gesi asilia cha Maurel & Prom.

Alitoa shukrani hizo hivi karibuni wakati wa ziara ya Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene mkoani humo kukagua miradi mbalimbali inayosimamiwa na Wizara yake hususan Mradi wa bomba la gesi asilia kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam.

“Kazi iliyofanyika imewezesha kudhibiti kasi ya maji kuendelea kumega sehemu ya ardhi iliyobaki. Kazi ya kudhibiti kingo za bahari inaendelea vizuri na tunashukuru uwezeshaji wa haraka uliofanywa na Wizara na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC),” alisema Dendegu.

Akielezea hali halisi iliyopo sasa baada ya jitihada zilizofanywa kukabiliana na janga hilo, Dendegu alisema kiwanda cha kuchakata gesi asilia cha Mnazi Bay kinachoendeshwa na kampuni ya Maurel & Prom, kinaendelea kuzalisha gesi na Mikoa ya Lindi na Mtwara inaendelea kupata umeme.

Kwa upande wake, Waziri Simbachawene alipongeza jitihada zilizofanywa na uongozi wa Mkoa wa Mtwara kusimamia zoezi zima la kuzuia mmonyoko wa ardhi katika kingo za bahari, Pwani ya Mnazi Bay. “Nawapongeza wenzetu, mmejitahidi. Mmefanya kazi kubwa kuokoa mali ya taifa,” alisema.

Janga hilo la mmomonyoko wa ardhi, Pwani ya Mnazi Bay lilitokana na mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali na kusababisha kujaa kwa maji katika Pwani hiyo tofauti na hali ilivyo siku zote.

Kujaa huko kwa maji kulisababisha mazingira ya hatari kwa bomba la gesi la inchi 16 ambapo ilibakia mita nne tu maji hayo kulifikia bomba hilo. Aidha, hali hiyo ya kujaa maji pia ilisababisha mazingira ya hatari kwa kiwanda cha kuchakata gesi asilia cha Mnazi Bay kinachoendeshwa na kampuni ya Maurel & Prom Tanzania (M&P) ambapo zilibaki mita 29 tu maji kufikia kiwanda hicho.

Kiwanda hicho ndicho kinachochakata gesi inayoendesha mitambo ya Tanesco iliyopo Mtwara Mjini na umeme wake kutumiwa na wananchi wa mikoa ya Lindi na Mtwara.

Makundi ambayo yamekuwa mstari wa mbele kushirikiana kukabiliana na janga hilo ni pamoja na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jeshi la Polisi, na Jeshi la Magereza.

Mengine ni Kampuni ya Dangote, Kampuni ya Maurel & Prom Tanzania, Shirika la Petroli Tanzania (TPDC), Wizara ya Nishati na Madini na Wataalam kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...