Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) lenye dhamana ya kufufua, kukuza na kuendeleza Sanaa kwa kushirikiana na taasisi ya Ako’mungoma Poverty Alleviation Organization (APAO) linaendesha programu ya wiki tatu ya Sanaa kwa watoto katika Wilaya ya Temeke Mkoani Dar es Salaam. 

Kwa mujibu wa Sera ya Taifa ya Utamaduni ya mwaka 1997 sura ya 9.6.16 Baraza linaelekezwa kushirikiana na wadau katika kuendesha matukio mbalimbali ya sanaa  kama programu hii ya watoto. 

Programu hii ya Sanaa kwa watoto ambayo kilele chake kitakuwa tarehe 07/03/2015 na kuhusisha  maonesho, inatarajia kushirikisha watoto 215 ambapo 100 wanaishi katika mazingira magumu eneo la Mbutu - Kigamboni na wengine 100 kutoka shule za Msingi Gomvu na Mbutu. Aidha, watakuwepo wanafunzi waalikwa 15 kutoka shule ya msingi Msimbazi iliyopo wilaya ya Ilala. 

Programu hii ambayo mwaka huu inadhaminiwa na Kampuni ya Mohamed Enterprises na Haakneel production (T) Ltd inalenga kukuza vipaji vya watoto katika fani za uchoraji, maigizo hususan majigambo na ngoma za asili. Pia tunatarajia udhamini toka wadau na makampuni mengine. 

Kilele cha programu hii yenye kauli mbiu ya “Amani na Uchaguzi 2015” kitapambwa na burudani ikiwemo mpira wa miguu kutoka kwa watoto wa Kituo cha APAO na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoka jimbo la Kigamboni Mheshimiwa Faustine Ndugulile.

Aidha programu hii ni mwendelezo wa programu ya Sanaa kwa watoto ya Baraza iliyoanza tangu miaka ya 80 ambayo ilipata kuibua na kukuza vipaji vya wasanii kama Mrisho Mpoto na Masoud Kipanya ambao hadi sasa wanafanya vizuri. 

Kwa mwaka 2014 programu hii iliendeshwa katika wilaya ya Ilala kwa kushirikisha shule tano (5) ikiwemo ya Buguruni Viziwi na ilidhaminiwa na kampuni ya Msama Promotion. 

Baraza linachukua fursa hii kuwaalika wananchi na wadau wote wa sanaa kufika kwa wingi kushuhudia vipaji vya sanaa walivyonavyo watoto.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...