WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema mkoa wa Mbeya unaweza kupaa kiuchumi kama utazingatia fursa za kibiashara ilizonazo na kuwekeza zaidi kwenye viwanda vya usindikaji mazao ya kilimo na mifugo.

Ametoa kauli hiyo  jana (Jumatatu, Machi 2, 2015) wakati akizungumza na viongozi mbalimbali wa mkoa wa Mbeya waliofika kusikiliza majumuisho ya ziara yake ya siku saba kwenye mkoa huo. Mkutano huo ulifanyika kwenye ukumbi wa Mkapa, jijini Mbeya.

“Nguvu kubwa mnayo katika biashara hasa kama mtajitahidi kutumia vema fursa kubwa ya uwekezaji katika viwanda vya kuongeza thamani kwenye mazao ya kilimo na mifugo mliyonayo,” alisema.

Waziri Mkuu alisema mkoa wa Mbeya katika msimu wa 2013/2014 umeweza kuzalisha tani 4,159,907 za nafaka na kuuwezesha kuwa na ziada ya chakula ya tani 3,347,680.

Hata hivyo, Waziri Mkuu alisema mkoa wa Mbeya bado una fursa nzuri ya kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara na unaweza kuiwezesha kama nchi kuuza chakula katika masoko ya Afrika na Afrika ya Mashariki kama watajipanga vizuri.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu aliwapongeza viongozi hao kwa kuuwezesha mkoa wa Mbeya kutoa mchango mkubwa katika Pato la Taifa. “Katika taarifa ya mkoa, nimeelezwa kuwa mwaka 2013, mkoa huu ulichangia shilingi trilioni 3.951 na hivyo kushika nafasi ya tatu kati ya mikoa yote nchini ikitanguliwa na mikoa ya Dar es Salaam na Mwanza.”

Alisema kutokana na ukuaji wa kasi wa idadi ya watu ambao ni asilimia 2.7, mtu akichukua pato hilo la mkoa na kuligawanya kwa idadi ya watu wa mkoa wa Mbeya anapata wastani wa pato la kila mwananchi kuwa ni sh. 1,420,427. “Kipato hicho, ni sawa na shilingi 118,369 kwa mwezi au shilingi 3,946 kwa siku sawa na Dola za Kimarekani (US $) 2.3,” alifafanua.

Waziri Mkuu alibainisha kwamba mtu akichukua wastani wa pato la kila mwananchi kwa mwaka 2013 na kupanga kwa mikoa yote, mkoa wa Mbeya unashuka na kushika nafasi ya sita kitaifa. Aliitaja mikoa inayowatangulia kuwa ni Dar es Salaam sh. 1,990,043/- ambao ni wa kwa kwanza; wa pili ni Iringa (sh. 1,660,532/-); wa tatu ni Arusha (sh. 1,448,782/-); wa nne ni Kilimanjaro (sh. 1,444,882/-); wa tano ni Ruvuma (sh. 1,438,392/-) na wa sita ni Mbeya (sh. 1,420,427/-).

“Nawashauri muongeze juhudi za kuipita mikoa hiyo kwa kuwa mna fursa nyingi za kuongeza uzalishaji hasa katika mazao ya kilimo cha kahawa, kakao, mpunga, mahindi, viazi, pamoja na mazao ya maliasili kama vile mazao ya misitu, na uvuvi na uchimbaji madini,”.

Waziri Mkuu amemaliza ziara yake ya siku saba mkoani Mbeya leo kwa kufanya majumuisho ya ziara yake na amerejea jijini Dar es Salaam jana jioni (Jumatatu, Machi 2, 2015) .

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. Hongereni Mbeya! Sasa mfute hilo wazo la kuugawa Mkoa. Mbaki kama mlivyo, mjipange kama alivyosema na kuwashauri Waziri Mkuu ili mpae kiuchumi kwa manufaa ya wote. Acheni hizi njaa za watu wachache wanaotafuta madaraka na umaarufu kwa kuwagawa.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...